1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TOKYO: Waziri wa kilimo wa Japan ajinyonga

28 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBxF

Waziri wa kilimo wa Japan, Toshikatsu Matsuoka, amefariki dunia baada ya kujinyonga nyumbani kwake mjini Tokyo.

Waziri huyo alikuwa amekanusha madai ya kufanya makosa katika kashfa ya kudhamini shughuli za kisiasa na alitarajiwa kuhojiwa zaidi na bunge la Japan katika kikao chake cha leo mjini Tokyo.

Jeffrey Kingston wa chuo kikuu cha Temple nchini Japan amesema, ´Kashfa dhidi ya waziri aliye serikalini kila mara imekuwa ikichukuliwa na uzito mkubwa. Hali iliyomkabili waziri Matsuoka wa kitengo cha kikonsavativ cha chama cha LDP, ya mara kwa mara kuhusishwa kwenye kashfa katika miezi kadhaa iliyopita, bila shaka imekuwa jambo la kumtatiza.´

Wiki iliyopita waongozaji mashtaka waliwatia mbaroni maafisa wawili wa serikali kuhusiana na kashfa hiyo.

Kifo cha waziri Matsuoka kinaongeza matatizo yanayomkabili waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe, ambaye uungwaji mkono wake miongoni mwa wananchi umepungua huku uchaguzi ukikaribia kufanyika mwezi Julai mwaka huu.

Baraza lake la mawaziri tayari limekuwa likikabiliwa na hasira ya wananchi kwa usimamizi mbaya wa malipo ya uzeeni na wakala wa bima ya jamii ya serikali ya Japan.