1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tofauti yazuka miongoni mwa nchi za Afrika kuhusu teknologia ya kubadilisha asili ya viumbe

Mwakideu, Alex15 Mei 2008

Kenya imeamua kufanya utafiti zaidi kabla ya kukata kauli kuhusu sheria itakayolinda viumbe na vitu vyote vinavyoishi

https://p.dw.com/p/E0Tu
wanyama walioboreshwa katika teknologia ya bayo anuaiPicha: Laura Spurway / DW

Tofauti imezuka miongoni mwa nchi za Africa katika mjadala wa kutafuta suluhu juu ya malipo kwa nchi zinazoathiriwa na teknologia mpya ya  kuboresha mbegu kwa minajili ya kupata mazao makubwa zaidi.


Kampuni kubwa duniani zinazoendesha teknologia hiyo zinapendekeza makubaliano ya hiari badala ya sheria ya kimataifa kuhusu malipo ya fidia kwa nchi zinazoathirika.


Siku tatu baada ya kikao hicho kinachoendelea hapa mjini Bonn kuanza rasmi, tofauti kuhusu kuundwa kwa sheria itakayoongoza dunia juu ya teknologia hiyo ya kuboresha mbegu ingali miongoni mwa wajumbe.


Takriban wajumbe 2000 wanaowakilisha serikali na mashirika yasiokuwa ya kiserikali wanahudhuria kikao hicho kitakachochukua siku tano.


Kikao chenyewe kinachohudhuriwa na nchi zilizokubaliana kulinda viumbe na vitu vinayoishi kinatarajiwa kutunga sheria zitakazolinda ubadilishaji wa asili ya mchele au mahindi au pia maharagwe kwa minajili ya kusababisha zao kubwa zaidi la nafaka hizi.


Nchi kadhaa za Africa zinapendekeza kulipwa iwapo sayansi hii itatumika na mataifa mengine na kuleta hasara.


Duru kutoka kwa kikao hicho zinasema wajumbe walilazimika kujadiliana kuhusu swala hili hadi usiku wa manane bila kupata suluhu.


Wajumbe wengine kutoka Ethiopia na Zimbabwe ambao hawakutaka kutajwa majina yao wamesema walishangazwa na wajumbe wa Kenya ambao waligeuza kauli yao na kupinga hatua ya kuundwa kwa sheria hiyo ya kimataifa itakayolinda uboreshaji wa mimea.


Hata hivyo mwenyekiti wa ujumbe wa Kenya Harrison Kamau ambaye ni katibu mkuu anaehusika na sayansi ya kulinda viumbe na vyote vinavyoishi amesema Kenya inahitaji wakati wa kutafakari msimamo wake kama nchi na kufanya utafiti zaidi juu ya teknolojia hii mpya.


Mkurugenzi mkuu wa uhifadhi wa mazingira na utumizi bora wa mali ya asili katika wizara ya mazingira nchini Ujerumani Jochen Flasbarth amesema sheria hiyo ingali inapingwa vikali. Jechen amesema "Kando na kampuni kuna nchi ambazo pia lazima zishawishiwe kuhusu uundwaji wa sheria hiyo, lakini mwishoe mjadala wetu hata kwa kampuni za ujerumani, ni iwapo unataka kupata mali ya asili ya genetiki basi lazima ukubali kugawa mazao utakayopata la sivyo nchi zenye bayo anuai zinatakapinga kushiriki katika siku za usoni"


Kampuni sita za kimataifa Bayer CropScience, Dow AgroSciences,

DuPont/Pioneer, Monsanto na Syngenta zimepinga sheria hiyo na zinapendekeza maelewano ya hiari kati yake na nchi husika.


Hata hivyo makundi kadhaa ya mazingira yakiwemo yameshutumu mpango huo. Juan Lopez ambaye ni mshirikishi wa kundi la Friends of the Earth (FoE) ameushutumu akisema hautaleta uajibikaji iwapo uboreshaji wa mimea utaleta hasara.


Jochen anasema lengo la kupunguza uharibu wa vitu na viumbe vinavyoishi ifikapo mwaka wa 2010 ambalo liliafikiwa mwaka wa 2002 na viongozi 110 wa mataifa na serikali huenda lisifaulu. "Kile tunachoona leo ni kwamba tungali katika njia mbaya na lengo hilo la 2010 halionekani likiwa la muhimu kusema kweli pia tunapaswa kukagua, mifano ya nchi na majimbo yaliyofaulu kulinda mazingira yake ipo wapi na je tulikosea wapi na ukaguzi huu ndio utakaotusaidia kutengeneza vifaa vipya vitakavyotusaidia kufanya vyema zaidi baada ya mwaka wa 2010" Hayo yalisemwa na Jochen,.


Miongoni mwa mada zinazojadiliwa katika kikao cha kulinda mazingira ni Mada katika kikao cha kulinda mazingira uharibifu wa misitu inayosababisha mvua, bahari na pia njia za kukabiliana na kupotea kwa bayo anuai.


Kikao hicho kitaendelea hadi mei tarehe 16.