1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TI: Rushwa imeongezeka Afrika

Admin.WagnerD1 Desemba 2015

Rushwa inaathiri maendeleo katika mataifa ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara , ambako watu wanaokadiriwa kufikia milioni 75 wametoa rushwa katika mwaka mmoja uliopita.

https://p.dw.com/p/1HFQa
Logo Transparency International
Nembo ya Transparency International

Hayo yamesemwa na shirika la kimataifa la uchunguzi wa masuala ya rushwa la Transparency International katika ripoti iliyochapishwa leoJumanne (01.12.2015).

Mataifa ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara lina jumla ya watu milioni 973, kwa mujibu wa benki ya dunia.

Südafrika Protest gegen Korruption
Maandamano nchini Afrika kusini kupinga rushwaPicha: picture-alliance/dpa/K. Ludbrook

Kiasi ya asilimia 22 ya Waafrika ambao wametafuta huduma za umma katika kipindi cha miezi 12 iliyopita wametoa hongo, kwa mujibu wa shirika hilo linaloangalia masuala ya rushwa katika ripoti yake, ambapo watu 43,143 wamehojiwa.

Polisi na mahakama zinahusishwa kwa kiwango kikubwa katika rushwa. Polisi mara nyingi wanalipwa ili , "kupuuzia uhalifu wowote, hata ikiwa ni mkubwa kiasi gani na wa kutisha," limesema shirika hilo la Transparency International. Shirika hilo limetoa mfano wa msichana wa miaka 9 nchini Zimbabwe ambaye mtu aliyembaka alimuambukiza virusi vya ukimwi na aliachiwa baada ya kutoa rushwa.

Rushwa imeongezeka

Wakati baadhi ya watu wanatoa rushwa kuepuka adhabu kwa uhalifu waliofanya, wengine wanalazimishwa kutoa rushwa ili kupata huduma muhimu ambazo wanazihitaji sana," ripoti hiyo imesema.

Südafrika Proteste gegen die Korruption
Maandamano yanaongezeka barani Afrika kupinga rushwaPicha: Getty Images/AFP/G. Guercia

Karibu asilimia 60 ya wale waliohojiwa wamesema rushwa imeongezeka katika muda wa mwaka mmoja uliopita. Hii imetokea zaidi nchini Afrika kusini , ambako asilimia 83 wameripoti ongezeko la rushwa.

Raia wa Sierra Leone, Nigeria, Liberia na Ghana wameshuhudia viwango vya juu vya rushwa.

Katika nchi zote 28 zilizochunguzwa , polisi , wakuu wa shughuli za kibiashara , maafisa wa serikali na mahakama wote wanaonekana kuwa wala rushwa, ambapo watu milioni 75 wanakadiriwa kuwa walitoa hongo katika mwaka mmoja uliopita.

Uchunguzi huo pia umeeleza kwamba wakati ulipozuka ugonjwa hatari wa Ebola nchini Liberia na Sierra Leone, rushwa huenda imechangia serikali kuchukua hatua za kujivuta mno katika kupambana na ugonjwa huo.

"Katika nchi hizo mbili kuna viwango vya juu vya ulaji rushwa na sekta ya binafsi inafikiriwa kwamba imeathirika na viwango vikubwa vya rushwa," umesema uchunguzi huo.

Südafrika Privates Anwesen Präsident Jacob Zuma
Nyumba za binafsi za rais Zuma wa Afrika kusini katika kijiji cha Nkandla zilizokarabatiwa kwa fedha za serikaliPicha: AFP/Getty Images

Kuna mafanikio pia

Kwa upande unaotoa picha nzuri, Botswana imepata alama nzuri, ikiwa na asilimia 54, ikiashiria kwamba serikali yao inafanya vizuri kupambana na rushwa.

Ni asilimia 20 tu ya raia wa Afrika kusini wanasema wanamtazamo kama huo.

Afrika kusini imetikiswa na kashfa kubwa za rushwa katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na matumizi makubwa ya fedha za umma kukarabati nyumba ya binafsi ya rais Jacob Zuma.

"Watu wamekasirishwa, wanaona matumizi hayo makubwa kama sehemu ya rushwa katika serikali," David Lewis, mkurugenzi wa shirika la nchi hiyo linaloangalia masuala ya rushwa, Corruption Watch, ameliambia shirika la habari la AFP.

Madagascar imekuwa chini kabisa , ikiwa na asilimia 9, katika juhudi za serikali kupambana na rushwa.

Karim Wade Minister Sengal Prozess Anklage 2013
Mtoto wa rais wa Senegal Karim Wade akiwasili mahakamani katika kesi ya rushwaPicha: AFP/Getty Images

"Rushwa husababisha na kuongeza umasikini na kuachwa nyuma kwa sehemu ya jamii," mkuu wa Transparency International Jose Ugaz amesema katika taarifa.

Amesema hatua za watu kujitokeza kufichua rushwa ni muhimu katika mapambano dhidi ya tatizo hilo, lakini watu wanaogopa kujitokeza kwa kuwa wanahisi kwamba ni "hatari sana, ama haisaidii".

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / dpae

Mhariri: Daniel Gakuba