1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Thuluthi moja ya watu duniani wana matatizo ya maji

22 Machi 2018

Huku idadi ya watu duniani ikiongezeka, ndivyo mahitaji ya maji kwa ajili ya viwanda, kilimo na matumizi ya nyumbani yanavyoongezeka. Ukataji wa miti na uchafuzi wa maji ni mambo yanayowekea shinikizo vyanzo vya maji.

https://p.dw.com/p/2ukxt
UN-Weltwassertag 22.03.2018
Picha: Getty Images/AFP/M. Abdiwahab

Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba zaidi ya thuluthi moja ya idadi ya watu duniani tayari wanakabiliwa na matatizo ya kupata maji.

Katika mji wa Cape Town Afrika Kusini watu milioni 4.5 wanakabiliwa na ukame. Milolongo mirefu inashuhudiwa katika kituo cha manispaa cha kutoa maji ambapo kila mkaazi anatakiwa kupata lita 25 tu za maji kwa siku. Polisi wanaweka ulinzi kuhakikisha kwamba hakuzuki machafuko. Utawala na wakaazi wana matumaini kwamba msimu ujao wa mvua utasaidia kuyajaza mabwawa.

Hali ya Cape Town ni mbaya ila hakuna bara ambalo halikabiliwi na uhaba wa maji. Katika mji wa Zagora huko Morocco kulikuwa na maandamano yaliyoibua vurugu msimu uliopita wa mapukutiko kutokana na uhaba wa maji wakati ambapo kiwango cha joto kilikuwa kimepanda na kufikia nyuzi 40.

Hali ni mbaya kutokana na mabadiliko ya tabia nchi

Nchini Uhispania na Ureno kiwango cha maji katika hifadhi za maji kimefika chini mno kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Kilimo Uhispania kinatumia asilimia 85 ya maji yanayotumika kitaifa.

Syrien Wasserkrise in Damaskus
Raia mmoja wa Syria akikinga maji katika mji wa DamascusPicha: picture-alliance/dpa/EPA/Y. Badawi

Mabadiliko ya tabia nchi yanafanya hali kuwa mbaya zaidi. DW imefanya mahojiano na Ines Dombrowsky ambaye ni afisa kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Ujerumani na alikuwa na haya ya kusema kuhusiana na hali ya maji ilivyo sasa hivi duniani.

"Suala la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi tayari limezingatiwa katika mipango ya kitaifa," alisema Dombrowsky, "kuna mikakati muhimu ambayo imewekwa hasa katika visa vya ukosefu wa maji vinavyohitaji kushughulikiwa kwa haraka hasa katika nchi zinazoendelea na zile zilizo na uhaba wa maji," aliongeza afisa huyo.

Dombrowsky  anakiri kwamba kuna changamoto hasa katika kukabiliana na athari za tabia nchi kwani kiwango cha uvunaji na matumizi bora ya maji kwa sasa kiko chini mno duniani.

Ujerumani ina maji mengi kwa ajili ya wananchi wake kupita kiasi

Amesema Singapore ndiyo mfano mzuri katika suala hilo akidai kwamba zaidi ya raia milioni tano na nusu wa nchi hiyo wanapata maji yao ya kunywa kutokana na maji machafu ambayo yamesafishwa vizuri kwa kutumia kemikali.

Sambia Energiekrise - Wasser
Msichana akiteka maji mferejini huko Bauleni ZambiaPicha: DW/J. Jeffrey

Kulingana na shirika la mazingira la Ujerumani, nchi hii imebarikiwa na wingi wa maji kwani takwimu zilizopo zinaonesha hifadhi ya maji iliyopo inazidi matumizi ya maji ya Wajerumani, matumizi ya viwanda na hata kilimo. Idadi kubwa ya watu duniani wangekuwa wenye furaha kama wangekuwa wanapata maji vyema kama hali ilivyo Ujerumani.

Katika mojawapo ya malengo ya Umoja wa Mataifa katika ruwaza yake ya mwaka 2030 ni upatikanaji wa maji kwa kila mmoja na matumizi yake mazuri. Upatikanaji wa maji kwa kila mmoja ni muhimu zaidi ili kuyafanikisha malengo yote kumi na saba yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Helle Jeppesen

Tafsiri: Jacob Safari

Mhariri: Yusuf Saumu