1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haki za raia wa pande zote mbili zitaheshimiwa

22 Julai 2016

Rais Francois Hollande wa Ufaransa amemhimiza waziri mkuu wa Uingereza Theresa May aharakishe mazungumzo ya kujitoa nchi yake kutoka Umoja wa Ulaya,ingawa amekiri kwamba bibi May anahitaji muda kuratibu talaka hiyo.

https://p.dw.com/p/1JU9v
Rais Hollande akimkaribisha waziri mkuu wa Uingereza bibi May katika ikulu ya ElyséePicha: Getty Images/AFP/S. de Sakutin

Siku moja baada ya kansela Angela Merkel wa Ujerumani kuunga mkono wito wa waziri mkuu wa Uingereza Theresa May wa kupatiwa wasaa kidogo wa kuandaa mazungumzo rasmi yatakayoitoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya ,waziri mkuu huyo wa Uingereza amejipatia pia ridhaa ya rais wa Ufaransa Francois Hollande ya kutuma maombi rasmi ya kujitoa ifikapo mwisho wa mwaka huu. Lakini rais Francois Hollande anaekabwa na shinikizo kufuatia shambulio la kigaidi la Nice, amesisitiza hata hivyo kwa kusema tunanukuu" bora ikiwa haraka,kwa masilahi ya pande zote,Umoja wa Ulaya,Uingereza na kwa shughuli za kiuchumi za pande zote mbili.

Theresa May atahakikisha haki za rais wa Umoja wa ulaya zinaheshimiwa Uingereza kama za waingereza zitaheshimiwa Ulaya

Katika mkutano na waandishi habaria mwishoni mwa mazungumzo yao, waziri mkuu wa Uingereza Theresa May ametilia mkazo umuhimu wa kuendelezwa mazungumzo ya kujitoa nchi yake kutoka Umoja wa ulaya kwa utulivu na kwa njia ya maana.Amesema atahakikisha haki za raia wa nchi za Umoja wa Ulaya wanaoishi Uingereza zinaheshimiwa,Uingereza itakapotoka katika Umoja huo. Waziri mkuu Theresa May anaendelea kusema:"Kwa kuwazingatia wafaransa wanaoishi Uingereza wakati tukiwa wanachama kamili wa Umoja wa Ulaya,bila ya shaka hakutakuwa na mabadiliko yoyote ,au kwa waingereza wanaoishi Ufaransa au katika nchi wanachama wa Umoja wa ulaya. Siku za mbele nnataka kuwa na uwezo wa kudhamini haki za wakaazi wa Umoja wa Ulaya wanapishi Uingereza na ningependelea kuwa na uwezo wa kufanya hivyo-njia pekee itakayopelekea hayo yasiwezekane ni kama haki za raia wa Uingereza wanaoishi atika mataifa ya Umoja wa Ulaya hazitalindwa."

Deutschland Berlin Angela Merkel und Theresa May
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: picture alliance/AP images/Sight

Uingereza pekee ndiyo itakayoamua lini kukitumia kifungu nambari 50 cha makubaliano ya Umoja wa Ulaya kuhusu kujitoa katika Umoja huo. Maombi rasmi yatakapotolewa tu,majadiliano yataanza na kumalizika miaka miwili inayokuja,ikimaanisha Uingereza itatoka rasmi mwaka 2019.

Akiwa ziarani jumatano iliyopita mjini Berlin,Theresa May alisema nchi yake haitotuma maombi rasmi ya kujitoa kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Enzi mpya baada ya Brexit

Baada ya kura ya Brexit,rais Hollande , kansela Angela Merkel na waziri mkuu wa Italy Matteo Renzi walitoa wito mjini Berlin wa kubuniwa"enzi mpya barani Ulaya."Viongozi hao watatu wanapanga kukutana tena Agosti 22 nchini Italy.

Paris Westbalkan Konferenz Merkel und Hollande
Kansela Angela Merkel na rais Hollande wa UfaransaPicha: picture-alliance/dpa/E. Laurent

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga