1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya watoto CAR wakosa masomo

11 Mei 2016

Maelfu ya watoto katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wanakosa masomo wakati shule zikifanya jitihada za kufunguliwa upya kutokana na machafuko. Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya watoto, UNICEF.

https://p.dw.com/p/1Iinv
Französische Soldaten in der Zentralafrikanischen Republik
Picha: AFP/Getty Images/M.Medina

Moja kati ya shule nne za msingi katika nchi hiyo iliyoathiriwa na mizozo, yenye shule takriban 500 hazina wanafunzi, na theluthi moja ya watoto walio katika umri wa kwenda shule, hawahudhurii masomo, taarifa ya UNICEF imesema.

Jamhuri ya Afrika ya Kati imekuwa katika machafuko baina ya kundi kubwa la waislamu, walioasi serikali la Seleka na wapiganaji wa kikristu wa Anti Balaka, tangu waasi hao walipomwondosha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Francois Bozize, mwaka 2013.

Wakati waangalizi wengi wakitumai kuchaguliwa hivi karibuni kwa rais mpya wa nchi hiyo, Faustin-Archange Touadera, kutachangia kumaliza machafuko, hali ya usalama bado imeendelea kuwa ya wasiwasi, kama mashirika ya Umoja wa mataifa yanavyosema.

"Kurejea kwa shughuli za masomo ni changamoto kubwa, wakati ambapo takriban asilimia 20 ya idadi ya watu nchini humo, wanaofikia Milioni 4.6 wakiwa wamehamishwa kutoka kwenye makazi yao" amesema mwakilishi mkazi wa UNICEF, nchini Afrika ya Kati, Mohamed Malick Fall.

Fall ameliambia shirika la misaada la Thomson Reuters, kwamba bado kuna masuala ya usalama na masuala ya shule kuweza kufikiwa, lakini pia hali ya hatari inayowakabili watoto wanapokwenda shule, na upungufu wa watumishi wa umma pamoja na walimu walioyakimbia maeneo yao.

Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin-Archange Touadera
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin-Archange TouaderaPicha: Reuters/S. Modola

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi, UNHCR, limesema mzozo huo umesababisha raia 400,000 kukimbia nchini humo, na wengine takriban nusu milioni kuomba ukimbizi katika nchi jirani za Chad, Cameroon na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

UNICEF, imeendelea kutoa vifaa vya kufundishia na kuwafunza maelfu ya watoto waliohama makazi yao ili wasiendelee kubaki nyuma kimasomo. Hata raia walioyahama makazi yao pia wanajitolea kufundisha, amesema Fall.

"Wanaweza kuwa hawana msingi mzuri wa kitaaluma ama mafunzo, lakini inaonyesha uthabiti wa watu hawa na jamii nzima katika kuhakikisha watoto hawakosi masomo" aliongeza Fall.

Walimu hupata taaluma ya kuwezesha wanafunzi kisaikolojia kurejea katika hali ya kawaida kwa kuwa wanafunzi wengi wamepata kiwewe kwa kuwa wameathirika na matokeo ya baada ya vita, UNICEF imesema. Wapo baadhi ya watoto waliokuwa wakiona haya na wengine walikataa kuzungumza, wakati wengine walikuwa wajeuri na mara nyingine walitoa silaha tayari kuzitumia, baadhi ya walimu wameuambia Umoja wa Mataifa.

Mpiganaji wa Anti-Balaka
Mpiganaji wa Anti-BalakaPicha: Getty Images/AFP/I. Lieman

Fall anasema ana imani kuwa shule zitafunguliwa tena, ili kusaidia kuwalinda watoto kutokana na machafuko, kusajaliwa katika makundi ya wapiganaji na unyanyasaji wa kingono. Takriban asilimia 40 ya shule zilikuwa zimefungwa wakati wa kilele cha mzozo kutokana na mashambulizi, uporaji na uvamizi wa wapiganaji wenye silaha.

Siku ya Jumatano shirika la UNICEF limeweka wazi mafungu ya fedha kwa ajili ya kuwasaidia watoto kurejea madarasani wakati wa dharura, na lengo ni kuwafikia watoto milioni 13.6, walio katika umri wa chini ya miaka mitano, na hatimaye watoto Milioni 75, ifikapo mwaka 2030.

Mwandishi: Lilian Mtono/rtre

Mhariri: Josephat Charo