1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

THE HAGUE:Charles Taylor akataa kufika mahakamani

4 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBuv

Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor amekataa kufika mahakamani katika ufunguzi wa kesi yake ya uhalifu wa kivita.Katika waraka wake uliosomwa mahakamani na wakili wake Karim Khan,Bwana Taylor anasusia kikao hicho kwa kuamini kuwa hatatendewa haki katika mahakama hiyo maalum.Kwa upande wake anadai kuwa ana mtetezi mmoja pekee ikilinganishwa na tisa wa upande wa mashtaka.

Bwana Taylor ni kiongozi wa kwanza wa taifa barani Afrika kujibu mashtaka ya uhalifu wa kivita mbele ya mahakama ya kimataifa.Mahakama hiyo maalum ya Sierra Leone inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ndiyo itakayosikiza kesi hiyo.Bwana Taylor aliye na umri wa miaka 59 anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita na dhidi ya ubinadamu uliotendeka wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone mwaka 91-2001.

Takriban watu laki mbili walipoteza maisha yao katika vita hivyo huku waasi wakiwachinja na kuwakatakata maelfu ya wakazi wa taifa hilo la Afrika magharibi.Kwa mujibu wa mashtaka yanayomkabili Bwana Taylor aliwafadhili na kuwapa mafunzo na silaha waasi wa Revolutionary United Front, RUF wanaodaiwa kutekeleza vitendo vyote vya kikatili ili kupata almasi.Taylor kwa upande wake anakanusha madai yote hayo.

Kesi hiyo inatarajiwa kumalizika baada ya kipindi cha miezi 18 kabla mwisho wa mwaka 2008.

Endapo kiongozi huyo anapatikana na hatia,sheria za nchi ya Sierra Leone zinaeleza kuwa Bwana Taylor atafungwa kwa miaka kadhaa bila muda maalum kuwekwa.Katika makubaliano ya kesi yake kusikilizwa Uholanzi,endapo Taylor anahukumiwa atatumikia kifungo chake katika jela ya Uingereza.