1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Thailand yatangaza hali ya hatari

P.Martin2 Septemba 2008

Waziri Mkuu wa Thailand ametangaza hali ya hatari mjini Bangkok baada ya maelfu ya wapinzani na wafuasi wake,kupambana mitaani katika machafuko mabaya kabisa tangu zaidi ya mwongo mmoja uliopita.

https://p.dw.com/p/F9lQ
Thai soldier stand guard with shields as they block a street to avoid clash between Thai pro-government protestors and anti-government protesters near the Government House, in Bangkok in the early morning of Tuesday, Sept 2, 2008.Thailand's prime minister declared a state of emergency in the capital Tuesday after street fighting overnight between opponents and supporters of the government left one man dead and dozens of people injured.(AP Photo/Wason Wanichakorn)
Polisi walinda barabara kuzuia mapambano kati ya wafuasi na wapinzani wa serikali karibu na jengo la serikali mjini Bangkok,02 Septemba,2008.Picha: AP

Waziri Mkuu wa Thailand Samak Sundaravej ameamua kutangaza hali ya hatari,baada ya mapambano makali ya usiku kucha,kati ya wapinzani na wafuasi wa serikali,kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine 44.Vile vile amewataka wapinzani waliovamia jengo la serikali tangu juma moja lililopita,waondoke bila ya kusababisha machafuko.Samak amesema,katika juhudi ya kuutenzua mgogoro huo,hakuwa na chaguo jingine isipokuwa kutangaza hali ya hatari.

Maandamano ya upinzani yaliyoanza juma moja lililopita,yalisambaa kote nchini mwishoni mwa juma.Ghasia hizo zilichukua sura mpya siku ya Jumatatu,baada ya chama kikubwa kabisa cha wafanyakazi kutoa wito wa kugoma,kuanzia siku ya Jumatano na hivyo kuhatarisha huduma za maji na nishati nchini humo.

Kuambatana na hali ya hatari iliyotangazwa,mkuu wa majeshi Jemadari Anupong Paojinda amekabidhiwa udhibiti wa mji mkuu Bangkok,ikiwa ni miezi minane tu tangu kuteuliwa kwa serikali ya kiraia ya Samak ambayo ilimaliza utawala wa kijeshi wa zaidi ya mwaka mmoja.Jemadari Anupong sasa ana mamlaka ya kuvunja mikutano ya zaidi ya watu watano lakini amesema, polisi na wanajeshi hawatotumia nguvu dhidi ya raia,bali watajaribu kujadiliana na wapinzani wa Samak.

Lakini waandamanaji kutoka chama cha People´s Alliance Democracy-PAD wanaomshinikiza waziri mkuu Samak aondoke madarakani, wanajiandaa kwa mapambano. Barabara katika sehemu za kati za Bangkok zimezibwa kwa sengénge na wanaharakati walioshika magongo wanapiga doria katika maeneo muhimu.

Chama cha PAD kinasema,Samak ni wakala wa waziri mkuu wa zamani Thaksin Shinawatra anaeishi uhamishoni nchini Uingereza.Kundi hilo la wapinzani ndio lililosaidia kuchochea mapinduzi ya kijeshi yaliyomngóa Thaksin mwaka 2006. Lakini washirika wengi wa Thaksin bado wapo serikalini na wanadhibiti vyeo vya juu.Waziri Mkuu Samak alishinda uchaguzi wa Desemba kwa kufanya kampeni kama wakala wa Thaksin aliekuwa akiungwa mkono na masikini katika maeneo ya mashambani na hivi sasa watu hao ni wafuasi wa Samak.Yeye ndio amekula kiapo kuwa hatoondoshwa madarakani kwa kampeni za mitaani.