1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tetemeko la ardhi laua zaidi ya watu 200 Mexico

Grace Kabogo
20 Septemba 2017

Watu wapatao 226 wamekufa baada ya tetemeko la ardhi kutokea nchini Mexico jana. Wakati huo huo, kimbunga kilichopewa jina Maria kinatarajia kupiga kusini mashariki mwa Puerto Rico leo.

https://p.dw.com/p/2kL0j
Mexiko Erdbeben Mexiko Stadt
Picha: picture-alliance/AP/E. Marti

Tetemeko hilo la ardhi lililokuwa na ukubwa wa 7.1 katika kipimo cha Richter, limetokea chini ya wiki mbili baada ya tetemeko jingine kulikumba eneo la kusini mwa Mexico na kusababisha vifo vya watu 90.

Mkuu wa shirika la kuwalinda raia, Luis Felipe Puente amesema kiasi ya watu 117 wameuawa katika mji Mexico City, 55 kwenye jimbo la Moreles, 39 kwenye jimbo la Puebla, 12 kwenye jimbo la Mexico na watatu kwenye mji wa Guerrero. Miongoni mwa waliouawa ni zaidi ya watoto 20 waliokufa baada ya jengo la shule yao ya msingi kuanguka.

Taarifa zinaeleza kuwa idadi hiyo inaweza ikaongezeka wakati ambapo timu za uokozi zinaendelea kuwatafuta waathirika katika vifusi. Rais wa Mexico, Enrique Pena Nieto, ametangaza hali ya maafa na amesema kipaumbele cha serikali yake ni kuendelea na juhudi za uokozi na kuwapatia matibabu wale waliojeruhiwa.

Mexiko  Enrique Pena Nieto PK
Rais wa Mexico, Enrique Pena Nieto Picha: picture alliance/AA/D.Cardenas

''Huduma za dharura kutoka kitengo cha usalama, jeshi na wanajeshi wa majini wako kwa ajili ya kutoa msaada kwa mtu yeyote anayehitaji. Kwa bahati mbaya watu wengi wamepoteza maisha, wakiwemo wasichana na wavulana katika shule. Natoa salama zangu za pole kwa wale wote waliopoteza ndugu na wapendwa wao,'' alisema Pena Nieto.

Takwimu za awali zilionyesha kuwa zaidi ya watu milioni 30 wangeathiriwa na tetemeko hilo. Utabiri uliotolewa na idara ya Marekani inayohusika na utafiti wa kijiolojia, ulionyesha kwamba patakuwepo na madhara na uharibifu mkubwa na maafa hayo yanaweza kuenea zaidi.

Tetemeko limepiga Atencingo

Idara hiyo imesema tetemeko hilo limetokea umbali wa maili 5 kusini mashariki mwa Atencingo katika jimbo la Puebla na kufuatiwa na matetemeko mengine madogo 11. Tetemeko hilo la ardhi limetokea siku ambayo Mexico ilikuwa ikiwakumbuka kiasi ya watu 10,000 waliokufa katika tetemeko la ardhi lililotokea mwaka 1985.

Puerto Rico Hurrikan Maria
Upepo ukivuma wakati kimbunga Maria kikikaribia Puerto RicoPicha: Getty Images/AFP/R. Arduengo

Wakati huo huo, kimbunga Maria kinatarajia kutua kusini mashariki mwa Puerto Rico leo, baada ya kupiga mashariki mwa Caribbean umbali wa kilomita 130 kusini mashariki mwa eneo la St. Croix lililopo kwenye visiwa vya Virgin vya Marekani. Mamlaka ya kukabiliana na vimbunga nchini Marekani, NHC, imesema kimbunga hicho chenye nguvu kinaendelea kuwa katika kiwango cha nukta cha tano.

Kimbunga hicho kiko umbali wa maili 85 kusini mashariki mwa San Juan huku kikiambatana na upepo mkali wa kasi ya maili 165 kwa saa. Imeripotiwa kuwa kimbunga hicho kinasafiri kwa kasi na huenda kikasababisha dhoruba ya hatari, na jana kilisababisha kifo cha mtu mmoja huko Guadeloupe, baada ya kukiharibu kisiwa kidogo cha Dominica.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AP, AFP, Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba