1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Arbeitsmarkt Deutschland

Charo Josephat30 Aprili 2009

Mpango wa kuufua uchumi bado haujafaulu

https://p.dw.com/p/Hh1C
Waziri wa uchumi wa Ujerumani Karl-Theodor zu GuttenbergPicha: dpa/picture-alliance

Fedha zilizotolewa mwanzoni mwa mwaka huu kwa lengo la kuufufua uchumi wa Ujerumani na kuyasaidia masoko ya fedha bado hazijafua dafu kutokana na kuendelea kunywea kwa uchumi mwezi huu wa Aprili.

Idadi ya watu wasio na ajira mwezi huu imefikia watu milioni 3,9 kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa leo na idara ya kazi ya serikali kuu ya Ujerumani mjini Nürnberg. Kiwango hicho ni watu takriban 200,000 zaidi ambao hawana ajira ikilingansiwha na mwaka jana. Je ukosefu wa ajira unatarajiwa kuongezeka kwa kiwango gani hapa Ujerumani?

Uchumi wa Ujerumani uko katika hali mbaya ya kuendelea kunywea. Serikali kuu ya Ujerumani mjini Berlin pamoja na taasisi za kiuchumi hapa nchini zimekadiria kwamba pato jumla la kitaifa la Ujerumani litapungua kwa asilimia sita mwaka huu. Hali hii itasababisha athari kubwa kwenye soko la ajira licha ya mpango ambao umeanza kutumiwa na kampuni kadhaa za hapa Ujerumani kupunguza muda wa kufanya kazi.

Kai Carstensen ni mtaalamu wa maswala ya uchumi katika taasisi ya mjini Munich, anasema kampuni zitalazimika kupunguza wafanyakazi wake ikiwa hali ya kiuchumi itazidi kuendelea kuwa mbaya.

"Ni kweli kwamba mageuzi ya kupunguza saa za kufanya yatasaidia kulinda nafasi za ajira. Lakini pia kampuni zitajikuta zikikabiliwa na shinikizo kubwa kupunguza wafanyakazi wake ili mradi uwezo wao kifedha utazidi kupungua kupita kiasi."

Wirtschaftsforscher stellen Prognose für 2009/2010
Kai Carstensen (katikati) akiwa na viongozi wengine wa taasisi za uchumi za UjerumaniPicha: dpa/picture-alliance

Aidha bwana Kai Carstensen amesema taasisi yake mjini Munich haitarajii nafuu yoyote katika kupotea kwa nafasi za ajira huku ikitarajiwa idadi ya wasio na ajira kufikia watu milioni tano mwishoni mwa mwaka huu.

Maoni ya mtaalam huyo wa kiuchumi yameungwa mkono na waziri wa uchumi wa Ujerumani, Karl-Theodor zu Guttenberg. Waziri Guttenberg anasema idadi ya watu wasio na ajira hapa Ujerumani inatarajiwa kuongezeka zaidi mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana.

"Tunakadiria pamoja na taasisi mbalimbali kwamba takwimu za watu wasio na ajira zitaongezeka mwaka huu kwa kiasi cha watu 450,000 na kufikia watu takriban milioni 3,7 kwa makadirio ya mwaka mzima."

Idadi hiyo inatisha na imezusha hofu kubwa hapa nchini. Sasa onyo inatolewa kuhusu kutokea kwa maandamano ya kijamii kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu wasio na ajira.

Jutta Allmendinger, mtaalam wa masoko ya ajira na kiongozi wa taasisi ya sayansi ya utafiti wa maswala ya kijamii mjini Berlin, anasema hawezi kufutilia mbali uwezekano wa kufanyika maandamano ya kijamii yanayowajumulisha watu kuanzia milioni tano au zaidi wasio na ajira.

Mtaalam huyo pia amesema iwapo hakutakuwa na sera ya kuwajumulisha watu wasio na ajira katika jamii, itakuwa vigumu kuutuliza wasiwasi wao na hivyo basi kitisho cha kutokea machafuko ni kikubwa.

Hatua zitakazochukuliwa na wanasiasa katika kukabiliana na hali ilivyo hivi sasa kwenye soko la ajira zitatoa uamuzi muhimu, onyo ambalo limetiliwa maanani na vyama vya kisiasa katika serikali ya Ujerumani. Wanasiasa wa Ujerumani nao pia wanataka kuokoa nafasi nyingi za ajira kadri inavyowezekana wakati huu uchumi ukiendelea kunywea.

Katika swala hili wameungana mikono na waajiri ambao wanataka kuwaokoa wafanyakazi wao wasipoteze ajira na halafu baadaye mgogoro wa kiuchumi utakapomalizika, waje kukabiliwa na tatizo la kutafuta wafanyakazi wengine wapya ambao hawatakuwa na uzoefu wa kutosha kufanya kazi. Njia mojawapo itakayotumiwa kuweza kulifikia lengo hili ni kupunguza saa za kufanya kazi.