1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Wasichana wengi waolewa mapema

Elizabeth Shoo/HRW30 Oktoba 2014

Shirika la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch, linaema wasichana wa Kitanzania wanaoolewa wakiwa na umri mdogo kabisa. Shirika hilo linataka umri wa chini uwe miaka 18.

https://p.dw.com/p/1Ddzi
Maandamano dhidi ya ndoa za watoto
Picha: picture alliance/AP Photo

Katika ripoti hiyo, Human Rights Watch inaelezea visa vya wasichana walioolewa wakiwa na umri mdogo kabisa, wengine hata miaka saba. Shirika hilo linaitaka serikali ya Tanzania kuamuru umri wa mtu kuoa au kuolewa uwe miaka 18, likisema kwamba wasichana wanaoolewa wakiwa wadogo wananyimwa haki zao za msingi.

Ripoti ya Human Rights Watch yenye kurasa 75 inaelezea maisha ya wasichana walioolewa wakiwa wadogo. Brenda Akia ni mmoja wa watafiti walioandaa ripoti hii. "Baada ya kuolewa wanakutana na matumizi ya nguvu. Waume zao wanawapiga, wanawalazimisha kulala nao. Hawawapi hela za matumizi hivyo wasichana hao kiujumla hawana furaha."

Sheria zinaruhusu

Sheria ya ndoa ya mwaka 1971, inasema umri wa chini wa msichana kuolewa ni miaka 15 huku mvulana akitakiwa awe ametimiza miaka 18 kabla ya kuoa. hata hivyo, watoto wenye umri kuanzia miaka 14 wanaweza kuoana iwapo mahakama itatoa ruhusa.

Human Rights imeikosoa Tanzania kwa kushindwa kuweka sheria mpya kwenye rasimu ya katiba, sheria itakayomtaka mtu awe amefikisha miaka 18 kabla ya kuoa au kuolewa. Ingawa idadi ya watoto wanaofunga ndoa imepungua katika miaka iliyopita, idadi hiyo bado ni kubwa. Kwa mujibu wa takwimu za serikali, asilimia 40 ya wanawake waliolewa kabla ya kufikisha miaka 18.

Wamasai ni miongoni mwa jamii zinazoozesha wasichana mapema
Wamasai ni miongoni mwa jamii zinazoozesha wasichana mapemaPicha: DW/A.Wasike

Mfano mmoja ni msichana Anita. Baba yake alimlazimisha kuolewa alipokuwa na miaka 16. Wakati huo alikuwa akisoma kidato cha pili. "Baba yangu aliniambia kuwa hana hela ya kunilipia ada. Baadaye niligundua kuwa alikuwa ameshapokea mahari ya ng'ombe 20 ili aniozeshe," anaeleza Anita.

Elimu ni muhimu

Sehemu kubwa ya wasichana na wanawake waliohojiwa walieleza kwamba waume zao walikuwa wamewaacha nyumbani bila hela yoyote ya kuwatunza watoto. katika baadhi ya visa, wasichana wanapigwa na wakwe zao. Na katika baadhi ya akabila, kama vile kwa wagogo au wamasai, wasichana hukeketwa kama njia ya kuwaandaa kuolewa.

Brenda Akia wa Human Rights watch anasema wasichana wanaokatisha masomo yao wako kwenye ghatari kubwa ya kuolewa. "Tunataka serikali ipige marufuku upimajiwa mimba mashuleni na mfumo wa kuwafukuza shuleni wasichana wajawazito. Serikali ihakikishe kwamba wasichana waliofeli mtihani wa darasa la saa wanapewa nafasi ya kuurudia mtihani huo," alisema Akia.

Baadhi ya wizara nchini Tanzania, ikiwemo ile ya sheria, zimeahidi kufanya juhudi zaidi kuzuia wasihan kuolewa wakiwa na umri mdogo.

Mwandishi. Elizabeth Shoo

Mhariri: Saumu Yusuf