1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taarifa za mfichua siri wa pili huenda zikamuathiri Trump

Amina Mjahid Yusuf Saumu
7 Oktoba 2019

Mfichua siri wa pili ametoa maelezo kuhusu mazungumzo ya simu kati ya rais wa Marekani Donald Trump na Ukraine, taarifa zinazokipa chama cha Democrats muelekeo wa kuchunguza mwenendo wa Trump.

https://p.dw.com/p/3QpNc
USA Trump zu Ukraine-Affäre und China
Picha: Getty Images/AFP/J. Watson

Mwanasheria Mark Zaid, anaewawakilisha wafichua siri wote wawili amesema katika ujumbe wa mkononi aliotuma kwa shirika la habari la Associated Press, kwamba mtu wa pili amezungumza na shirika la ndani la kijasusi na anaweza kuthibitisha taarifa za mfichua siri wa kwanza.

Kwamba nyaraka iliyopo inadai kuwa Trump, alimshinikiza rais wa Ukraine kuchunguza familia ya mgombea wa chama cha Democrats Joe Biden. Wakili huyo amesema mfuchua siri wa pili anafanya kazi na idara ya kijasusi na ana taarifa muhimu ya jinsi mambo yalivyokuwa.

Taarifa hizi za mfichua siri wa pili zinatishia kudhoofisha malalamiko ya Trump pamoja na washirika wake, kutaka malalamiko  ya kwanza kupuuzwa kwa hoja kuwa hayana ukweli wowote huku wakisema yamechochewa kisiasa na yasioaminika.

Kulingana na nyaraka iliyotolewa juu ya mazungumzo ya simu kati ya Trump na rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy iliyotolewa na ikulu ya Marekani, imethibitisha wazi kuwa Trump aliishinikiza Ukraine kuichunguza familia ya Biden.

Shinikizo hilo linakuja licha ya kutokuwa na ushahidi wa matendo yoyote mabaya yaliofanywa na makamu huyo wa zamani wa rais nchini Marekani au mwanawe anayefanya kazi  katika bodi ya kampuni ya gesi nchini Ukraine.

Chama cha Democrats chaendelea na uchunguzi wake dhidi ya Trump

USA Joe Biden mit Sohn Hunter
Mgombea wa chama cha Democrats Joe Biden na mwanae Hunter Biden Picha: Reuters/J. Ernst

Ushahidi wa simu ya mkononi pia wa maafisa wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani zilitoa maelezo zaidi ikiwemo Zelensky kuahidiwa kukutana na Trump iwapo serikali hiyo ya Ukraine ingekubali kuchunguza uchaguzi wa mwaka 2016  pamoja na kampuni ya gesi ya taifa hilo Burisma.

Hata hivyo Jim Himes, D-Conn kutoka chama cha Rebulican ambaye ni mwanachama wa kamati ya kijasusi amesema matamshi ya mfichua siri wa pili yanaashiria mabadiliko makubwa ndani ya serikali. "Tatizo la rais ni kwamba tabia yake imefikia mahali ambapo watu wamechoshwa,” alisema Himes.

Huku hayo yakiarifiwa chama cha Democrats kinaendeleza uchunguzi wake kwa Trump kwa nia ya kuendeleza mpango wa kumuondoa madarakani. Kamati ya kijasusi na kamati ya masuala ya mambo ya nje tayari zimemhoji Kurt Volker, aliyekuwa mjumbe maalum kwa Ukraine aliyetoa jumbe za simu ya mkononi.

Mashshidi wengine wawili wanatarajiwa kutoa ushahidi wao wiki hii ambao ni Gordon Sondland, balozi wa Marekani katika  Umoja wa Ulaya na  Marie Yovanovitch, aliyeondolewa ghafla kama balozi wa Marekani nchini Ukraine mwezi May mwaka huu.

Lakini licha ya haya yote Trump na wafuasi wake wanakanuisha kuwa Trump alifanya makosa huku ikulu ya marekani ikijizatiti kuja na jibu la pamoja juu ya suala hilo.

Chanzo: AP