1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yatetea Operesheni ya Idlib, yaijibu Ufaransa

Lilian Mtono
11 Januari 2018

Syria imejibu ukosoaji uliotolewa na Ufaransa juu ya kampeni yake ya kijeshi katika mji unaoshikiliwa na waasi wa Idlib, ikisema iliyalenga makundi ya kigaidi ambayo ni sehemu ya makubaliano ya kupunguza mapigano Idlib.

https://p.dw.com/p/2qhZJ
Syrien Luftangriffe auf Idlib
Picha: picture-alliance/AA/M. Cebes

Serikali ya Syria imejibu ukosoaji uliotolewa na Ufaransa kuhusiana na kampeni yake ya kijeshi katika mji unaoshikiliwa na waasi wa Idlib, ikisema kampeni hiyo iliyalenga makundi ya kigaidi ambayo ni sehemu ya makubaliano ya kupunguza mapigano katika eneo hilo linalodhibitiwa na waasi.

Ufaransa ilisema hapo jana kwamba ilikuwa na wasiwasi mkubwa na mashambulizi yaliyofanywa na serikali ya Syria katika mji wa Idlib, mji mkubwa uliosalia ambao bado unakaliwa na waasi wanaoipinga serikali, na kutaka makubaliano yaliyofikiwa ya kupunguza uhasama katika eneo hilo kuheshimiwa.

Uturuki, ambayo inapakana na Idlib pia imetoa mwito kwa Urusi na Iran kuishinikiza Syria kusimamisha mashambulizi katika eneo hilo ambalo lina idadi kubwa ya raia waliokimbia mashambulizi yanayofanywa na serikali katika maeneo mengine. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu alipozungumza na kamati ya bunge ya masuala ya kigeni hapo jana alinukuliwa akisema "katika siku za hivi karibuni, serikali ya Syria ilifanya mashambulizi katika mji wa Idlib na mashariki mwa Ghouta. Jana, tuliwaomba wawakilishi wa Iran na Urusi kutoa onyo kwa sababu katika makubaliano tuliyoyafikia, Urusi na Iran ni wadhamini wa serikali ya Syria katika kusimamisha mzozo na kuzuia ukiukaji". 

Türkei Sondergipfel der Organisation für Islamische Kooperation (OIC)
Waziri wa masuala ya kigeni wa Uturuki Mevlut Cavusoglu, ameitaka Syria na Urusi kuishinikiza Syria kusimamisha mashambulizi, Idlib.Picha: Reuters/A.H. Yaman

Syria yasema Ufaransa haikujua lolote kuhusu yaliyotokea Idlib.

Shirika la habari la serikali ya Syria, limenukuu chanzo kutoka wizara ya mambo ya kigeni kilichosema kwamba wizara ya masuala ya kigeni ya Ufaransa imeonyesha "ujinga mkubwa kuhusu kile kilichotokea katika jimbo la Idlib", na kwamba jeshi lilikuwa likipambana kulikomboa kutokana na ugaidi wa kundi la Al-Nusra Front na taasisi nyingine za kigaidi zinazomilikiwa na kundi hilo.

Taarifa hiyo pia ilikana kwamba jeshi liliwalenga raia ama hospitali kama ilivyodaiwa na Ufaransa.

Uturuki kwa upande wake imeituhumu serikali ya Syria kwa kuwatumia wanamgambo wa Nusra Front, ambao kwa sasa wanapambana chini ya mwamvuli wa muungano wa Tahrir al-Sham, kama kama sababu ya kuwashambulia raia na makundi ya upinzani ya wastani.

Vikosi vya serikali ya Syria vinavyoungwa mkono na wapiganaji washirika vinailenga kambi ya ndege za kijeshi iliyopo kusini mashariki mwa jimbo la Idlib.  

Taasisi za kutoa misaada ya kiutu, waokozi na wanaharakati wamedai mashambulizi ya angani yaliyofanywa na Syria na Urusi yalilenga hospitali, shule na maeneo ya soko ambayo yana idadi kubwa ya raia katika miji inayodhibitiwa na waasi.

Kwa pamoja jeshi la Syria na Urusi wamekana kushambulia maeneo yenye raia na kusema mashambulizi makubwa yalilenga tu maeneo yenye wapiganaji.

Mapema mwezi huu, ndege za kijeshi ziliilipua kwa mabomu hospitali ya wazazi katika mji wa Maarat al Numan uliopo kwenye jimbo la Idlib, ambayo ni hospitali kuu inayohudumia maelfu ya raia, na kusababisha vifo vya watu watano, ikiwa ni pamoja na watoto wachanga na wengi kujeruhiwa. Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa taasisi ya Syrian American Medical Society(SAMS) na makundi mengine ya misaada ya kiutu. 

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE
Mhariri: Grace Patricia Kabogo