1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yasisitiza itaheshimu mpango wa amani

Admin.WagnerD18 Aprili 2012

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Syria, Walid Muallem ambaye yuko ziarani China, amesema nchi yake itaheshimu ahadi iliyoitoa ya kutekeleza mpango wa amani wa mpatanishi wa kimataifa Kofi Annan.

https://p.dw.com/p/14ffV
Walid Muallem, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Syria
Walid Muallem, waziri wa mambo ya nchi za nje wa SyriaPicha: AP

Tangazo la wizara ya mambo ya nchi za nje ya China limesema kuwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Syria Walid Muallem amehakikisha kuwa nchi yake itaendelea kuuheshimu mpango wa amani wa mpatanishi wa Umoja wa Mataifa na wa Nchi za Kiarabu, Kofi Annan, na kutoa ushirikiano kwa kikundi cha waangalizi wa Umoja wa Mataifa ambao wametumwa kukagua utekelezwaji wa mpango huo.

Muallem aliyasema hayo wakati wa mazungumzo na mwezake wa China Yang Jiechi. Ziara yake inanuia nchini kuieleza nchi hiyo hatua zilizopigwa na serikali yake katika kutekeleza mpango wa Annan, ambao unahimiza usitishwaji wa mapigano na kuondolewa kwa vikosi vya jeshi kutoka mijini.

Kundi la kwanza la waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria
Kundi la kwanza la waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini SyriaPicha: AP

Wakaguzi wakumbwa na mkwamo

Kikundi cha waangalizi sita wa amani wa Umoja wa Mataifa kiliwasili nchini Syria siku chache zilizopita, lakini duru za kidiplomasia zimeeleza kuwa mazungumzo kati ya waangalizi hao na serikali yamekwama, hasa kuhusu uwezekano wa kuendesha kazi zao katika maeneo yote ya nchi.

Ahadi ya waziri Wallid Muallem inakuja baada ya wito wa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton kwa Syria, unaoitaka nchi hiyo kutekeleza mpango mzima wa amani wa Kofi Annan, na siyo kusimamisha mapigano tu kama ilivyoahidi. Bi Clinton amesema kuwa mpango huo pia unahusisha kuruhusu maandamano ya amani, kuachiwa kwa wafungwa wa kisiasa, na kuruhusu kuanza kwa kipindi cha mpito kisiasa.

Mpatanishi katika mzozo huo wa Syria Kofi Annan, amesema kuna umuhimu wa jamii ya kimataifa kuendelea kushirikiana, kuepusha hatari inayoweza kutokana na kupanuka kwa mgogoro nchini Syria.

Kofi Annan, mpatanishi wa kimataifa kuhusu Syria
Kofi Annan, mpatanishi wa kimataifa kuhusu SyriaPicha: Reuters

Kosa dogo, athari kubwa

''Kosa dogo tu, au kujidanganya kidogo vinaweza kuwa na athari zisizofikirika, kutokana na mahali ilipo Syria, kijiografia na kisiasa. Ndio maana nasema kuna umuhimu wa nchi zote kushirikiana kupata suluhu muafaka, na naamini hilo linawezekana''. Alisema Annan.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Syria, pia akiongea nchini China, amesema kuwa idadi ya waangalizi 250 inayopendekezwa inaeleweka. Awali Umoja wa Mataifa ulisema huenda wakahitajika wangalizi zaidi pamoja na ndege. Muallem hata hivyo amesema haelewi ni sababu ya kuhitaji namba kubwa ya waangalizi, na kuongeza kuwa Umoja wa Mataifa ukitaka unaweza kutumia ndege za Syria.

Lebanon yajitenga na mzozo wa Syria

Katika taarifa zinazohusiana na waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Lebanon imekataa ombo la Umoja wa Mataifa kutumia uwanja wake ulio karibu na mpaka wa Syria, kuelekea kwenye jimbo la Homs linalokumbwa na ghasia. Gazeti la nchini humo la An Nahar limesema kukataa huko kunaendana na sera ya Lebanon ya kujitenga mbali na mzozo wa Syria.

Syria inatakiwa kuruhusu maandamano ya amani
Syria inatakiwa kuruhusu maandamano ya amaniPicha: AP

Na katika kile kinachoonekana kama kutishiwa kwa mpango wa usitishwaji wa ghasia, mapema leo, vikosi vya Syria vimewashambulia kwa mabomu waasi karibu na mpaka baina yake na Uturuki, na wanaharakati wameliambia shirika la habari la dpa kuwa waasi wawili wameuawa katika mashambulizi hayo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/RTRE/DPA

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman