1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Syria: Waziri mkuu naye aikimbia serikali

Waziri mkuu wa Syria, amejitenga na utawala wa Assad na kukimbilia Jordan usiku wa kuamkia Jumatatu. Msemaji wa waziri huyo amekanusha taarifa ya televisheni ya taifa ya Syria kwamba waziri mkuu alifukuzwa kazi.

Waziri Mkuu wa Syria, Riad Hijab

Waziri Mkuu wa Syria, Riad Hijab

Mohammed al-Otri, ambaye ni msemaji wa waziri mkuu wa Syria Riad Hijab, alilisoma tamko la waziri huyo katika kituo cha televisheni cha al-Jazeera. "Ninatangaza kujitenga na utawala huu unaofanya mauaji na ugaidi na nimeamua kujiunga na wapinzani," alisema Hijab na kuongezea kwamba Assad anafanya mauaji ya halaiki dhidi ya raia wa taifa lake. Msemaji wa waziri huyo alieleza kwamba mpango wa Hijab kuikimbia serikali ya Assad ulipangwa kwa miezi kadhaa na hatimaye ulifanikiwa leo usiku ambapo Hijab pamoja na mawaziri wengine wawili na maafisa watatu wa jeshi walivuka mpaka na kuingia nchi jirani ya Jordan.

Huko Hijab aliungana na familia yake na inasemekana kwamba yuko katika mazingira salama. Hijab alikuwa miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa madhehebu ya Sunni katika utawala wa Assad ambao kwa sehemu kubwa unajumuisha waumini wa Kialawi. Kiongozi huyo, mwenye umri wa miaka 46, aliteuliwa kuwa waziri mkuu Juni 6 mwaka huu. Kabla ya hapo alikuwa waziri wa kilimo.

Hijab kuelekea Doha

Guido Westerwelle, waziri wa mambo ya nje wa ujerumani

Guido Westerwelle, waziri wa mambo ya nje wa ujerumani

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amesema kwamba kujitenga kwa Hijab ni ishara ya kumomonyoka kwa haraka kwa utawala wa Bashar al-Assad. Waziri huyo aliongezea kuwa ni muhimu kwa mapigano kusitishwa sasa na utawala mpya usioongozwa na Assad kuanzishwa.

Baada ya kuutangaza uamuzi wa waziri Hijab kujitenga na serikali, msemaji wake ameliambia shirika la habari la AFP kwamba baada ya siku chache Hijab ataondoka Jordan na kuelekea Qatar, akiufuta mfano wa viongozi wengine wa ngazi za juu walioukimbia utawala wa Assad. Wakati huo huo, mwanachama mmoja wa upinzani anayeishi Jordan ameeleza kwamba Hijab huenda akaondoka kwenda Doha, mji mkuu wa Qatar, leo usiku. Mtu huyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alieleza kwamba alikuwa miongoni mwa wale waliomsaidia Hijab kuvuka mpaka na kutaja sababu kuu inayowafanya waelekee Qatar ni kuepusha kuiletea Jordan matatizo katika uhusiano wake na Syria.

Mapigano baina ya majeshi ya Assad na waasi bado yanaendelea. Shirika la kutetea haki za binadamu Syria, lenye makao yake makuu London, Uingereza, limeripoti kwamba watu 37 wameuwawa nchini humo leo, 27 kati yao wakiwa raia wa kawaida. Katika mji wa Aleppo, ambao ni wa pili kwa ukubwa, jumla ya watu 10 walipoteza maisha yao kwenye machafuko.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp

Mhariri: Othman Miraji

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com