1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria: Wakaazi wa jimbo la Idlib bado wana wasiwasi mkubwa

Zainab Aziz
20 Septemba 2018

Mashambulio yaliyopangwa kufanyika katika jimbo la Idlib, ngome ya mwisho kabisa ya waasi nchini Syria, yameepushwa angalau kwa sasa, lakini wakaazi wa eneo hilo bado wana wasiwasi mkubwa.

https://p.dw.com/p/35Dbr
Syrien Idlib Rauch nach Luftangriffen der Regierungskoaliltion
Picha: Getty Images/AFP/O.H. Kadour

Miaka saba baada ya vita vya nchini Syria majeshi ya nchi hiyo na washirika wao wa Urusi walikuwa wamepanga kulikomboa jimbo  la Idlib ambalo ni ngome ya mwisho ya waasi wa nchini Syria. Raia kati ya milioni tatu hadi nne wanaishi katika jimbo hilo. Lakini hakuna mwenye uhakika juu ya hesabu hizo. Karibu nusu ni wale walioyakimbia majimbo mengine ya Syria. Kwa watu hao jimbo la  Idilib la kaskazini magharibi mwa Syria ndiyo matumaini yao ya mwisho.

Familia nyingi zilizokimbilia kwenye mpaka na Uturuki zina wasi wasi juu ya ndugu na jamaa zao. Raia mmoja Abdulmajid Al-Halabi huwasiliana na dada yake Fatima kwa njia ya Whatsapp wakati huduma za mtandao wa Intaneti zikiwepo. Fatima hakutarajia kuona vita vya nchini Syria vikiendelea. Miaka sita iliyopita alikimbillia kwenye mpaka na Uturuki. Hata hivyo, hali sasa imebadilika baada ya Uturuki kuufunga mpaka wake na Syria na imejenga uzio wa kilometa 800 kwa lengo la kuwazuia magaidi na wahalifu wanaosafirisha binadamu kinyume cha sheria.

Wakimbizi wa Syria zaidi ya milioni tatu na nusu wanaishi nchini Uturuki. Rais Recep Tayyip Erdogan hivi karibuni alisema kuwa nchi yake  imefikia mwisho wauwezo wake katika kuwapokea wakimbizi wa Syria. Shida za wakimbizi hao zinaongezeka. Kutokana na hofu ya mashambulio ya majeshi ya Syria na washirika wake wa Urusi maalfu ya wakimbizi wa  Syria wamekimbilia karibu na mpaka wa Uturuki.

Raia wa Uturuki Abdulmajid Al-Halabi,aliyekimbilia Uturuki
Raia wa Uturuki Abdulmajid Al-Halabi,aliyekimbilia UturukiPicha: DW/J. Hahn

Kwa mujibu wa taarifa za mashirika ya misaada wakimbizi wa Syria zaidi ya laki saba wamelundikana karibu na mpaka wa Uturuki. Afisa mmoja wa shirika la misaada Kadir Akgündüz amesema watu hao wanaishi kwa dhiki. Hata hivyo afisa huyo amesema  makubaliano  yaliyofikiwa  baina  ya Urusi na Uturuki ya kuahirisha mashambulio ni hatua ya mafanikio.

Viongozi wa nchi hizo marais Putin na Edogan walikubaliana  mwanzoni mwa wiki, kujenga ukanda wa usalama katika  jimbo la Idlib hadi ifikapo tarehe 15  mwezi ujao. Ukanda  huo utasimamiwa na wanajeshi wa Uturuki na polisi ya Syria na jeshi  la Urusi. Kulingana na makubaliano kati ya marais wa Urusi na Uturuki, wapiganaji wenye itikadi kali na hasa wa kundi la kigaidi la Al-Nusra watapaswa kuondoka Idlib.

Lakini haijafahamika jinsi zoezi hilo litakavyotekelezwa. Hata hivyo, Rais Erdogan wa Uturuki  amesema makubaliano yaliyofikiwa ni mafanikio ya kidiplomasia. Amesema Uturuki na Urusi zimeweza kuepusha maafa makubwa kwa binadamu katika jimbo la Idlib. Baadhi ya wakimbizi wa Syria walioko kwenye mpaka na Uturuki wamesema hata hivyo makubaliano hayo hayana maana ya kumalizika haraka kwa vita vya nchini Syria.

Mwandishi: Zainab Aziz/Hahn Julia

Mhariri: Mohammed Khelef