1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria: Vikwazo ndiyo njia pekee ya Ulaya dhidi ya Urusi

Iddi Ssessanga
18 Oktoba 2016

Umoja wa Ulaya unasema uungaji mkono kijeshi wa Urusi unachangia katika uhalifu wa kivita wa utawala wa Syria mkoani Aleppo. Lakini Brussels inasitasita kumchukulia hatua rais Vladimir Putin, anasema Barbara Wesel.

https://p.dw.com/p/2RMjF
Syrien Krieg - Zerstörung in Aleppo
Picha: Reuters/A. Ismail

Ni kweli kwamba lugha inayotumiwa na Ulaya dhidi ya Moscow inazidi kuwa kali. Mkuu wa sera ya kigeni na usalama wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ameiambia moja kwa moja Urusi iache mara moja kufanya mashambulizi Aleppo. Na mjini London, Paris na Berlin yanasisikika mazungumzo ya wazi kuhusu uhalifu wa kivita unaofanywa na majeshi ya Urusi. Lakini ghadabu hizo hazijafuatiwa na vitendo mpaka sasa. Vyovyote vile hakuna muafaka miongoni mwa mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya juu ya nini kinaweza kufanywa zaidi ya kuminya mikono.

Mwishoni mwa wiki waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson alijitoa kimasomaso na kugusia njia za kijeshi pale alipozungumzia kuwekwa eneo lisiloruhusiwa kuruka ndege katika anga ya Aleppo. Alisema hayo chini ya ushawishi wa waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry, ambaye katika mkutano wake wa karibuni mjini London, alizungumzia kukatishwa kwake tamaa na duru nyingine ya mazungumzo iliyopotezwa kati yake na mwezake wa Urusi, mbeuzi Sergei Lavrov.

Inaeleweka kwamba mikutano kama hii isiyoisha na waziri wa mambo ya nje wa Urusi ingemuweka Mmarekani katika hali ya kijeshi. Lakini ni wazi kabisaa kwamba hakuna kati ya Washington wala Umoja wa Ulaya alie tayari kuanzisha vita kuu vya tatu vya dunia kwa sababu ya mambo yanayotokea Aleppo. Hakuna atakaezidungua ndege za kivita za Urusi katika anga ya mji huu wa Syria.

Barbara Wesel Kommentarbild App *PROVISORISCH*
Mwandishi wa DW mjini Brussels Barbara Wesel.

Mamilioni ya Assad yaliofichwa

Hivyo njia pekee iliyosalia ni kutekeza vikwazo zaidi - ilimradi tu hakuna njia nyengine kabisaa. Rais wa Syria Bashar al-Assad na ukoo wake ndiyo wanapaswa kuwa shabaha ya kwanza. Hapo ndipo viongozi wa Uingereza na Ufaransa, wanaopaza sauti zaidi kuhusiana na kuchukizwa na kughadhabishwa kwao, wangepata fursa kulipia kile walichoshindwa kukifanya kwa miaka kadhaa. Waingereza na Wafaransa hapo wataweza kuwashughulia mwasahiba, akaunti za benki, majengo na mabilioni yaliyofichwa ya familia ya Assad. Ufaransa imetangaza kuwa itachukuwa hatua za mwanzo. Lakini maafisa wa Uingereza wamekuwa wakisimama na kuzitazama shughuli za marafiki wa Assad na watafuta misaada ya kifedha kwa miaka kadhaa bila kuchukuwa hatua zozote.

Njia ya haraka na iliyochelewa kutekelezwa dhidi ya utawala wa wahalifu wa kivita mjini Damascus ingekuwa kukata msaada na ugavi kwa dikteta muuaji. Hadi watakapofanya hivyo, Boris Johnson na mwenzake wa Ufaranda Jean-Marcj Ayrault wanapaswa kujihadhari zaidi.

Mgogoro wa kiuchumi humdhoofisha Putin

Njia pekee ya kuchukuwa hatua ni kuweka vikwazo zaidi dhidi ya Vladmir Putin. Udhaifu wa rais huyo wa Urusi uko katika hali ya kiuchumi ya taifa lake. Kwa sasa mambo hayapimiki, na hili siyo tu kwa sababu tu ya kuanguka kwa bei za mafuta bali pia kutokana na vikwazo vilivyopo ambavyo vimewekwa na Umoja wa Ulaya na Marekani tangu Urusi ilipoanza kuingilia kati nchini Ukraine.

Hii ndiyo njia pekee Umoja wa Ulaya unaweza kuitumia kuishinikiza Urusi kwa ufanisi. Kwa Ujerumani hii itamaanisha kusitisha kwanza mradi wa bomba la gesi la Nordstream. Huu siyo wa kuendelea na biashara kama kawaida na rais wa Urusi. Huu ni wakati wa kumuonyesha kuwa Umoja wa Ulaya haufanyi biashara na wahalifu wa kivita.

Zaidi ya hapo, mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya yanaweza kuchangia juu ya namna ya kufanya iwe vigumu kwa mabenki ya Urusi, walio na udhibiti wa madaraka nchini humo na taasisi za serikali kufanya kazi kimataifa. Bado ipo nafasi ya kufanya vizuri katika nyanja hii, lakini ili kufanikisha hili, ni muhimu kuwa na muafaka miongoni mwa mataifa wanachama. Pengine viongozi wa serikali wataweza kupata muafaka huu katika mkutano wa kilele mwishoni mwa wiki hii - lakini ishara hazionekani kuwa nzuri sana.

Mwandishi: Barbara Wesel/DW

Mtayarishaji: Iddi Ssessanga

Mhariri: Grace Patricia Kabogo