1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria kughubika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

25 Septemba 2012

Viongozi wa dunia wako mjini New York, Marekani, kuhudhuria kikao cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa ambacho kinaanza leo. kwenye mada kuu upo mzozo wa Syria ambao mpatanishi Lakhdar Brahimi amesema unazidi kuwa mbaya.

https://p.dw.com/p/16DdE
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle na mpatanishi kwa ajili ya Syria, Lakhdar Brahimi
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle na mpatanishi kwa ajili ya Syria, Lakhdar BrahimiPicha: picture-alliance/dpa

Rais wa Marekani Barack Obama anatarajiwa kuongoza mashambulizi ya nchi za magharibi, dhidi ya ukandamizaji unaofanywa na serikali ya rais Bashar al Assad katika mgogoro wa miezi 18 nchini Syria, na kutaka hatua kali zaidi zichukuliwe ili vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo viweze kusimamishwa.

Viongozi wengine watakaomuunga mkono rais Obama ni pamoja na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, viongozi wa nchi za Ulaya na wale kutoka baadhi ya mataifa ya kiarabu. Wito wa hatua zaidi kukomesha umwagaji damu nchini Syria unakuja baada ya mpatanishi wa kimataifa kuhusu mgogoro huo, Lakhdar Brahimi, kuliarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana kwamba hali inazidi kuwa mbaya.

Mpango wenye vipengele sita

Mzozo wa Syria unatazamiwa kuchukua muda mwingi wa baraza la Umoja wa Mataifa
Mzozo wa Syria unatazamiwa kuchukua muda mwingi wa baraza la Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/dpa

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani ambayo ndio mwenyekiti wa Baraza la Usalama kwa mwezi Septemba, Guido Westerwelle, amesema bado Umoja wa Mataifa unauthamini mpango uliopendekezwa na mpatanishi wa kwanza, Kofi Annan.

''Nadhani tunao mpango. Na mpango huo ni ule wenye vipengele sita, ambao ulipitishwa na Baraza la Usalama.'' Amesema Westerwelle.

Mpatanishi mpya wa kimataifa kuhusu Syria Lakhdar Brahimi, amesema mpango huo ni mojawapo ya zana anazoweza kutumia katika majukumu yake magumu.

Amesema, ''Mpango wenye vipengele sita, pamoja na mkataba wa Geneva, ni vitu ambavyo nasema ni zana katika kijisanduku changu cha vifaa. Namna zana hizo zitakavyotumiwa, tutajua baadaye.''

Mizozo ya Afrika pia itaangaziwa

Vita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo viko kwenye agenda
Vita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo viko kwenye agendaPicha: picture alliance/dpa

Mizozo mingine itakayoshughulikiwa zaidi katika kikao hiki cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa, ni pamoja na ule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hatua iliyopigwa nchini Somalia, na Mali ambako wapiganaji wa kiislamu wameiteka sehemu kubwa ya kaskazini. Mali tayari imeomba msaada wa Umoja wa Mataifa kukabiliana na wapiganaji hao.

Mpango wa Nyuklia wa Iran na wasiwasi Israel na nchi za magharibi juu yake, pia unatarajiwa kuangaziwa kwa mapana na marefu. Na kiongozi wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina Mahmoud Abbas anatarajiwa kuwasilisha ombi kutaka Umoja wa Mataifa uitambue Palestina kama mwanachama asiye na hadhi ya nchi, kinyume na mwaka jana ambako alitaka uanachama kamili.

Hiki ni kikao cha 67 cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa, na kimekuwa kikiendelea kwa ngazi mbali mbali tangu tarehe 18 Septemba.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/RTRE

Mhariri:Josephat Charo