Swasiland maandamano kudai demokrasia | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.04.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Swasiland maandamano kudai demokrasia

Wanaharakati kadha wamekamatwa nchini Swaziland leo walipokuwa wakielekea kwenye maandamano katika mji mkuu Mbabane.

default

Mfalme Mswati III wa Swaziland

Taarifa za hivi punde zinaeleza kuwa wanaharakati kadhaa wamekamatwa walipokuwa wakielekea kwenye maandamano katika mji wa Mbabane.Maandamano hayo ni ya kuuupinga utawala wa mfalme Mswati wa 3. Ifahamike kuwa Swaziland ni nchi pekee katika bara la Afrika inayotawaliwa na utawala wa Kifalme. Katika miaka iliyopita kila mara huzuka maandamano katika nchi hii ndogo iliyoko kusini mwa Afrika, ambapo wananchi hudai mabadiliko ya kisiasa ambayo hayafanyiki. Uhuru wa vyombo vya habari pamoja na uhuru wa kutoa maoni unazuiwa kwa kiasi kikubwa, vyama vya kisiasa vimepigwa marufuku na mfalme Mswati wa 3 , anachukua jukumu kubwa la kisiasa nchini humo tangu miaka 23 iliyopita. Mara hii waandamanaji wameamua kufanya maandamano ambayo yataendelea kwa siku kadha na kuacha kufanyakazi.

Maandamano hayo yaliyopangwa safari hii yamepangwa kuwa makubwa ambayo hadi sasa hayajawahi kutokea katika taifa hilo la kusini mwa Afrika. Mara hii vyama vyote vikubwa vya wafanyakazi vinashiriki. Inakadiriwa kuwa watu zaidi ya 20,000 wataingia mitaani. Baraza kuu la wafanyakazi limetoa wito wa kulinda maisha.

Muzi Mhlanga ni katibu mkuu wa baraza hilo. Tunataka utawala huu ujiuzulu. Kile tunachokitaka ni mfumo wa vyama vingi. Utawala huu wa sasa haufanyikazi kwa ajili yetu.

Kwa hakika kuandamana katika nchi hii ya kifalme ni hatari, kila mara hapo nyuma kumekuwa na mapambano na polisi. Mhlanga amesema kuwa hahusishi maandamano haya na kile kinachotokea katika mataifa ya Afrika kaskazini. Asubuhi ya leo polisi walilisimamisha basi dogo lililokuwa limewachukua watu kadha wanaotayarisha maandamano hayo wakati wakielekea katika mji wa Manzini. Muzi Mahlanga alizungumza na shirika la habari la AFP leo kwa simu baada ya kusimamishwa na polisi katika moja ya vizuizi vya barabarani karibu na mji mkuu Mbabane.

Amesema askari polisi 10 wakiwa na virungu wamewatoa katika basi hilo dogo na kuongeza kuwa yeye pamoja na wanaharakati wenzake 10 wamepelekwa makao makuu ya polisi. Kwa mujibu wa Mahlanga , polisi leo asubuhi wamemzuwia Sipho Kunene na Vincent Ncongwane, ambao ni viongozi wa juu wa baraza hilo la wafanyakazi. Mhlanga ameliambia shirika la habari la AFP kuwa ana wasi wasi kuwa polisi wataleta hali ya kuchochea ghasia na kuzuwia watu wengi kufika katika maandamano hayo. Mhlanga amesema hata hivyo kuwa watu nchini Swaziland wamezowea hali hiyo na kwamba wameanza maandamano kama yanayotokea katika nchi za Afrika magharibi karibu miaka mitatu iliyopita.

Tunataka kufanya maandamano ya amani. Hatutaki, hali kama inayotokea nchini Libya, itokee kwetu. Swaziland ni nchi ndogo. Tuna umoja na tuna uhusiano wa kindugu. Hatutaki kumwaga damu.

Wale ambao wanaguswa zaidi na ukandamizaji wa haki za binadamu pamoja na hali mbaya ya maisha nchini Swaziland ni wanawake. Shirika la umoja wa mataifa linaloshughulika na maswala ya ugonjwa wa ukimwi na HIV limesema kuwa nchi hiyo ina idadi kubwa zaidi ya watu wenye virusi vya HIV duniani. Asilimia 26 ya wakaazi wote wanavirusi vya ukimwi na sehemu kubwa ya watu hao ni wanawake.

Die verwaiste Generation

Mtoto wa miaka sita Sibusiso Mamba, ambaye ana virusi vya HIV.

Wanawake wanakandamizwa kwa kiasi kikubwa. Mary Rayner kutoka katika shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International ni mtaalamu kuhusiana na Swaziland na anaifahamu hali ilivyo nchini humo.

Kwa kawaida hali ya kulindwa kwa haki za binadamu ni ndogo mno katika katiba ya nchi hii. Na hali hii inaathiri sana haki za wanawake, ambao mara nyingi hujikuta katika hali mbaya pamoja na ukandamizaji. Hakuna sheria, ambayo inawalinda wanawake dhidi ya ubakaji. Wengi wao wameambukizwa virusi vya HIV na hii inatisha.


Hakuna taarifa nyingi zinazotolewa kuhusiana na hali hii. Uhuru wa vyombo vya habari unakandamizwa. Na pia uhuru wa kukusanyika unakandamizwa.

Mwandishi : Salamata Saenger / ZR / Sekione Kitojo

Mhariri :Abdul-Rahman,Mohammed

 • Tarehe 12.04.2011
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/10rpP
 • Tarehe 12.04.2011
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/10rpP

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com