1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan ya Kusini yasheherekea uhuru wake leo

Miraji Othman9 Julai 2011

Sudan ya Kusini . Taifa jipya lazaliwa leo barani Afrika

https://p.dw.com/p/11sGi
Bendera mpya ya taifa jipya la Sudan ya KusiniPicha: dapd

Maelfu kwa maelfu ya Wasudan ya Kusini walicheza ngoma na kusheherekea kwa vifijo na nderemo leo pale nchi yao mpya ilipotangazwa rasmi kuwa huru, hivyo kujitenga na Sudan ya Kaskazini. Hata hivyo, taifa hilo changa sasa linaingia katika hali isiojulikana mbele yake.

Katika sherehe za leo huko Juba, mji mkuu, rais wa nchi hiyo, Salva Kiir, alisimama ubavu kwa ubavu na hasimu wake wa zamani katika vita vya kienyeji vilivopelekea uhuru huu wa Sudan ya Kusini, Omar Hassan al-Bashir, ambaye sasa ni kiongozi  tu wa Sudan ya Kaskazini. Majeshi ya usalama yalijaribu kuweka udhibiti mabarabarani katika mji wa Juba uliojaa mavumbi, lakini yalirejea nyuma pale wananchi waliokuwa na furaha jana usiku wa manane walipoingia mabarabarani wakipiga kelele  na kusema Kusini Oyei, Uhuru Oyei. Inasemekana kuna watu waliozimia kutokana na joto pale spika wa bunge, James Wani Igga, aliposoma uwanjani hii leo tangazo rasmi la uhuru. Kuna watu waliolia, wengine wakikumbatiana.

Kuweko kwa Rais Omar Bashir katika sherehe hiyo ya leo, mtu aliyepigania kuibakisha Sudan nchi ilio moja, ilioungana, kunadhihirisha ishara muhimu juu ya nia njema ya Sudan ya Kaskazini. Pia ni aibu kwa wanadiplomasia wa nchi za Magharibi, kwa vile Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita huko The Hague imetoa waranti wa kukamatwa Rais al-Bashir. Kulikuweko pia wafuasi wa kiongozi wa waasi wa Darfur, Abdelwahid al-Nur, ambaye majeshi yake yanapigana na yale ya serekali ya Khartoum huko Darfur. Sherehe hizo zilifanyika katika uwanja ambako kuna mnara mkubwa wa sura ya marehemu John Garang, shujaa wa vita vya kienyeji vilivopelekea mapatano ya amani yalioleta uhuru wa leo.

Südsudan Unabhängigkeitserklärung
Wasudan ya Kusini wako katika hekaheka za kusheherekea siku ya uhuru wa nchi yaoPicha: dapd

Ninakwenda sasa katika uwanja wa sherehe za uhuru huko Juba, na naungana kwa njia ya simu na mwandishi wa Deutsche  Welle, Leylah Ndinda...Leylah tuelezee mambo yalivyo hivi sasa....

Nasikitika  wapendwa wasikilizaji mawasiliano ya simu na Juba yalikuwa sio mazuri.

Nchi ya kwanza jana usiku wa manane kuitambua Sudan ya Kusini ni Sudan ya Kaskazini. Risala ya Simu imetumwa kutoka  Khartoum kuwatakia kila la heri wananchi wa Sudan ya Kusini katika mustakbali wao mpya.

Bado Sudan ya Kaskazini na Kusini hazijafikia mapatano katika masuala kadhaa, kama vile mistari ya mipaka, eneo la utajiri wa mafuta la Abyei liwe upande gani, na vipi watakavogawana mapato ya mafuta,  muhimu kwa uchumi wa nchi zote mbili. Mengi ya mafuta hayo yako Sudan ya Kusini.

Gazeti moja la Sudan ya Kaskazini, Sudan Vision, limeandika kwamba kupotea kwa Kusini mwa Sudan ni heri kutoka tumbo la shari, likisema hali hiyo itavikomesha vita na likafananisha na kuukata mkono au mguu uliokuwa mgonjwa. Hata hivyo, watu wengi wa Kaskazini wanaona mgawanyiko huo kuwa ni aibu kubwa kwao .

Jana baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliamua kuunda jeshi la la kuweka amani la askari 7,000 kwa ajili ya ya Kusini mwa Sudan.

Naye waziri wa mambo ya kigeni wa Tanzania,  Bernard Membe, alikuwa na haya ya kusema kwa Deutsche Welle  juu ya kuzaliwa kwa taifa jipya la Kusini mwa Sudan...

Pia kutokana na siku hii ya uhuru wa Sudan ya Kusini, mjini Nairobi kulikuwako na sherehe, kama anavosimulia mwandishi wetu wa huko, Alfred Kiti...

Naam kwa hayo basi tunaitekea kila la heri Sudan ya Kusini iliokuwa huru kutoka leo, na pia wananchi wake waishi katika amani na neema...

Ni Othman Miraji kutoka Bonn, Ujerumani

Mwandishi: Miraji Othman

Mhariri: Sekione Kitojo