1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan waitisha maandamano makubwa zaidi

Yusra Buwayhid
21 Mei 2019

Viongozi wa maandamano Sudan wameitisha maandamano makubwa zaidi, baada ya mazungumzo yao na viongozi wa baraza la kijeshi kushindwa kufikia makubaliano juu ya upande gani ni wa kuiongoza nchi katika kipindi cha mpito.

https://p.dw.com/p/3IqV6
Sudan Khartum Proteste gegen Militär-Regierung
Picha: AFP/M. El-Shahed

Viongozi wa maandamano ya Sudan walifanikiwa kufikia makubaliano na baraza la kijeshi la kuhusu masuala kadhaa ya kipindi hicho cha mpito. Lakini mapema Jumanne, majenerali waliomuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir mwezi uliopita wamepinga madai ya waandamanaji, ya kutaka kiongozi wa nchi awe wa kiraia na idadi kubwa ya raia wa kawaida kuwamo katika baraza jipya lililokubaliwa kuongoza kipindi hicho cha mpito cha miaka mitatu hadi itakapopatikana demokrasia kamili wakati utakapoitishwa uchaguzi.

Chama cha Wanataaluma wa Sudan kinachoongoza maandamano hayo ya miezi minnne ya nchini kote, yaliyopelekea al-Bashir kuondoka madarakani, kimesema ili kupata ushindi kamili wanawataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maandamano makubwa zaidi. Mmoja wa waandamanaji kwa jina la Moujahed Mohamed amesema hawatokubali abadan kuachana na madai yao ya kutaka serikali ya kiraia.

"Baraza la kijeshi limekuwa likikawia sana, hatutoachana na madai yetu ya kutaka serikali ya kiraia. Nahisi nimebanwa sana kwavile majadiliano yamesimamishwa na sijizungumzii mimi mwenyewe tu, lakini wengi hapa wanakasirishwa na huku kuchelewa kwa baraza la kijeshi bila ya sababu za msingi," amesema Mohamed.

Sudan Militärrat Abdel Fattah al Burhan
Mwenyekiti wa Baraza la Kijeshi la Mpito, Jenerali Abdel Fattah al BurhanPicha: picture-alliance/AA

Baraza la kijeshi chini ya shinikizo

Pande hizo mbili zilifanya kile kilichoelezwa kuwa ni duru ya mwisho ya mazungumzo Jumapili jioni. Baraza la kijeshi la mpito limekuwa chini ya shinikizo kutoka nchi za magharibi na Umoja wa Afrika, kukubali madai ya waaandamanaji ya kutaka serikali ya kiraia katika kipindi cha mpito cha miaka mitatu. Na kwa hakika hilo ndiyo dai kubwa kutoka kwa maelfu ya waandamanaji, wanaokita kambi kwa wiki kadhaa sasa nje ya makao makuu ya kijeshi mji mkuu wa Sudan wa Khartoum.

Baada ya mazungumzo kuvunjika mapema Jumanne, hamna upande uliosema watarudi lini tena katika meza ya mazungumzo.

Kiongozi wa maandamano hayo Siddiq Yousef amewaambia waandishi habari kwamba mazungumzo yamesitishwa na kipengele kikuu cha mzozo ni kuhusu idadi ya wawakilishi kutoka upande wa kiraia na wa kijeshi itakayounda baraza jipya la mpito, na nani atakuwa kiongozi wa baraza hilo litakaloiongoza Sudan.

Baraza la kijeshi linataka mwenyekiti wake Jenerali Abdel Fattah al-Burhan awe kiongozi wa baraza hilo jipya la mpito, lakini waandamanaji wanataka kiongozi mpya awe ni wa kiraia.

Mwandishi: Yusra Buwayhid (rtre,afp)

Mhariri: Sekione Kitojo