1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini yatimua mjumbe wa Umoja wa Mataifa

Admin.WagnerD3 Juni 2015

Sudan Kusini imekataa wito wa Umoja wa Mataifa wa kuitaka nchi hiyo kubatilisha uwamuzi wa kumtimua mratibu mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja huo, na kudai mjumbe huyo amekuwa mara kwa mara akiikosoa serikali vikali.

https://p.dw.com/p/1Fb98
Toby Lanzer
Mratibu mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa kwa Sudan Kusini, Toby LanzerPicha: UN Photo/Martine Perret

Sudan Kusini imeupinga wito wa Umoja wa Mataifa wa kuitaka ibatilishe uamuzi wake wa kumtimua mjumbe mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa nchini humo. Nchi hio ilisema Toby Lanzer mratibu mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja huo, aliikosoa serikali mara kwa mara na kuwa alivuka mipaka kwa kusema serikali ya nchi hiyo inaelekea kuanguka.

Msemaji Mkuu wa rais wa Sudan Kusini Ateny Wek Ateny, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa ni vigumu kubadilisha uwamuzi wa kumfukuza nchi Toby Lanzer. Na kuongeza kuwa baraza la mawaziri lilitoa uwamuzi huo, baada ya kutathmini maoni ya mara kwa mara ya mjumbe huyo dhidi ya serikali.

Umoja wa Mataifa na Marekani zalaani uwamuzi wa Sudan Kusini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amelaani uwamuzi huo na kusema Toby Lanzer mzaliwa wa Uiengereza amekuwa mstari wa mbele katika kushughulikia mahitaji ya kibinaadamu yanayoengezeka katika jamii zilizoathirika kutokana na migogoro nchini humo.

Marekani nayo pia imeulaani uwamuzi wa Sudan Kusini wa kumtimua mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa na kusema kuwa ni kitendo kisichoheshimu jumuiya ya kimatifa.

Msemaji Mkuu wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani John Kirby amesema kutimuliwa kwa mjumbe huyo kunaonesha kutokujali kwa maafa ya watu wa Sudan Kusini.

Konflikt im Südsudan Flüchtlinge 17.01.2014
Wakimbizi wa mgogoro nchini Sudan KusiniPicha: Phil Moore/AFP/Getty Images

Kirby pia amaesema serikali ya Sudan Kusini inapaswa kulipa kipau mbele suala la kuleta amani katika nchi hiyo na kusitisha machafuko. Machafuko hayo yamesababisha zaida ya watu milioni mbili kupoteza makaazi, wengi kati yao ni wakimbizi katika nchi jirani. Aliongeza kwamba watu milioni 4.6 wanakabiliana na janga la njaa nchini humo.

Sudan Kusini ni miongoni mwa nchi zenye janga kubwa la kibinaadamu, na Lanzer mara kwa mara aliwalaumu viongozi wa serikali kwa kuengezeka machafuko pamoja na kusaini mikataba ya amani na kushindwa kuitekeleza.

Lanzer hata hivyo alikuwa anakaribia kumaliza muda wake kama Naibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, na Eugene Owusu kutoka Ghana alishateuliwa kuchukua nafasi yake.

Lazer atachukua wadhifa mpya kama mratibu wa misssada ya Umoja wa Mataifa katika eneo la Sahel, mwishoni mwa mwezi Juni.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/RTRE/AFPE

Mhariri:Yusuf Saumu