1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan kusini ni taifa jipya

10 Julai 2011

Sudan Kusini imetangaza rasmi uhuru wa eneo hilo kutoka Sudan Kaskazini katika sherehe zilizofanyika katika mji mkuu mpya Juba.

https://p.dw.com/p/11sNn
Rais mpya wa Sudan kusini, Salva Kiir akiinyanyua katiba mpya nchini humoPicha: dapd

Aliyekuwa kiongozi wa waasi, Salva Kiir ameapishwa kuwa rais wa kwanza wa taifa hilo jipya.

Salva Kiir Mayardit Südsudan
Rais Salva Kiir MayarditPicha: picture alliance / dpa

Katika hotuba yake, Rais Kiir ametoa msamaha kwa makundi yote yaliojihami na kupigana dhidi ya serikali yake na ameahidi kuleta amani katika maeneo ya mipakani yanayokumbwa na matatizo. Sherehe zilitanda mjini Juba kuanzia saa sita za usiku kuamkia jana Jumamosi, wakati umati wa watu ulisherehekea uhuru wa taifa hilo.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi 30 wa Afrika, maafisa wakuu wa mataifa ya magharibi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon. Miongoni mwa wageni wa heshima, alikuwepo adui wa zamani wa taifa hilo jipya, Rais wa Sudan, Omar Hassan al Bashir.

Symbolbild politische Spaltung im Sudan vor der Präsidentschaftswahl
Rais Omar Hassan Al Bashir.Picha: DW/AP

Kwengineko Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, ameahidi msaada wa Ujerumani katika kuanzishwa kwa mfumo imara wa kisiasa nchini Sudan Kusini, baada ya eneo hilo kujitenga na kuwa taifa jipya.

Katika hotuba yake ya kila wiki kupitia kanda ya video, Merkel amesema sasa ni muhimu kuiunga mkono Sudan Kusini, kuelekea utulivu utakaowaletea watu wa eneo hilo amani, usalama na maendeleo ya kiuchumi.

Kansela huyo wa Ujerumani anatarajiwa kulitembelea bara la Afrika kwa mara ya pili kama kiongozi wa serikali, kuanzia hapo kesho Jumatatu hadi siku ya Alhamisi. Ziara hiyo inampeleka Kenya, Angola na Nigeria.

Mwandishi Maryam Abdalla/epd, afp, dpa, rtr
Mhariri:Martin, Prema.