1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Suala la Bashir latia kiwingu Mkutano wa Umoja wa Afrika

Admin.WagnerD15 Juni 2015

Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika umefunguliwa mjini Johannesburg Jumapili (14.06.2015) kwa kulenga masuala ya kuwawezesha wanawake, usalama wa kanda na mpango wa maendeleo wa muda mrefu wa bara hilo.

https://p.dw.com/p/1FhM4
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma.Picha: Issouf Sanogo/AFP/Getty Images

Mkutano huo wa Kilele wa 25 wa Umoja wa Afrika mada yake ikiwa kuwawezesha wanawake na maendeleo kuelekea Agenda ya Afrika mwaka 2063 umewakutanisha viongozi wa zaidi ya nchi hamsini wanachama wa umoja huo. Katika hotuba yake ya ufunguzi Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Afrika Nkosazana Dlamini - Zuma amepongeza juhudi za pamoja za kukabiliana na mripuko wa karibuni wa gonjwa la Ebola huko Afrika magharibi.

Likizungumziwa suala la kuwawezesha wanawake Dlamini Zuma amesema kipau mbele kinapaswa kuwa wanawake na watoto katika maeneo ya mizozo kwa kuhakikisha usalama wao na kurudisha amani katika maeneo hayo.Amesema kwa bahati mbaya wanawake na watoto ni wahanga wakuu wa vita na mizozo ambayo hawahusiki katika kuianzisha.Ameongeza kusema kwamba azma yao ni kuzinyamzisha bunduki na kuwapa matumaini wanawake na watoto wanaoteseka kutokana na vitisho vya Boko Haram na Al- Shabab.

Dlamini Zuma pia ametowa wito kwa nchi za Kiafrika kujifunza kutokana na kuripuka kwa matumizi ya nguvu yanayotokana na chuki dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini na maafa yanayowakuta maelfu ya wahamiaji haramu wa Kiafrika wanaofia katika bahari ya Mediterenia wakati wakijaribu kukimbilia Ulaya. Ametaka mchakato wa kushughulikia tatizo hilo la uhamiaji na kujumuishwa kwa wageni katika jamii uharakishwe.

Afrika inakua

Katika hotuba yake ya ufunguzi Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amesema Afrika imeingia kwenye ukuaji wa kiuchumi na maendeleo.

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini na viongozi wa Kiafrika.
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini na viongozi wa Kiafrika.Picha: picture alliance/dpa/Gcis/Siyasanga Mbambani

Amezitaka nchi za Kiafrika kuimarisha ushirikiano wao kushughulikia mizozo ilioko ndani ya bara hilo na kuchukuwa maamuzi mazito ya kukabiliana na changamoto mpya kama vile ugaidi.

Hata hiyo mkutano huo umetiwa dosari na shinikizo la Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC kutaka Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan akamatwe kutokana na mashtaka yanayomkabili ya kuhusishwa katika mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita katika jimbo la Dafur nchini Sudan.Mahakama ya Afrika Kusini inatazamiwa kutowa uamuzi wake leo iwapo kiongozi huyo akabidhiwe katika mahakama hiyo.

Suala la Bashir

Waziri wa habari wa Sudan Ahmed Bilal Osman amesema serikali ya Afrika Kusini itamuachia kiongozi wa nchi hiyo kurudi nyumbani bila ya kujali uamuzi wa mahkama hiyo.

Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan.
Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan.Picha: Reuters/Str

Amekaririwa akisema "Rais Zuma ametamka kwamba Rais Bashir ni mgeni wetu Afrika Kusini anaweza kubakia kwa muda wote anaotaka na kuondoka wakati wowote ule anaoutaka.Hivi sasa rais wetu anahudhuria kikao na atarudi Sudan baada ya kama masaa mawili."

Masuala mengine makuu yanayojadiliwa na mkutano huo wa kilele wa Umoja wa Afrika ni mzozo wa kisiasa nchini Burundi,pendekezo la kuwepo kwa eneo la biashara huru barani Afrika na jinsi ya kupata vyanzo vipya vya mapato kugharamia operesheni za umoja huo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ AFP /

Mhariri :Iddi Ssessanga