1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Stuttgart yateua kocha mpya kuinusuru kushuka daraja

10 Machi 2014

Bayern Munich yazidi kupata mafanikio katika Bundesliga msimu huu,wakati katika nafasi ya kushuka daraja Stuttgart yaachana na kocha wake Thomas Schneider na kumteua Huub Stevens kuiokoa timu hiyo kutoshuka daraja.

https://p.dw.com/p/1BMxQ
Huub Stevens PK VfB Stuttgart 10.03.2014
Kocha mpya wa Stuttgart Huub Stevens akitambulishwaPicha: picture-alliance/dpa

Katika mchezo wa 24 wa ligi ya Ujerumani Bundesliga FSV Mainz 05 ilitoshana nguvu na Hertha BSC Berlin kwa kufungana bao 1-1 jana Jumapili na Borussia Dortmund ikaizamisha Freiburg kwa bao moja kwa bila katika ushindi ambao ulikuwa ni wa kibarua kigumu kwa Borussia ambayo inashikilia nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ikiwa na points 48 , points 4 mbele ya timu inayoshikilia nafasi ya tatu Bayer Leverkusen ambayo nayo Jumamosi ilikubali sare ya bao 1-1 dhidi ya Hannover 96 na pia hakukuwa na mshindi kati ya Borussia Moenchngladbach na FC Augsburg.

Fußball Bundesliga 24. Spieltag 1. FSV Mainz 05 - Hertha BSC
Mchezaji wa Mainz ChupomotingPicha: picture-alliance/dpa

Nahodha wa Borussia Dortmund Sebastian Kehl amesema kuwa Borussia ilikuwa na bahati kutokana na ushindi huo.

"Nilijaribu tu kuupiga mpira huo na ni dhahiri kulikuwa na hali ya bahati. Mlinda mlango Oliver Baumann alikuwa amesimama kidogo nje ya goli lake, kwa kuwa yeye huwa ni mchezaji mlinda mlango na ndio sababu mkwaju wangu ulifanikiwa kumpita, lakini pamoja na hayo kuna bahati ndani yake."

Fußball Bundesliga 25. Spieltag SC Freiburg Borussia Dortmund
Wachezaji wa Borussia Dortmund wakimpongeza nahodha Kehl kwa kufunga bao la ushindiPicha: Thomas Kienzle/AFP/Getty Images

Bayern yararua

Bayern Munich iliirarua Wolfsburg kwa mabao 6-1 na VFB Stuttgart ilitoshana nguvu na Eintracht Braunschweig kwa kufungana mabao 2-2. Hali hiyo iliwalazimkisha viongozi wa klabu hiyo kongwe kuamua kuachana na kocha Thomas Schneider baada ya kutopata ushindi katika michezo tisa aliyokuwa akiiongoza. Mkurugenzi wa spoti wa Stuttgart, Fredi Bobic ametangaza jana Jumapili(09.03.2014)kuwa kocha huyo hatakaa tena katika benchi la ufundi la Stuttgart na badala yake kocha mpya Huub Stevens atachukua hatamu za uongozi.

"Tunataka kwa hakika kujenga msukumo mpya kwa wachezaji. Kwa kuwa hilo halikuwapo kwa kocha Thomas Schneider. Lakini tumegundua kwamba mbinyo kwa sasa ni mkubwa mno na kwamba tunatakiwa pia kujinasua kidogo kutoka katika hali hii kwa sasa. Uamuzi wa kumteua Huub Stevens kwangu mimi ni uamuzi utakaodumu hadi mwisho wa msimu."

Huub Stevens PK VfB Stuttgart 10.03.2014
Kocha Huub StevensPicha: picture-alliance/dpa

Kikosi cha kocha Thomas Tuchel cha Mainz 05 kina kila nafasi kuweza kucheza katika mashindano ya Ulaya iwapo kitaendelea kufanya vizuri kama kinavyofanya hivi sasa, kama anavyoeleza mchezaji wa Mainz Christoph Moritz.

"Tuko katika eneo la msimamo wa ligi, ambapo inawezekana kutamaliza msimu huu kwa kushiriki katika ligi ya Ulaya, lakini kwa sasa hatuwezi kufikiria sana kuhusu hilo. Tunaangalia kufuatana na kila mchezo katika msimamo wa ligi, lakini kwa sasa haitoi maelezo kamili. Tunaona , kwamba Bayern iko mbali sana na sisi tuko mbali na eneo la kushuka daraja."

Pellegrini hatakaa katika benchi la ufundi

Wakati huo huo kocha wa Manchester City Manuel Pellegrini, amewashutumu wachezaji wake kwa kubweteka baada ya kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya mabingwa wa kombe la FA Wigan Athletics katika mchezo wa robo fainali ya kombe hilo hapo jana.

Ndoto za Man City za kupata mataji matatu ama hata mataji matatu ya nyumbani yaliongezeka wakati ilipotwaa taji la kombe la ligi katika uwanja wa Wembley dhidi ya Sunderland wiki iliyopita.

Lakini dhidi ya timu hiyo iliyoko katika daraja la pili Wigan, timu inayoongozwa na mchezaji wa zamani wa City Uwe Rosler na timu ambayo iliishinda City katika fainali ya kombe hilo mwaka jana , City walijikuta wakiwa nyuma kwa mabao 2-0 kwa magoli ya Jordi Gomez na James Perch kabla ya Samir Nassir kupachika bao la kufutia machozi na kutoa matumaini ya hata kulazimisha sare ya kurudiwa kwa mchezo huo.

Katika ligi ya Uhispania La Liga Real Madrid wamechukua fursa ya Barcelona kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Real Valladolid na kuiadhibu Levante kwa mabao 3-0 nyumbani jana Jumapili na kukiweka kikosi hicho cha kocha Carlo Ancelotti points tatu juu ya msimamo wa ligi hiyo.

Schalke vs. Madrid
Wachezaji wa Real Madrid wakishangiria baoPicha: Reuters

Mkwaju wa Kwandwo Asamoah katika kipindi cha kwanza umeihakikishia Juventus Turin ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Foorentina wakati wakiweka rekodi ya kutofungwa nyumbani katika ligi ya msimu huu.

Juve sasa inaongoza kwa points 14 kutoka timu inayoifuatia AS Roma ambayo ilikubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya SSC Napoli jana Jumapili.

Mchezaji wa kiungo wa Arsenal London Mesut Ozil ambaye alinunuliwa kwa kitita kikubwa mwanzoni mwa msimu huu kutoka Real Madrid amejitoa kutoka hali ya fadhaa baada ya kukosa penalti katika mchezo wa Champions League dhidi ya Bayern Munich na kumaliza ukame wa magoli kwa kuonesha mchezo safi katika ushindi dhidi ya Everton katika mchezo wa robo fainali ya kombe la FA, amesema kocha wa Arsenal , Arsene Wenger.

Mesut Özil beim Arsenal Spiel gegen Norwich
Mchezaji wa Arsenal Mesut ÖzilPicha: picture-alliance/dpa

Mchezaji huyo wa kati raia wa Ujerumani alionekana kuwa katika hali ambayo si ya kawaida katika wiki za hivi karibuni wakati Arsenal iliteleza kutoka juu ya msimamo wa ligi ya Uingereza Premier League na kujikuta katika hali mbaya zaidi baada ya Arsenal kushindwa katika mchezo wa nyumbani kwa mabao 2-0 dhidi ya Bayern Munich.

Hata hivyo Arsenal London pamoja na Manchester City zote za Uingereza zinakabiliwa na kibarua kigumu wakati zitakapofanya ziara kwa miamba wa soka katika bara la Ulaya Bayern Munich na Barcelona zikiwania kubadilisha majaliwa yao baada ya kipigo cha mabao 2-0 nyumbani katika mchezo wa pili wa timu 16 katika Champions League hapo kesho Jumanne.

Kocha wa Arsenal Aserne wenger hata hivyo anamatumaini ya kurudia kile alichokifanya msimu uliopita katika kiwango kama hiki.

Kibarua cha Manchester City dhidi ya Barcelona kinaonekana kuwa kigumu na watahitaji kupambana bila kocha wao mkuu Manuel Pellegrini ambaye anatumikia adhabu ya kutokuwa katika benchi la ufundi la timu hiyo kwa michezo miwili wakati kikosi chake kitakapoingia katika uwanja wa Camp Nou kesho Jumanne(11.03.2014).

Timu za Misri bado jinamizi kwa Yanga

Huko katika bara la Afrika , Dar Young African , Yanga imetolewa katika kinyang'anyiro cha kuwania kuingia katika awamu ya makundi katika Champions League barani Afrika, baada ya kutolewa na Al-Ahly ya Misri kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya timu hizo kutoka uwanjani katika dakika 90 baada ya Al-Ahly kupata ushindi wa bao 1-0.

Katika mchezo wa kwanza mjini Dar Es Salaam Yanga iliishinda Al-Ahly kwa bao 1-0. Ndipo timu hiyo zilipopigiana mikwaju ya penalti na Al-Ahly ilifanikiwa kupata mikwaju 4 na Yanga 3.

Huko mjini Nairobi , AFC Leopards ilijikuta ikiyaaga mashindano hayo baada ya kutoka sare na Super Sport ya Afrika kusini ya mabao 2-2 na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2.

Zaidi ya theluthi moja ya tikiti 61,000 kwa ajili ya mpambano wa fainali ya Champions League katika bara la Ulaya itakayofanyika mjini Lisbon Ureno Mei 24 mwaka huu zitakwenda kwa maafisa, wafadhili pamoja na takrima kwa makampuni mbali mbali.

Jumla ya tiketi 37,000 katika uwanja huo ambao una uwezo wa kuingia mashabiki 61,000 zitauzwa kwa mashabiki wa timu zitakazoingia fainali pamoja na watu wengine watakaopenda kuuona mchezo huo. Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA limeongeza kuwa tikiti nyingine 24,000 zitagawiwa kwa kamati ya utayarishaji wa fainali hiyo nchini Ureno, UEFA pamoja na vyama vya soka vya mataifa wanachama , washirika wa kibiashara wa shirikisho hilo pamoja na vyombo vya utangazaji, pamoja na mpango wa takrima wa shirikisho hilo.

Timu mbili zitakazoingia fainali zitapewa tikiti 17,000 kila moja na 3,000 zitauzwa kwa mashabiki duniani kote kupitia tovuti ya shirikisho la UEFA.

Rais wa Bayern afikishwa kizimbani

Rais wa klabu ya soka ya Bayern Munich Uli Hoeness, aliiambia mahakama katika kesi ya kukwepa kulipa kodi iliyoanza rasmi leo dhidi yake kuwa alificha mamilioni ya euro kuliko maafisa walivyofikiria lakini amekana kuwa kupe wa kijamii.

Prozessauftakt Uli Hoeneß Steuerhinterziehung
Rais wa Bayern Munich Uli HoennesPicha: Reuters

Katika mabadiliko ambayo hayakutarajiwa , mwendesha mashtaka Hanns Feigen amesema kuwa Hoennes ameidanganya idara ya kodi kiasi cha euro milioni 18.5, zaidi ya euro milioni 3.5 zilizoorodheshwa katika mashataka ya mwanzo.

Kesi hiyo dhidi ya Hoennes imevuta hisia za wapenzi wa soka katika taifa la Ujerumani kwa kiasi kikubwa.

Mwandishi : Sekione Kitojo rtre / afpe / dpae

Mhariri : Mohammed Abdul Rahman