1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Stevens achukua usukani katika klabu ya Hoffenheim

27 Oktoba 2015

Klabu ya Bundesliga Hoffenheim imemteuwa Huub Stevens kuwa kocha wake mkuu. Tangazo hilo limekuja saa chache tu baada ya habari kutolewa kuwa Markus Gisdol amepigwa kalamu

https://p.dw.com/p/1GufK
Deutschland Huub Stevens neuer Trainer 1899 Hoffenheim
Picha: Imago/Revierfoto

Taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya TSG Hoffenheim 1899 imethibitisha kuwa Stevens mwenye umri wa miaka 61 ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo.

Pia imethibitisha kuwa Gisdol ameachishwa kazi, pamoja na makocha wawili wasaidizi wake, Frank Kaspari na Frank Fröhling. Stevens amepewa mkataba wa hadi mwisho wa msimu huu.

Gisdol mwenye umri wa miaka 46 amekuwa katika wadhifa huo tangu Aprili 2013, wakati alifaulu kuiokoa klabu hiyo dhidi ya kushushwa ngazi katika ligi ya divisheni ya pili. Gisdol ni kocha wa pili wa Bundesliga kuachishwa kazi, baada ya Lucien Favre wa Borussia Moenchengladbach kujiuzulu baada ya mwanzo mbaya wa msimu.

Kazi ya mwisho ya Stevens katika Bundesliga ilikuwa katika klabu ya Stuttgart, ambako aliisaidia timu hiyo kuepuka shoka la kushushwa daraja msimu uliopita. Alfred Schreuder mwenye umri wa miaka 42 ameteuliwa kuwa msaidizi wake.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Daniel Gakuba