1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier na Kouchner waimba, Merkel na Sarkozy wakubali juu ya Iran

Maja Dreyer12 Novemba 2007

Kila baada ya miezi sita, mabaraza ya mawaziri ya Ujerumani na Ufaransa yanakutana kwa mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa. Leo hii, mkutano huu unafanyika mjini Berlin na mawaziri hao walikuwa na mbinu mpya kabisa kuonyesha ushirikiano wao.

https://p.dw.com/p/CH71
Angela Merkel amemkaribisha rais Sarkozy wa Ufaransa mjini Berlin
Angela Merkel amemkaribisha rais Sarkozy wa Ufaransa mjini BerlinPicha: AP

Safari hii, mkutano wa mabaraza ya mawaziri ya nchi hizo mbili jirani ulikuwa wa aina maalum. Walizingatia hasa suala la kuwaunganisha wageni katika jamii zao, mawaziri wa Ufaransa na Ujerumani hawakukaa ndani ya chumba cha mkutano tu, bali walikuwa na shughuli kadhaa. Mawaziri wa nje Frank-Walter Steinmeier na Bernard Kouchner walikutana na kundi la wanamuziki wa asili ya Kituruki na Kijerumani kurikodi wimbo unaosifu utajiri wa jamii yenye watu wa asili tofauti. Nadhani kama waziri sikuimba vibaya, Bw. Kouchner wa Ufaransa alisema baada ya kutoka studioni. Wimbo huu utasikika baadaye leo hii kupitia mtandao wa Internet.

Mawaziri wengine pia walishirikiana kitaalamu na kutembelea miradi fulani ya kuwajumuisha wageni mjini Berlin. Kansela Angela Merkel na rais Nicolas Sarkozy ambaye kwa mara ya kwanza tangu kuingia madarakani amezuru mjini Berlin, walitembelea shule ya sekondari na kuhudhuria mjadala na wanafunzi wenye asili ya kigeni. Mbele ya watoto hao, rais Sarkozy alisema inabidi kudhibiti uhamiaji mipakani ili kufanikiwa kuwajumuisha wageni katika jamii. Adui wa umoja wa jamii ni uhamiaji usio halali, Sarkozy alisema kwani bila ya udhibiti, mifumo ya kijamii itaharibika. Kansela Merkel kwa upande wake alisisitiza muda umewadia kujifungua kwa wageni. Wajerumani wawe tayari kuwaunganisha katika jamii yao. Lakini msingi wa umoja ni lugha, Bi Merkel alisema.

Baada ya safari hizo ndogo ndogo, mawaziri wote walikutana kwa mazungumzo yao. Baada ya hapo, viongozi wa nchi hizo mbili walisema Ujerumani na Ufaransa zitaongeza ushirikiano wao katika suala la uhamiaji. Mawaziri wa mambo ya kigeni, ndani na sheria wanatarajiwa kutafuta suluhisho la pamoja kudhibiti na kuzuia uhamiaji usio halali. Vilevile, Kansela Merkel na rais Sarkozy waliarifu kwamba wanataka vikwazo dhidi ya Iran viongezwe kuwa vikali zaidi ikiwa sera za kinyuklia za Iran hazitaboreka.

Na Angela Merkel aliongeza kusema: “Tunataka kuzijumuisha pia China na Urusi katika msimamo wa jumuiya ya kimataifa kwamba hatuwezi kukubali mradi huu wa kinyuklia na tulikubaliana pamoja na nchi nyingine za Ulaya kupunguza uhusiano wetu wa kibiashara na Iran. Mfano ni kwamba benki za Kijerumani hazifanyi biashara tena huko Iran. Kwa hivyo naona kuna maelewano kuhusu suala hili.”

Katika matamshi yake, rais Sarkozy wa Ufaransa alikiri lakini misimamo inatofautiana juu ya kasi ya kuchukua hatua. Ufaransa inataka Umoja wa Ulaya kuweka vikwazo vingine, Ujerumani lakini inataja kusubiri ripoti mpya ya shirika la kudhibiti nishati ya kinyuklia IAEA. Wote wawili, Sarkozy na Merkel, walisisitiza kuendelea na mazungumzo. Sababu ya kukumbusha hayo huenda ni kwamba Marekani inaelekea kuwa tayari kuishambulia Iran.