1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier akutana na Gül

Josephat Charo27 Juni 2007

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, jana alikutana na waziri wa kigeni wa Uturuki, Abdullah Gül. Mazungumzo yao yalituwama juu ya uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya na mzozo juu ya kijana wa kijerumani wa miaka 17 anayezuiliwa na polisi nchini Uturuki.

https://p.dw.com/p/CHC4
Marco kijana wa kijerumani anayezuiliwa nchini Uturuki
Marco kijana wa kijerumani anayezuiliwa nchini UturukiPicha: picture-alliance/ dpa

Hata baada ya mazungumzo marefu kati ya waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujeruamni, Frank Walter Steinmeier, na mwenzake wa Uturuki, Abdullah Gül, yaliyoendelea hadi usiku, bado hakuna matumani ya Marco W kijana wa kijerumani kuachiliwa huru kwa haraka. Kijana huyo anazuiliwa katika jela moja ya Uturuki na anahojiwa na polisi kuhusiana na madai kwamba alimuhujumu kimapenzi msichana wa miaka 13 wa Uingereza alipokuwa likizoni katika eneo la mapumziko la Antalya nchini Uturuki.

Mamake msichana huyo amemfungulia mashtaka kijana huyo akimshitaki kwa kumuingilia kimapenzi msichana wake. Lakini Marc anasisitiza alimshikashika tu msichana huyo. Kwa mujibu wa sheria za Uturuki kijana huyo anakabiliwa na kifungo cha miaka minane gerezani iwapo atapatikana na hatia.

Waziri Steinmeier alisema mjini Brussels wakati wa mazungumzo ya uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya kwamba alizungumza na mjumbe wa Uturuki kwenye mkutano huo, Ali Babacan, kuhusu swala la kijana huyo.

´Tunaheshimu uhuru wa mahakama ya Uturuki. Kinachozungumziwa hapa ni umakini muhimu unaohitajika kutoka kwa vyombo vya Uturuki kuhusu swala hili kuongoza na kusadia ili suluhisho lipatikane na kijana aweze kurejea kwa wazazi wake nchini Ujerumani haraka iwezekanavyo.´

Wazazi wa kijana huyo aliyekamatwa mnamo mwezi Aprili mwaka huu wana hofu na wameathiriwa sana kiafya. Mjumbe wa Uturuki katika mkutano wa mjini Brussels, Ali Bababacan, amesema amehuzunishwa na kesi ya Marc lakini serikali ya Uturuki haiwezi kufanya lolote kuishinikiza mahakama kuhusu kesi hiyo. Hata hivyo alisema juhudi zitafanywa ili wazazi wa kijana huyo waweze kumtembelea.

Katika mahojiano yake na gazeti al Hürriyet la Uturuki na gazeti la Bild la hapa Ujerumani, Marc alisema msichana huyo wa Uingereza alimwambia ana umri wa miaka 15 na kwamba hakufanya mapenzi naye. Kijana huyo wa shule anazuiliwa pamoja na washukiwa wengine 30 katika mahabusi. Hajafanyiwa ubaya wowote lakini amekiri anasumbuka kulala.

Kuhusu mazungumzo ya uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya, umoja huo jana ulikataa kuanzisha mazungumzo kuhusu sera za kiuchumi na kifedha. Uturuki imekasirishwa na hatua hiyo. Mjumbe wa Uturuki kwenye mkutano wa mjini Brussles, Ali Babacan, alisema, ´Hatujaridhishwa na sababu tulizopewa na tunatumai kutakuwa na maendeleo mazuri wakati Ureno itakapochukua urais wa Umoja wa Ulaya.´

Lakini waziri wa kigeni wa Ujrumani, Frank Walter Steinmeier, anasema ipo haja ya kuendeleza majadiliano.

´Kila mara kunapokuwa na haja ya mazungumzo ndani ya Umoja wa Ulaya ni utamaduni mzuri kutoikataa haja hii bali kwa pamoja kutafuta ufumbuzi. Vinginevyo nawahakikishieni tunabakia katika msimamo wa Ulaya wa kuzingatia sheria msingi na kuheshimu mikataba.´

Ureno inachukua urais wa Umoja wa Ulaya kuanzia Julai mosi kutoka kwa Ujerumani.