1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sports: Chelsea na Manchester United sasa zapigania ubingwa wa Uingereza

Mwakideu, Alex2 Mei 2008

Baada ya Champions League Chelsea na Manchester sasa zalitupia macho kombe la Premeir

https://p.dw.com/p/DsLD
Mchezaji wa kiungo cha kati wa Chelsea Michael Ballack anasherehekea bao la pili dhidi ya Manchester United katika ligi ya UingerezaPicha: AP

Baada ya kujikatia tikiti ya kuenda Moscow kwa fainali ya kombe la klabu bingwa-ulaya Champions league, Manchester United na Chelsea sasa zinang'ang'aniana kikombe cha ligi ya nyumbani Uingereza Premiership.


Wakati huo huo Bayern Munich ambayo imekuwa ikiongoza msimamo wa ligi ya Ujerumani inatarajiwa kutawazwa bingwa wa Bundesliga wikendi hii.


Mechi tatu zimesalia kabla ya ligi ya ujerumani Bendesliga kumalizika hapo mei 17 na Bayern Munich inaongoza kwa pointi 12.


Timu hiyo inatarajia kutawazwa bingwa wa Ujerumani kwa mara 21 wikendi hii.


Ikiwa na wakati mchache wa kujiliwaza kutokana na mechi ya duru ya pili ya kombe la shirikisho la ulaya kule St Petersburg Bayern ambayo ilipewa kichapo cha mabao nne kwa nunge itatumia uwezo wake kucheza mechi mbili muhimu zinafuatana kwa karibu.


Kocha wa Wolfsburg Felix Magath ambaye alipigwa kalamu na Bayern mwezi februari mwaka uliopita anaonekana kana kwamba atakuwa na wakati mgumu kutazama timu hiyo ikiinua kombe la Bundesliga juu juu.


Anasema timu yake imepata pointi moja dhidi ya Leverkusen hivi majuzi na inataka kusherehekea ushindi mwengine dhidi ya Munich hapo kesho angalau kwa pointi tatu.


Lakini iwapo Wolfsburg imeendelea kiasi cha kwamba inaweza kumenyana na Bayern Munich tangu ilipochapwa mabao mawili kwa moja November mwaka uliopita, hilo ni swala la kusibiri na kujionea.


Iliyobaki sasa ni muujiza wa mahesabu ndio unaoweza kuzifanya Werder Bremen na Schalke 04 zikafikisha pointi 12 na kuindoa Bayern katika kilele cha ligi.


Iwapo pande timu hizo mbili zitashindwa au zitatoka sare wikendi hii basi taji hilo litaishia mikononi mwa Bayern Munich.


Kwa upande mwengine Man-U na Chelsea ambazo zimejikatia tiketi ya fainali ya kupigania ubingwa wa uropa zinarejea uwanjani kushughulikia maswala ya nyumbani yaani kombe la Uingereza Premiership ili kwanza tujue nani bingwa Uingereza.


Man U inayoongoza kwa mabao mengi zaidi katika ligi hiyo inaikaribisha West Ham hii leo uwanjani Old Trafford kwa awamu ya mwisho ya muondoano ikitarajia kuongeza matumaini yake ya kutawazwa mabingwa wa Uingereza.


Chelsea nayo itakaribishwa na New castle kwa kivumbi kisichoweza kutabirika. Iwapo Man U itaicharaza West Ham, basi timu hiyo itakuwa inaelekea kutawazwa mabingwa wa Uingereza.


Chelsea itakuwa inajaribu kuongeza pointi zake angalau iifikie Man U itakapokutana na New Castle jumatatu. Mechi nne zilizopita Chelsea ilikuwa nyuma ya Man U kwa pointi nne jambo ambalo lilikuwa linaonyesha matumaini makubwa ya kombe la Uingereza kuangukia mikononi mwa Man U.


Lakini hayo yaligeuzwa wikendi iliyopita wakati Man-U ilipoalikwa na Chelsea uwanjani Stamford Bridge na kucharazwa mabao mawili kwa moja yaliyomfanya mchezaji wa kiungo cha kati wa Chelsea Michael Ballack ambaye alifunga mabao hayo kusema mchezo ushageuzwa na sasa Man-U ndio wanaotapa tapa.


Hata hivyo wingi wa mabao kwa timu ya Man-U unaipatia timu hiyo pointi nyingine moja, na iwapo itashinda mechi yake dhidi ya West Ham na baadaye ishinde mechi nyingine dhidi ya Wigan basi timu hiyo itakuwa na wakati mzuri wa kupumua.


Vijana wa Alex Ferguson hawawezi kuidharau timu ya West ham kwani timu hiyo ya London ilishinda mechi yake dhidi ya Man U msimu uliopita uwanjani Old Trafford wakati Carlos Tevez mchezaji wa Man U alikuwa angali anaichezea West ham.


Safari ya Chelsea kuelekea New Castle inakuja wakati timu hiyo imeanza kupata uhai chini ya mkufunzi Kevin Keegan kwani haijafungwa katika mechi saba iliyocheza.


Kwa mshambulizi wa Chelsea Didier Drogba ambaye aliisaidia timu hiyo kuingia katika fainali ya kombe la klabu bingwa ulaya ushindi wa nyumbani ni lazima kwani timu hiyo imeshinda ligi ya premier mwaka wa 2005 na 2006 chini ya mkufunzi wake wa zamani Jose Maurinho.


Keegan anasema timu yake lazima ifanye vibwanga mbele ya Chelsea, na iwapo hilo litaisaidia Man-U kushinda basi hilo halimhusu.


Kesho itakuwa siku kubwa kwa real Madrid kwani timu hiyo inatarajia kushinda kombe la ligi ya uhispania La liga kwa mara ya 31 na kuingia katika historia kama timu ya kwanza kushinda kombe hilo mara mbili mfululizo tangu mwaka wa 1990.


Lakini timu hiyo lazima ishinde mechi dhidi ya Osasuna au itarajie kwamba Villareal haitaifunga Getafe mapema hapo kesho.


Real ina pointi 10 ikifuatiwa na Vallareal alafu Barcelona ambayo inamenyana katika nambari tatu huku ikiwa imesalia na mechi nne tu.


Timu hiyo itakosa huduma za Guti aliepata jeraha la kifundo cha mguu lakini mshambulizi Ruud Van Nisterlrooy atakuwa uwanjani kuisaidia timu yake.


Osasuna inahitaji pointi zaidi ya Real kwani timu hiyo inashikilia nambari nne kutoka chini na pointi 40 pointi mbili zaidi ya Zaragoza na imesalia nafasi moja tu itakayoamua. Timu ya Levante tayari iko chini kihesabu Murcia yenye pointi 30 bila shaka itafuata mkondo huo huo.


Raundi ya 35 ya mechi hizo inaanza jumamosi wakati timu ya Atletico Madrid inakapomenyana na Recreativo Huelva.


Atletico inashikilia nambari nne licha ya kuonyesha mchezo usiovutia msimu huu. Racing Santander ambayo itakuwa na kibarua kigumu hapo kesho itakapokutana na Murcia imeachwa na Atletico kwa pointi mbili.


Rais wa Atletico anasema msimu huu umekuwa mgumu kwao na anatamani umalizike tuu timu yake ikiwa na nafasi ya kushiriki katika dimba la klabu bingwa ulaya.


Huelva kwa upande wake iko na pointi 40 sawa na Osasuna. Baadaye leo Zaragoza itaikaribisha Deportivo Coruna ambayo imepanda katika msimamo wa ligi hadi nambari saba katika wiki za hivi karibuni.


Kushindwa kwa Zaragoza katika mechi hiyo kutailetea timu hiyo mashaka zaidi na kuilazimisha imkaribishe tena mshambulizi Diego Milito kwa mikono miwili.


Sevilla inayoshikilia nafasi ya sita iko nyumbani kesho ikicheza na Valladolid huku Valencia ikikaribishwa na Barcelona.


Valencia haijapoteza uwanjani Nou Camp kwa miaka sita iliyopita na lazima itakuwa na matumaini makubwa hapo kesho haswa baada ya Barca kupoteza mechi ya nusu fainali ya Champions League kwa Manchester United.