Somalia bado hali ya usalama ni mbaya | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.02.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Somalia bado hali ya usalama ni mbaya

Serikali ya mpito yasema imeunda kikosi cha kupambana na ugaidi

Wanajeshi wa serikali ya mpito ya Somalia na wenzao wa Ethiopia, wakiwa katika harakati za ulinzi mjini Mogadishu.

Wanajeshi wa serikali ya mpito ya Somalia na wenzao wa Ethiopia, wakiwa katika harakati za ulinzi mjini Mogadishu.

Katika kupambana na ukosefu wa usalama katika mji mkuu wa Somalia-Mogadishu, serikali ya mpito inasema imeunda kikosi cha kupambana na ugaidi. Taarifa ya afisa mmoja wa wizara ya ulinzi imesema kikosi hicho kimepewa mafunzo na wanajeshi wa Ethiopia. Hayo yanafuataia mripuko uliowauawa watu wane jana mjini Mogadishu, huku bado wanajeshi wa kulinda amani wa nchi za kiafrika wakisubiriwa kuwasili nchini humo.

Naibu waziri wa ulinzi katika serikali ya mpito ya Somalia Salad Ali Jelle alikataa kutaja idadi ya wanajeshi watakaohusika katika harakati hizo za kupambana na ugaidi n, lakini afisa mwengine alisema ni karibu 700. Tangazo hilo linafuatia mripuko wa bomu lililotegwa garini hapo jana katika mji mkuu Mogadishu ambapo abiria wanne waliuwawa.

Hadi sasa hakuna aliyetangaza kuhusika na shambulio hilo lililotokea karibu na uwanja mmoja wa michezo kaskazini mwa mji mkuu, pamoja na kwamba baadhi ya mashahidi walisema gari hilo lilishambuliwa kwa kombora kutoka gari jengine.Hata hivyo Bw Jelle alisema watu wanne waliouwawa walikua ni washambuliaji wa kujitoa mhanga, ambao huenda hawakua na ufundi wa kufyatua miripuko.

Serikali ya mpito ingali ikikabiliwa na matatizo ya usalama, tangu mwezi uliopita baada ya wanajeshi wake wakisaidiwa na majeshi ya nchi jirani ya Ethiopia, kuwashinda wapiganaji wa mahakama za Kiislamu, waliokua wakiushikilia mji mkuu na sehemu kubwa ya kusini mwa Somalia tangu mwezi Juni mwaka jana.

Kwa upande mqwengine katika taarifa yake mjini Nairobi leo, Jumuiya ya kimataifa ya waandishi wasio na mipaka yenye makao yake makuu mjini Paris, imelaani mauaji ya Ijumaa iliopita ya mwandishi mmoja wa redio ya Kisomali , aliyepigwa risasi wakati akirudi nyumbani katika mji wa Baidoa. Ali Mohamed Omar aliyekua na umri wa miaka 25 alikua mtangazaji na fundi mitambo wa Redio Warsan na mwanaharakati wa chama cha waandishi habari nchini humo.

Wakati ukosefu wa usalama unaendelea, bado kikosi cha kulinda amani cha nchi za kiafrika hakijawasili, licha ya taarifa kwamba Uganda itatuma hivi karibuni wanajeshi kiasi ya 1,500, na Burundi ikiahidi kupeleka wanajeshi wapatao 1,700. Wito uliotolewa ni wa jumla ya wanajeshi 8,000 lakini ahadi zilizotolewa hadi sasa ni za karibu wanajeshi 4,000 tu, huku maafisa wa kibalozi wa nchi za kigeni ukiyataka mataifa tajiri kuusaidia kwa fedha ujumbe huo wa Umoja wa Afrika wa kulinda amani nchini Somalia.

 • Tarehe 19.02.2007
 • Mwandishi Mohamed Abdul-Rahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHJw
 • Tarehe 19.02.2007
 • Mwandishi Mohamed Abdul-Rahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHJw

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com