1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Soko la ajira Ujerumani.

Halima Nyanza7 Julai 2010

Jamii za walio wachache hapa Ujerumani mara kwa mara zimekuwa zikihangaika kupata kazi katika soko la ajira.

https://p.dw.com/p/ODMh
Baadhi ya jamii ya Wajerumani walio wachache.Picha: AP

Ingawa makampuni mengi ya Kijerumani yanaona kuwa na mchanganyiko wa tamaduni mbalimbali ni muhimu, lakini mara nyingi ni nadra kwa mameneja kuwatathmini wanaoomba kazi bila ya hisia za upendeleo.

Hivi sasa kuna mradi mpya wa kutathmini maombi ya kazi bila ya kuwepo majina ya waombaji katika fomu za maombi hayo.

Iwapo mtu mwenye jina la ukoo wa Kituruki anapowasilisha maombi ya  kutafuta kazi nchini Ujerumani, kuna uwezekano wa upungufu wa asilimia 14 ya kutopata jibu zuri katika maombi hayo, ukilinganisha na mtu mwenye jina la Kijerumani. Hiyo ni kwa mujibu wa shirika linalopinga hali za kibaguzi hapa nchini, ambalo limesema chuki na uongozi mbovu  unamaanisha waombaji wengi wa nafasi hizo za kazi wenye asili za jamii za walio wachache kamwe hawafikii hatua hiyo muhimu ya kufanyiwa mahojiano katika mchakato wa kazi hizo walizoziomba.

Lakini sasa  mradi mpya ulioanzishwa na wakala unaopinga ubaguzi unataka kujaribu uwezekano wa kuwa na mchanganyiko wa tamaduni mbalimbali katika nguvu kazi, bila ya kuanzisha sheria mpya.

Makampuni makubwa matano, yakiwemo kampuni la Proctor& Gamble na lile la L'Oreal yamekubali kutoonesha majina ya waombaji katika kipindi cha mwaka mmoja.

Tofauti na nchi nyingi zinazozungumza lugha ya kiingereza, maombi ya kazi nchini Ujerumani hujumuisha hasa picha, tarehe ya kuzaliwa, hadhi ya kifamilia na uraia wako.

Hatua ya kuanzishwa mradi huo ilitokana pia na utafiti ulioendeshwa na taasisi inayoshughulikia masuala ya utafiti wa ajira yenye makao yake mjini Bonn, ambapo katika utafiti wao  ulionesha kuwa mtu ambaye aliwasilisha maombi ya kazi, akiwa na shahada ya uzamili juu ya masuala ya sayansi, na mwenye uzoefu wa kazi hiyo, alikataliwa mara 230 katika maombi yake.

Hali hiyo ya kuchanganyikiwa kwa muombaji ilisababisha abadili jina lake la Ali na aamuwe kuomba kazi kwa jina la Alex, na pia kutumia jina la ukoo wa mkewe ambaye ni Mjerumani.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa shirika hilo linalopinga ubaguzi na lenye makao yake mjini Berlin, Christine Luders, anasema kuwa mradi huo wa kutathmini maombi bila ya kuwepo majina ya waombaji katika fomu za maombi ni wa hiari na kwamba shirika lao halina nia ya kushinikiza, kwa kutumia hatua za kisheria.

Amefafanua kwamba makampuni madogo, kwa mfano, yanaweza kuona vigumu kuchukuwa dhamana ya waombaji wa ajira wasiotaja majina.

Bibi Luders anasema pia kwamba malalamiko hayo yanaonesha wazi kwamba hakuna usawa nchini Ujerumani na kwamba pia wanadhani kwamba asilimia kubwa ya visa vinavohusiana na ubaguzi vimekuwa vikizimwa.

Ameongezea kusema kuwa kwa kutuma maombi bila ya kuandika majina ya waombaji katika fomu za maombi, kitu pekee ambacho ni muhimu ni sifa zinazostahili kwa muombaji katika kazi husika.

Mradi huo mpya wa kutathmini maombi bila ya kuwepo majina ya waombaji katika fomu unatarajiwa kuendelea mpaka mwaka ujao wa 2011, na  baada ya hapo matokeo muhimu yatachapishwa katika ripoti.

Miradi kama hiyo pia imewahi kufanywa nchini Ufaransa, Uswisi, Sweden na Marekani.

Mwandishi: Halima Nyanza

Mhariri: Miraji Othman