1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Socceroos wazidiwa nguvu na Uholanzi

19 Juni 2014

Australia walionyesha mchezo wa kujituma dhidi ya Uholanzi katika mchuano wa kundi B lakini vijana wa kocha Louis Van Gaal - Uholanzi waliwavunja moyo kwa kuwafunga magoli matatu kwa mawili.

https://p.dw.com/p/1CLjY
WM 2014 Gruppe B 2. Spieltag Australien Niederlande
Picha: picture-alliance/dpa

Baada ya kuwaona Uholanzi wakiwazaba Uhispania magoli matano kwa moja katika duru ya kwanza ya mechi za kundi B, Australia huenda walivuta pumzi na kufanya maombi kabla ya kuingia uwanjani dhidi ya Oranje mjini Porto Alegre. Na kwa dakika za kwanza sitini, mambo yalionekana ni kama maombi yao yamejibiwa.

Socceroos walionyesha ujasiri mbele ya vijana wa Louis Van Gaal. Mathew Leckie alikuwa moto wa kuotea mbali kwa upande wa Australia na alishirikiana vyema na mwenzake Mark Bresciano katika lango la Uholanzi. Na wakati Lecki, Bresciano na nahodha Tim Cahill wakiwahangaisha mabeki waUholanzi, mabeki wa Australia nao walikuwa chonjo dhidi ya Arjen Robben.

WM 2014 Gruppe B 2. Spieltag Australien Niederlande
Nahodha wa Asutralia Tim Cahill alifunga goli la kiufundiPicha: Reuters

Lakini Robben alifaulu kupenya na kuwapa Uhopanzi goli la kwanza katika dakika ya 20. Lakini hata kabla ya mashabiki wa Uholanzi kumaliza kushangilia hilo goli, Tim Cahill aliungahisha kombora kali hadi ndani ya lango na kufanya mambo kuwa moja kwa moja.

Kisha baadaye katika kipindi cha pili Australia wakapata penalty baada ya Daryl Janmaat kuunawa mpira kutokana na shuti iliyopigwa na mchezaji nguvu mpya Oliver Bozanic. Nahodha Mile Jedinak akafanya mambo kuwa mawili kwa moja. Dakika tatu baadaye, Robin Van Persie akasawazisha na kuwapa matumini Uholanzi.

Matokeo ya sare yangekuwa afadhali kwa Australia, ambao waliendelea kujituma hata baada ya saa moja kukatika. Lakini nguvu mpya wa Uholanzi Memphis Depay akasukuma wavuni shuti ya mbali ambayo kipa wa Asutralia Mathew Ryan alishindwa kuizuia. Hii ina maana kuwa safari ya Asutralia imefikia hapo baada ya kushindwa na Chile katika mechi ya kwanza. Sasa watapambana na Uhispania wakati Uholanzi wakishuka dimbani dhidi ya Chile Jumatatu ijayo katika mechi za mwisho za kundi B.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu