1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sipendi 'ku-tweet', nalazimika tu - Trump

Mohammed Khelef
18 Januari 2017

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, anasema kuwa hapendi kutumia mtandao wa Twitter kama anavyoambiwa, isipokuwa analazimika kwa kuwa amepoteza imani na vyombo vya kawaida vya habari.

https://p.dw.com/p/2W0Jn
US Präsident Donald Trump
Picha: picture-alliance/Photoshot

"Sipendi 'kutwiti'," Trump alikiambia kipindi cha "Fox & Friends" cha televisheni ya Fox News hivi leo (Jumatano, 18 Januari). 
"Nina mambo mengine ninayoweza kuyafanya, lakini siviamini kabisa vyombo vya habari, kabisa kabisa. Na hiyo ndiyo njia yangu pekee ya kuweza kujibu," alisema.

Tangu ashinde urais mwezi Novemba, bilionea huyo aliyewania kwa tiketi ya Republican amekuwa akiitumia Twitter kutoa matamko ya kiutawala, akizungumzia sera za mambo ya nje na hata kumshambulia yeyote anayemuandama.

Alipoulizwa ikiwa ataendelea Twitter baada ya kuapishwa rasmi kuwa rais hapo tarehe 20 Januari, Trump alisema: "Ndiyo!"

Mwishoni mwa wiki, bilionea huyo alishambuliwa vibaya mtandaoni baada ya kuhitalifiana na mtetezi wa haki za kiraia, John Lewis.

Lewis, mwenye umri wa miaka 76, alisema hatahudhuria kuapishwa kwa Trump, akilalamikia kile alichokiita "uingiliaji kati wa Urusi kwenye uchaguzi." 

"Mbunge John Lewis anapaswa kutumia muda mrefu zaidi kutatua matatizo ya jimboni kwake, ambalo liko hali mbaya na linasambaratika (sijataja uhalifu uliojikita huko) kuliko kulalamika kwa kuzua juu ya matokeo ya uchaguzi," aliandika Trump kwenye Twitter. "Wote kuongea, kuongea, kuongea - hakuna vitendo wala matokeo. Msiba!"

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahma