1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Singapore yaomboleza kifo cha baba wa taifa

Mohammed Khelef23 Machi 2015

Singapore iko kwenye maombolezo ya kifo cha kiongozi wake wa muda mrefu, Lee Kuan Yew, anayetukuzwa sana kwenye taifa hilo aliloliinua kutoka mji usio matumaini hadi ngome imara ya kiuchumi.

https://p.dw.com/p/1EvTc
Lee Kuan Yew
Lee Kuan YewPicha: Toshifumi Kitamura/AFP/Getty Images

Serikali ya Singapore imetangaza kuwa Lee aliyekuwa na umri wa miaka 91, alifariki dunia kwa amani masaa kadhaa kabla ya alfajiri ya leo katika Hospitali Kuu ya nchi hiyo, ambako alikuwa amelazwa tangu mwanzoni mwa Februari akisumbuliwa na homa kali ya mapafu.

Waziri Mkuu Lee Hsien Loong ambaye ni mtoto wa kiume wa Lee, alitoa tangazo la kifo cha baba yake huku machozi yakimtoka. Akizungumza kwa lugha tatu ambazo zinatumiwa na nchi hiyo - Kimalay, Kimandarin na Kiingereza - waziri mkuu huyo alisema Lee alijenga taifa na kuwapa raia wa taifa hilo utambulisho wa kujifaharisha nao.

"Hatutaweza kumuona mtu mwengine kama yeye. Kwa raia wengi wa Singapore na kwa hakika hata kwa wengine, Lee Kuan Yew, alikuwa ndiye Singapore," alisema Lee Loong.

Televisheni ya serikali ilikatiza matangazo yake ya kawaida na kuanza kurusha vipindi vinavyoelezea maisha na mafanikio ya Lee, huku mmoja wa watangazaji akikiita kifo hicho kuwa ni habari mbaya na ya kutisha. Punde, salamu za rambirambi zikaanza kumiminika kutoka viongozi kadhaa wakubwa duniani, akiwamo Barack Obama wa Marekani, Xi Jinping wa China na Waziri Mkuu Narendra Modi wa India.

Kiongozi wa watu

Serikali ya Singapore imetangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa, ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti, ingawa bado hakujatangazwa siku ya mapumziko na maisha ya kawaida yanaendelea. Kwa raia wengi wa nchi hiyo, Lee ni kiongozi wa kuliliwa kwa kile wanachosema kwamba ameijenga nchi ambayo imekiuka makosa ya kiutawala yaliyomo kwenye mataifa yaliyowazunguka - ghasia za kisiasa, ufisadi na uhalifu.

Mkuu wa serikali ya mji wa Hong Kong, Leung Chun-ying, akisaini kitabu cha maombolezo kwa kifo cha Lee Kuan Yew.
Mkuu wa serikali ya mji wa Hong Kong, Leung Chun-ying, akisaini kitabu cha maombolezo kwa kifo cha Lee Kuan Yew.Picha: Reuters

"Imani aliyotuonesha, ustahamilivu wake, imani yake, kujitolea kwake katika kuijenga Singapore na pia kutujenga sisi raia wa Singapore kuwa bora zaidi. Nadhani maneno yangu hayawezi kueleza hasa vile ninavyomfikiria," alisema mkaazi mmoja wa Singapore.

Lee alianzisha mfumo wa makaazi ambao unafadhiliwa na dola na ambao unamuwezesha kila raia kuwa na mahala pa kuishi, na licha ya wengine kumchukulia kuwa mtawala mbabe aliyeuangalia ulimwengu katika uhalisia mchungu, alijijengea heshima kubwa miongoni mwa raia wa Singapore, ambao mwaka huu wataadhimisha miaka 50 ya uhuru wa nchi yao bila ya kiongozi wao huyu - baba wa uhuru wa taifa hilo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman