1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Silaha Ukraine zahatarisha mpango wa amani

20 Novemba 2015

Shirika la OSCE limesema licha ya kuondolewa kwa vifaru vingi vya kivita katika eneo la usalama mashariki ya Ukraine bado kuna silaha nzito nzito kwenye eneo la mpakani na hivyo kuhatarisha mpango wa amani.

https://p.dw.com/p/1H9MJ
Ukraine Konflikt Frontlinie im Gebiet-Donezk
Picha: DW/I. Kuprijanova

Karibu kila wiki wasuluhishi kutoka Ukraine,Urusi,upande wa waasi wa Donetsk na Luhansk wanazozana kuhusu utekelezwaji wa mkataba wa amani wa Minsk. Mkataba huo unaonekana umeandikwa vizuri lakini shirika hilo la usalama linasema mambo ni tofauti katika utekelezaji haswa walipozuru eneo ambalo linakaliwa na waasi la Luhansk.

Naibu mwenyekiti wa ujumbe wa OSCE mjini Kieve,Alexander Hug amesema wawakilishi kutoka kile kinachoitwa Jamhuri ya watu wa Luhansk waliwaamuru wawaondoe waangalizi wao wawili.Lakini anasema si jukumu la waasi kutoa uamuzi huo. Kutokana na ukweli huo Hug anasema inaonesha ni kwa jinsi gani hali ya kutatizwa kwa mkataba wa Minsk inavyoongezeka.

Ni hivi maajuzi tu tarehe 9 mwezi Novemba ambapo pande zinazozozana zilikubaliana kuhusu kuondoka eneo hilo.Hug amesema kufikia sasa hawajaweza kushuhudia kuondolewa kwa hata silaha moja kutoka eneo hilo.

Hakuna utaratibu unaoonyesha jinsi mambo yanavyostahili kutekelezwa,utaratibu ambao unastahili kuwasilishwa na pande zote katika mzozo huo, Jeshi la Ukraine na wapiganaji wanaoiunga mkono Urusi.

Mkataba wa amani umekiukwa

Silaha kama bunduki kubwa zinapatikana eneo hilo la mpaka mahali ambapo hazistahili kuwepo kulingana na makubaliano ya Minsk.Kwa mujibu wa mkataba huo pia eneo la la kilomita 15 kuelekea mashariki na upande wa magharibi yanatakiwa kuwa bila ya wanajeshi.

Kulingana na makubaliano ya hivi karibuni,shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya linatakiwa pia kujenga makazi ya wachunguzi katika miji ya Horlivka na Debaltseve lakini kwa sasa wapiganaji wa upande wa waasi wanazuia hatua hiyo.

Pamoja na hayo milio ya risasi inaendelea kusikika katika maeneo kadhaa kuelekea kaskazini magharibi na magharibi ya eneo la waasi la Donetsk.Siku ya Jumatano waangalizi wa OSCE katika Donetsk walinakili milipuko 107 katika muda wa saa moja na nusu.

Ukraine yatishia kulipiza kisasi

Mapema wiki hii Ukraine ilitishia kurejesha silaha zilizokuwa zimeondolewa katika eneo hilo.

Msemaji wa majeshi ya Rais Petro Poroshenko wa Ukraine amesema nchi yake ina uwezo wa kuchukua hatua hiyo kwa kipindi cha muda mfupi na kwamba majeshi yao yako tayari kulipiza kisasi.Hii haionekani kuwa amani ya kudumu haswa kutokana na kutotekelezwa kwa vipengele muhimu vya mkataba wa Minsk.

Tarehe 31 Disemba Ukraine sharti ianze kuudhibiti tena mpaka wake na Urusi ingawa shirika hilo la usalama la Ulaya halina uwezo wa kuchunguza maeneo ya zamani ya mipaka. Kwenye mkutano uliowaleta pamoja viongozi wa Ujerumani,Urusi,Ufaransa na Ukraine mjini Paris mwezi Oktoba kundi hilo lilikubaliana kufanya uchaguzi utakaoidhinishwa na OSCE katika maeneo yaliyokaliwa mwezi Februari mwaka ujao.Lakini afisa wa kibalozi kutoka mataifa ya magharibi anayeyafahamu kwa kina makubaliano hayo ya Minsk ,amesema tarehe hiyo haiwezi kutekelezeka na anadhani uchaguzi huo utafanyika mwezi Aprili kwani ukifanyika mwezi Mei utaonesha ishara mbaya.

Kiew Ausländische Kämpfer Ukraine-Konflikt
Picha: DW/A. Savizki

Lakini kwanza bunge la Ukraine mjini Kiev litalazimika kukubaliana kuhusu mabadiliko ya katiba ambayo yamejadiliwa kwa miezi kadhaa yanayonuia kusambaza mamlaka nchini humo.Lakini zoezi hilo la linabidi lifanyike mapema kabla ya mwisho wa Disemba.

Rais Poroshenko anahitaji kuungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge na pia kura kutoka upande wa rais aliyeondolewa mamlakani Victor Yanukovych.

Mwandishi:Bernard Maranga/DW
Mhariri.Yusuf Saumu