1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya tatu ya michezo ya Olimpiki

Admin.WagnerD8 Agosti 2016

Michezo ya Olimpiki ya mjini Rio yaingia katika siku yake ya tatu rasmi,leo(08.08.2016) medali kadhaa za dhahabu zanyakuliwa hasa katika kuogelea, kulenga shabaha na kuinua uzito.

https://p.dw.com/p/1Jdbh
Rio 2016 Schwimmen Katie Ledecky USA
Katie Ledecky wa marekani akifurahia ushindi wake katika michezo ya RioPicha: Reuters/D. Gray

Na katika mchezo wa kuogelea jana Jumapili Michael Phelps alijitupa tena bwawani katika michezo ya mchujo katika kuogelea mita 200 mtindo wa kipepeo , mbali ya kunyakua medali yake ya dhahabu ya 19 katika olimpiki.

Mmarekani Katie Ledecky alivunja rekodi yake binafsi katika kuogelea kwa mita 400 mtindo huru jana usiku na kunyakua medali ya dhahabu kwa Marekani , akishinda kwa sekunde 5 zaidi ya mtu aliyemfuatia , na sasa analenga kunyakua pia dhahabu katika kuogelea mita 200 kwa wanawake hii leo. Baada ya kushinda jana alikuwa na haya ya kusema.

Rio 2016 Schwimmen Michael Phelps USA
Michael Phelps(kushoto) akishangiria ushindi katika kuogeleaPicha: Getty Images/AFP/O. Andersen

"Ni hisia za kushangaza , kuimba wimbo wa taifa na kuona bendera ikipandishwa, nataka kwenda kuimba pamoja na wenzangu katika timu kwa sauti za juu kabisa."

Sarah Sjostrom wa Sweden alishinda kuogelea mita 100 mtindo wa kipepeo na Adam Peaty wa Uingereza alinyakua nae dhahabu kabla ya kikosi cha Marekani cha waogeleaji kunyakua dhahabu katika mbio za mita 100 mara nne mtindo huru wa kuogelea.

Baada ya ushindi Adam Peaty alisema .

"Inafurahisha, nashindwa kuamini. Siwezi kwa kweli kuamini kilichotokea. Nitajipiga mara kadhaa kujua kama ni kweli. Kazi yote ngumu niliyofanya imeleta matunda."

Marekani sasa imekabana na Australia kwa kupata medali mbili kila moja za dhahabu.

Rio Momente 06 08 Fussball Brasilien gegen Irak Neymar
Neymar akishindwa kuamini baada ya kushindwa kufunga bao dhidi ya IraqPicha: Reuters/U. Marcelino

Nae Lilly King wa Marekani amelenga kunyakua medali ya dhahabu na hataki azma yake hiyo izuiwe na mtu yoyote , hususan bingwa wa dunia Yulia Efimova wa Urusi katika mchezo huo.

Efimova anaruhusiwa kushiriki mashindano hayo ya Rio kufuatia kupigwa marufuku kwa miezi 16 kwa kutumia madawa ya kuongeza nguvu misuli , doping na licha ya kugunduliwa tena na madawa hayo mwilini mwaka huu kwa kutumia dawa ya meldonium.

Mrusi huyo mwenye umri wa miaka 24 ni mmoja kati ya wanamichezo kadhaa wa Urusi waliohusika katika kashfa ya doping. Yeye pamoja na King watapambana katika fainali ya kuogelea mita 100 leo Jumatatu(08.08.2016).

Na katika soka , Brazil inakaribia kupata fadhaa nyingine ya kutolewa na mapema katika mashindano hayo katika ardhi ya nyumbani baada ya kikosi hicho kinachoongozwa na nyota Neymar kushindwa kuvuka kizingiti dhidi ya Iraq kwa kutoka sare ya bila kufungana, jana.

Rio Momente 06 08 Fussball Brasilien gegen Irak Neymar
Wachezaji wa Iraq wakimfariji Neymar baada ya sare bila kufungana kati ya Brazil na IraqPicha: Reuters/U. Marcelino

Wenyeji hao wa mashindano ya olimpiki wanapaswa sasa kuishinda Denmark siku ya Jumatano ili kuepuka kuyaaga mashindano hayo na mapema.

Ureno na Nigeria ni timu za kwanza kukata tikiti zao katika robo fainali kwa ushindi dhidi ya Honduras na Sweden. Argentina , Denmark na Mexico pia zilishinda michezo yao.

Uli Hoeneß
Uli Hoeness anataka kuwania kiti cha urais wa Bayern MunichPicha: Getty Images/Bongarts/L. Preiss

Ujerumani ilitoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Korea kusini mjini Salvador. Ujerumani iko katika nafasi ya tatu katika kundi C , pointi mbili nyuma ya Mexico na Korea kusini. Ujerumani inalazimika kuishinda Fiji kwa takriban mabao manne katika mchezo wa mwisho wa kundi lao ili kusonga mbele, iwapo mchezo wa mwisho wa Korea kusini na Mexico pia utamalizika kwa sare.

Rais wa Bayern Munich

Uli Hoenness anatarajiwa kurejea kama rais wa Bayern Munich baada ya mabingwa hao wa Ujerumani kusema leo kuwa ameamua kugombea uchaguzi ujao baada ya kuachiliwa kutoka kifungoni mwezi Februari mwaka huu baada ya kutumikia kifungo kwa kukwepa kulipa kodi.

Fußball Champions League Finale Atletico Madrid v Real Madrid Zidane
Kocha wa Real Madrid Zinedine ZedanePicha: Reuters/S. Rellandini

Klabu ya Inter Milan ya Italia imetangaza leo kwamba kocha wake Roberto Mancini ataachana na klabu hiyo , katika makubaliano ya pamoja , huku kukiwa na ripoti kwamba wamiliki wapya wa klabu hiyo ya Serie A kutoka Uchina wameamua kwamba damu mpya inahitajika kuijenga upya timu hiyo.

F.C. Internazionale Milano inathibitisha kwamba imeachana na kocha wake mkuu Roberto Mancini kwa makubaliano ya pande zote, klabu hiyo ilisema katika taarifa.

EUFA super cup

Nae kocha wa Real Madrid Zinedine Zidane amemjumuisha mwanae Luca katika kikosi chake cha awali kwa ajili ya pambano la Super Cup la UEFA dhidi ya Sevilla kesho Jumanne.

Luca anajiunga na kikosi hicho akiwa mlinda mlango wa tatu, akijaza nafasi ya Keylor Navas. Kiko Casilla huenda akaanza katika mchezo huo utakaopigwa kesho Jumanne.

Jana Manchester United ilinyakua taji lake la kwanza msimu huu katika enzi za kocha nyota Jose Mourinho baada ya kuwashinda mabingwa wa ligi ya Uingereza Leicester City kwa mabao 2-1 katika uwanja wa Wembley na kunyakua taji la ngao ya jamii.

Manchester United Manager Jose Mourinho
Kocha wa Manchester United Jose MourinhoPicha: picture-alliance/dpa/N. Roddis

Kocha wa Manchester United Jose Mourinho amesema klabu yake inapaswa kujisikia fahari kupata saini ya mchezaji mahiri wa kati Paul Pogba wakati mchezaji huyo Mfaransa anakaribia kujiunga na timu yake ya zamani kwa kitita cha juu kabisa duniani.

Pogba , mwenye umri wa miaka 23, anatarajiwa kukamilisha uhamisho kutoka Juventus Turin utakaoigharimu timu hiyo ya Manchester pauni za Uingereza milioni 89 sawa na euro milioni 105 baada ya timu hizo kuthibitisha jana Jumapili kwamba atafanyiwa uchunguzi wa afya leo Jumatatu.

Juergen Klopp arejea Mainz 05

Juergen Klopp alirejea jana Jumapili katika klabu yake aliyochezea kama mchezaji na pia kama kocha ya Mainz 05 na kurejea kwake hakukuwa na hisia za urafiki pale vijana wanaoongozwa na kocha Martin Schmidt walipokichambua kama karanga kikosi cha Juergen Klopp kwa mabao 4-0.

Baada ya Liverpool kuirarua FC Barcelona katika mchezo wa majaribio siku ya Ijumaa kwa kiwango hicho hicho cha mabao, Juergen Klopp hakuwa na jibu kwa uchu wa mabao wa timu yake hiyo ya zamani.

Fußball Europa League Borussia Dortmund - Liverpool
Kocha wa Liverpool ya Uingereza Juergen KloppPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Ufadhili wa michezo Tanzania

Na huko nchini Tanzania mashabiki wanajadili kwa karibu suala la wawekezaji ambao wamejitokeza kuzidhibiti timu maarufu za Simba na Dar Young Africans , Yanga zote za jijini Dar Es Salaam , na kutangaza fedha nyingi kuziendesha timu hizo kongwe.

Mwanachama na mpenzi wa Simba Mohammed Dewji maarufu kama Mo, ametangaza kuipatia Simba shilingi za Tanzania bilioni 20 ili kununua hisa za asilimia 51 katika klabu hiyo kongwe na pia Yusuf Manji ambaye ni mfadhili wa Yanga ametangaza kitita cha shilingi za Tanzania bilioni 50 kuiendeleza Yanga na kwamba anataka akodishwe klabu hiyo kwa muda wa miaka 10.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae / ape /

Mhariri:Iddi Ssessanga