1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya kimataifa ya uhaianuai yaadhimishwa leo

Charo Josephat22 Mei 2009

Ban Ki Moon atoa mwito uhai wa viumbe ulindwe duniani kote

https://p.dw.com/p/HvSF
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moonPicha: AP

Leo ni maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uhaianuai. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameonya kwamba kupungua kwa bioanuai ulimwenguni kunabakia katika kiwango cha kutisha, licha ya makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa kimataifa kuhusu maendeleo endelevu kupunguza kasi ya kupotea kwa uhai anuai kufikia mwaka 2010.

Katika kuadhimisha siku ya uhai anuai hii leo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kwenye taarifa yake amesema sababu zinazosababisha kupotea kwa kasi kubwa kwa uhai anuai ni pamoja na ukataji wa misitu, mabadiliko ya eneo la makaazi na mmomonyoko wa ardhi unaohusishwa na athari zinazosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kitisho kingine ni kuenea kwa aina mbalimbali ya viumbe katika maeneo mageni, jambo ambalo ndio kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya kimataifa ya uhaianuai.

Kama matokeo ya utandawazi, viumbe vya kigeni katika mazingira asili vinaathiri huduma kwenye mifumo ya ikolojia, hali ya maisha na uchumi wa nchi mbalimbali duniani kote. Serikali ya Afrika Kusini peke yake inatumia dola milioni 60 kila mwaka katika juhudi ya kuangamiza mimea kama vile miwati, ambayo inayaivamia ardhi inayofaa kwa kilimo, mifumo ya mito na maeneo ambayo ni vivutio vya utalii.

Katika eneo la maziwa makuu huko Amerika Kaskazini, kome wa pundamilia wanaathiri usafiri wa meli, shughuli za uvuvi na utengenezaji wa umeme kutokana na maji. Katika visiwa vyote vya bahari ya Pacific, panya kutoka meli za kigeni wanawaangamiza ndege asili.

Katika nchi nyingi barani Afrika, magugu yanamea kwenye mito na maziwa na hivyo kuhatarisha maisha ya viumbe wanaoishi katika maziwa na mito na hata wanyama pori wanaokwenda kunywa maji katika maeneo hayo. Viwanda na jamii zinazonufaika kutokana na maji ya mito na maziwa hayo pia zinakabiliwa na hatari.

Kuna mifano mingine mingi kudhihirisha vipi viumbe vya kigeni vinavyoathiri uhai anuai asili, kilimo, misitu, uvuvi na hata afya ya binadamu. Vitisho vya aina hii vinazidishwa makali na mambo mengine yanayosababisha kupotea kwa uhai anuai, hususan mabadiliko ya hali ya hewa. Athari zake katika juhudi za kupunguza umaskini, kuhakikisha kuwepo kwa maendeleo endelevu na kuyafikia malengo ya milenia ya Umoja wa Mataifa, ni kubwa mno.

Mkataba juu ya uhai anuai unazingatia kitisho cha aina za kigeni za viumbe kwa kuunda mikakati na miongozo ya kimataifa, kubadilishana habari na utaalam, na kusaidia kuratibu juhudi ya kimataifa. Njia muafaka na ya gharama ya chini ni kuzuia kuenea kwa viumbe katika mazingira ya kigeni.

Ili mkakati huu uweze kufanikiwa, unahitaji ushirikiano kati ya serikali mbalimbali, sekta za kiuchumi na mashirika yasiyo ya kiserikali na ya kimataifa. Taifa moja linaweza tu kuzuia kuvamiwa na viumbe kutoka sehemu nyingine ikiwa linafahamu ni aina ipi ya viumbe vinavyoweza kuvamia, vinaweza kutokea wapi na ni hatua zipi bora zinazofaa kukabiliana navyo.

Watu binafsi pia wana jukumu. Kufuata sheria za nchi na za kimataifa kuhusu karantini na forodha kutazuia kuenea kwa wadudu waharibifu wa mazao, magugu na magonjwa. Sheria rahisi inayotakiwa kufuatwa na kila mtu ni kuacha viumbe hai katika mazingira yao ya asili na kubeba tu kumbumbuku peke yake kupeleka nyumbani.

Mwaka ujao ni mwaka wa kimataifa wa uhai anuai. Mikutano muhimu inayotarajiwa kufanywa mwakani ni pamoja na mkutano wa kitengo cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa na mkutano wa kumi wa nchi zilizosaini mkataba wa uhai anuai, utakaofanyika mjini Nagoya nchini Japan. Matukio hayo yatasaidia kuunda mikakati ya siku za usoni ya kuhifadhi mifumo ya ikolojia duniani.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amesema kukabiliana na kuenea kwa viumbe hai katika mazingira mapya na kushughulikia sababu nyingine za kupotea kwa uhai anuai ni jukumu linalotakiwa kutimizwa kwa haraka. Kiongozi huyo amezitolea miito serikali, mashirika na watu binafsi kuongezea nguvu juhudi zao za kulinda uhai wa viumbe duniani.

Mwandishi:Josephat Charo/www.cbd.int

Mhariri:M.Abdul-Rahman