1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Si habari nzuri tu"

Maja Dreyer11 Oktoba 2007

Wahariri leo wanazingatia kuachiliwa huru Mjerumani aliyetekwa nyara, Rudolf Blechschmidt, huku Afghanistan pamoja na habari nyingine nzuri, yaani tuzo mbili za Nobel ambazo mwaka huu zimeenda kwa wanasayansi wa Kijerumani.

https://p.dw.com/p/C7lO

Tuanze basi huko Afghanistan. Licha ya furaha juu ya kurudi kwa mhandisi Rudolf Blechschmidt, mhariri wa “Mitteldeutsche Zeitung” ana wasiwasi, kwa sababu:

“Upande wa siasa, habari hizo za kuachiliwa Mjerumani si habari nzuri tu, kwa sababu inaonekana kama kwamba katika kumuokoa Mjerumani huyu, wanamgambo watano wa Taliban waliachiliwa kutoka gerezani. Huenda pia fedha zimelipwa. Watekaji nyara hawakuweza kutekeleza lengo lao kuu, yaani kwamba jeshi la Ujerumani liondoke Afghanistan. Hata hivyo, walitelekeza malengo mengine. Kwa hivyo, utaratibu huu mzima unaonyesha nguvu ya Wataliban na unaweza ukasababisha utekaji nyara mwingine.”

Ni dukuduku la mhariri wa “Mitteldeutsche Zeitung”. Gazeti la “Frankfurter Allgemeine” haliamini kwamba watekaji nyara ni Wataliban. Limeandika:

“Wataliban hawangekubali kupunguza madai yao. Ni kutokana na Wataliban kuendelea kupigania kutawala Afghanistan ndiyo kwamba nchi hii bado iko mbali sana kuwa na usalama wa uhakika na amani. Inabidi jumuiya ya kimataifa ijiulize kweli iko tayari kuchukua hatua zinazohitajika – kijeshi na katika kuijenga upya Afghanistan. Kimsingi, kazi muhimu ni kuwashinda wanamgambo. Bila shaka, hiyo haitawezekana kupitia njia ya kijeshi pekee, lakini bila ya jeshi vilevile ushindi huu hautapatikana.”

Baada ya kupata habari juu ya mapatano na watekaji nyara, mhariri wa gazeti la “Die Rheinpfalz” anauliza:

"Je, nani tena atatekwa nyara kwa lengo la kudai Wataliban wengine waachiliwe huru? Hata ikiwa fedha hazikulipwa, bado mkasa huo ni ushindi kwa Wataliban, kwa sababu serikali ya Afghanistan ilizungumza nao na iliyakubalia madai yao. Hakuna matumaini yoyote kwamba Wataliban watakubali kushindwa kijeshi. Kwa hivyo inabidi kuzungumza nao, angalau na wale ambao hawana msimamo mkali sana.”

Mada nyingine: Baada ya kuarifiwa kuwa mwanasayansi wa Ujerumani atapata tuzo la Nobel ya fani ya fizikia, jana Mjerumani wa pili alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo la kemia. Hilo hapa ni gazeti la “Stuttgarter Zeitung” juu ya matukio haya na matokeo yake:

“Watu wengi walishtushwa kwamba Ujerumani imepata hata zawadi mbili za Nobel katika fani za kisayansi. Hivyo ni wazi kwamba watu wengi hawakuamini kuwa sayansi ya Ujerumani inaweza kuwa na mafanikio makubwa kama haya licha ya kwamba wanasayansi hao Peter Grünberg na Gerhard Ertl wanajulikana sana katika fani zao. Miaka ishirini iliyopita ilikuwa jambo la kawaida kusherehekea wanasayansi wa Ujerumani kupewa tuzo ya Nobel.”

Na hatimaye ni gazeti la “Offenburger Tagblatt” ambalo linaonya:

“Kabla ya kufurahia mno tukumbuke kwamba kulingana na utafiti juu ya hali ya elimu, Ujerumani iko nyuma. Tukiwaangalia washindi hao wa tuzo ya Nobel ambao wote wawili wana umri wa zaidi ya miaka 70 tunaona kwamba kilele cha sekta ya sayansi nchini humu kimeshapita. Inabidi kuwekeza zaidi katika elimu na utafiti ili Ujerumani ibakie kuwa na umuhimu katika sekta ya sayansi na ustawi katika siku za usoni.”