1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanariadha washutumiwa kwa doping

4 Agosti 2015

Wiki tatu kabla ya kuanza michezo ya dunia ya riadha , michezo ya riadha imetumbukia katika mtafaruku kutokana na shutuma mpya kuhusu matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu misuli, Doping.

https://p.dw.com/p/1G97K
Symbolbild Leichtathletik Laufen
Wanariadha wakikimbia mbio ndefuPicha: picture-alliance/dpa/B. Thissen

Kituo cha matangazo ya televisheni cha Ujerumani ARD pamoja na gazeti la Uingereza la Sunday Times vimesema wamepata fursa ya kupata matokeo 12,000 ya uchunguzi wa damu kutoka kwa wanariadha 5,000. Majalada hayo yametokana na kituo cha kuhifadhi data cha shirikisho la kimataifa la vyama vya riadha duniani IAAF na taarifa hizo zimevujishwa na mtu aliyekuwa na nia ya kuweka wazi tatizo hilo, kwa mujibu wa ripoti.

Lakini shirika la kupambana na matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu katika michezo WADA limejibu shutuma hizo kwa kutoa wito wa kufanyika uchunguzi huru utakaofanywa na chombo huru.

Thomas Bach IOK Sitzung in Monaco 08.12.2014
Rais wa IOC Thomas BachPicha: Getty Images/T. Barson

Rais wa shirika la WADA Craig Reedie amesema jana kuwa ameshangazwa na kiwango cha madai hayo, ikiwa ni pamoja kwamba theluthi moja ya medali katika mbio mbali mbali katika michezo ya Olimpiki na mashindano ya ubingwa wa dunia katika muda wa miaka 10 iliyopita zimenyakuliwa na wanariadha ambao wana rekodi za kutia shaka katika uchunguzi wa doping.

Rais wa shirikisho la kimataifa la vyama vya riadha duniani IAAF Lamine Diack amesema kuna shutuma lakini hakuna ushahidi.

"Kuna madai yaliyotolewa , hakuna ushahidi. Inawezekana iwapo tutagundua kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwamba mtu ametumia madawa hayo, na hapo ndio tutakubali, lakini iwapo si hivyo haiwezekani."

Eröffnung Weltmeisterschaften Leichtathletik
Rais wa shirikisho la kimataifa la vyama vya riadha duniani IAAF Lamine DiackPicha: AP

Tume huru inayoongozwa na rais ambaye ni mwasisi wa shirika hilo la kupambana na madawa ya kuongeza nguvu misuli , Doping , WADA Dick Pound imesema leo mjini Kuala Lumpur kwamba anashaka iwapo adhabu za vikwazo kwa nchi zinaweza kutolewa kutokana na madai hayo ya doping.

"Katika wakati fulani IOC ina sheria kwamba unapaswa kutatua matatizo yote yanayohusiana na michezo iliyopita kabla ya kufungua mengine, kwa hiyo haiwezi kuendelea na kuendelea tu."

Wakati huo huo IOC imesema itachukua hatua dhidi ya mwanariadha yeyote anayeshiriki michezo ya Olimpiki iwapo atagundulika kuhusika katika madai haya mapya ya doping, amesema rais wa IOC Thomas Bach leo Jumatatu.

Joseph Blatter
Rais wa FIFA Sepp BlatterPicha: Reuters/A. Wiegmann

Bach amesema ni wajibu wa shirika la dunia la kupambana na matumizi ya madawa hayo kufanya uchunguzi juu ya madai hayo , ikiwa ni pamoja na theluthi ya medali katika mbio za masafa marefu na fupi pamoja na ubingwa wa dunia kwa mwaka 2001 hadi 2012 ambazo washindi ni wanariadha ambao matokeo yanatia shaka kuhusu uchunguzi wa damu.

"Iwapo kutakuwa na kesi zinazohusisha matokeo katika michezo ya Olimpiki , IOC itachukua hatua bila kumhurumia mtu kwa sera zetu za kawaida, lakini katika wakati huu hatuna kitu zaidi ya madai na tunapaswa kuheshimu dhana ya kutokuwa na hatia kwa wanariadha."

Mkuu wa shirikisho la vyama vya raidha duniani IAAF , Lamine Diack hata hivyo amesema leo(03.08.2015) mjini Kuala Lumpur kwamba kampeni ya kutaka kugawa kwa usawa medali inahusika na ripoti hizi za vyombo vya habari zinazodai matumizi makubwa ya madawa ya kuongeza nguvu misuli , Doping, katika michezo.

Blatter kuachia ngazi IOC

Rais wa FIFA Sepp Blatter ameondolewa uanachama wake wa afisa wazamani katika kamati ya kimataifa ya Olimpiki leo, miezi saba kabla ya wadhifa wake wa urais wa shirikisho hilo la kandanda duniani kuchukuliwa na mtu mwingine, amesema rais wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki IOC Thomas Bach, mjini Kuala Lumpur.

Blatter kwa kawaida angechaguliwa tena kwa kipindi kingine cha miaka minane katika kikao kinachoendelea cha IOC nchini Malaysia , pamoja na wenzake wengine kadhaa , lakini atatakiwa kujiuzulu atakapoiacha FIFA mwishoni mwa mwezi Februari.

Mwandishi: Sekione Kitojo dpae / afpe / rtre
Mhariri: Mohammed Khelef