1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shughuli zaendelea Zimbabwe licha ya Mgomo

Mwakideu, Alex15 Aprili 2008

Wananchi wa Zimbabwe wameendelea na shughuli za kawaida huku usalama ukidumishwa katika miji kadhaa nchini humo

https://p.dw.com/p/Di84
Kiongozi wa chama cha MDC Morgan Tsvangirai akiwa mahakamaniPicha: AP

Shughuli za kawaida zimeonekana zikiendelea nchini Zimbabwe licha ya chama cha upinzani nchini humo kuitisha mgomo wa kitaifa hadi pale matokeo ya uchaguzi wa machi 29 yatakapowekwa wazi.


Maduka na shughuli zengine za kawaida zinaendelea baada ya serikali ya kutoa onyo kali kwamba itakabiliana vilivyo na yeyote atakaeharibu amani.


Wakati huo huo Uingereza na Marekani zimedokeza kwamba zitazua mada kuhusu Zimbabwe katika kikao cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.


Kufikia sasa hakuna habari zozote za vurugu kutoka Zimbabwe. Walinda usalama nchini humo wameshika doria katika miji mikuu kufuatia onyo lililotolewa na serikali kwamba atakayevuruga amani atakabiliwa vilivvo.


Chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change kiliitisha mgomo baada ya mahakama nchini humo kutupilia mbali ombi lake la kuyaweka wazi matokeo ya uchaguzi wa Urais.


Makamu mwenyekiti wa chama hicho Thokozani Khupe anasema serikali inachelewesha matokeo hayo kwa kusudi.


Kiongozi wa chama hicho Morgan Tsvangirai anadai kwamba amemshinda Rais Robert Mugabe katika uchaguzi huo.


Wananchi wengi nchini humo wamemiminika katika mabenki kwa nia ya kuchukua hela za kutosha tayari kwa lolote litakalotokea. Maduka makubwa ya vyakula yameshuhudia msururu wa wananchi wanaonunua mikate. Hata hivyo baadhi ya wafanyibiashara wamefunga shughuli zao wakisubiri kuona matokeo ya mgomo.


Wananchi wengine wameonekana wakienda kazini kama kawaida huku wakidai kwamba hawakupokea habari zozote za mgomo.


Katibu mkuu wa chama cha upinzani MDC Tendai Biti amewataka wafuasi wa chama hicho wakae nyumbani na kujiepusha na vurugu.


Msemaji wa polisi nchini humo Wayne Byudzijena ameshutumu mgomo huo akisema upinzani una nia ya kuvuruga amani.


Vizuizi vya barabarani viliwekwa usiku wa kuamkia leo. Katika moja wapo wa vizuizi hivyo polisi wamekuwa wakishushwa abiria na kuwapekuwa kabla ya kuwaruhusu waendelee na safari yao.


Kulingana na Winnie Kaizare mfanyikazi katika benki moja nchini Zimbabwe hakuna lolote linaloweza kufanyika baada ya mahakama kukataa ombi la kuyaweka wazi matokeo ya uchaguzi. Anasema kila kitu nchini humo kinaendeshwa na serikali.


Hata hivyo mgomo huo haukutarajiwa kufaulu kwani imekuwa ngumu kwa migomo kufaulu nchini Zimbabwe katika siku za karibuni.


Mfumuko wa bei nchini humo umefikia asilimia laki moja, na zaidi ya asilimia themanini ya raia hawana kazi.


Hata hivyo Marekani na Uingereza zitawasilisha mgogoro wa Zimbabwe katika kikao cha kesho cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa licha ya Africa Kusini kupinga hatua hiyo.


Kikao hicho ambacho kinaandaliwa Africa Kusini kinatarajiwa kujadili ushirikiano wa kudumisha usalama kati ya Umoja wa Mataifa na Jumuia ya Africa.


Viongozi wanaotarajiwa kuhudhuria ni Rais wa Africa Kusini Thabo Mbeki, na wenzake kutoka jamhuri ya demokrasia ya Congo, Ivory Coast, Somalia na Tanzania pamoja na mawaziri wakuu wa Uingereza Gordon Brown na wa Italy Romano Prody.


Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Dumisani Kumalo kutoka Africa Kusini amesema mgogoro wa Zimbabwe haupaswi kujadiliwa katika kikao hicho kwani unajadiliwa vizuri kwa ushirikiano wa nchi jirani zinazounda SADC.


Mnamo jumapili viongozi wa SADC waliitisha kikao cha dharura nchini Zambia ili kushinikiza kuwekwa wazi kwa matokeo ya uchaguzi wa Urais.