Shrika la Ujerumani la kupambana na ukoma na kifua kikuu latoa ripoti ya mwaka | Masuala ya Jamii | DW | 10.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Shrika la Ujerumani la kupambana na ukoma na kifua kikuu latoa ripoti ya mwaka

Shirika la misaada kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa ukoma na kifua kikuu la hapa Ujerumani, Deutsche Lepra und Tuberkulosehilfe, DAHW, limekamilisha miaka 50 tangu lilipoanzishwa mnamo mwaka wa 1957. Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana hapa mjini Bonn shirika hilo limetoa ripoti yake ya mwaka jana 2006.

Msichana wa kihindi anayeugua ukoma

Msichana wa kihindi anayeugua ukoma

Ripoti ya shirika la Ujerumani linatoa misaada kusaidia juhudi za kupambana na ugonjwa wa ukoma na kifua kikuu duniani, DAHW, inasema mbali na kiwango cha fedha kilichotolewa kuwasaidia waathirika wa janga la tsunami barani Asia na watu walioathirika kutokana na tetemeko la ardhi nchini Pakistan, mwaka jana 2006 ulikuwa mgumu kidogo kifedha.

Jürgen Hammelehle, kiongozi wa shirika hilo anasema walipokea euro zaidi ya milioni 13 kupitia michango, urathi, uuzaji wa mali na faini zilizotozwa. Mwaka juzi 2005 shirika la DAHW lilipokea kiwango cha zaidi ya euro milioni 17, zikiwemo euro milioni nne za misaada ya kiutu.

Changamoto kubwa inalolikabili shirika hilo ni kutoshughulikiwa ugonjwa wa kansa ya Buruli. Katibu katika wizara ya ushirikiano na maendeleo ya hapa Ujerumani, BMZ, Karin Kortmann, amesema shirika la DAHW linatoa misaada kwa ajili ya magonjwa ambayo hayashughulikiwi kikamilifu. Magonjwa ya kuambukiza ambayo hugunduliwa kuchelewa katika maeneo mbalimbali barani Afrika huathiri, mifupa na ngozi huku wanaothiriwa zaidi wakiwa ni watoto.

Bi Karin Kortmann anasema changamoto kubwa katika vita dhidi ya ukoma na kifua kikuu ni mifumo dhaifu ya afya.

´Changamoto zilizopo ni kama ilivyokuwa hapo zamani. Mifumo ya utoaji huduma za afya iliyopo ni dhaifu. Tunahitaji vituo zaidi vya afya ambavyo watu wataweza kuvifikia kwa kutembea kwa miguu. Inapaswa fedha zaidi zitolewe kuwekeza katika utoaji wa mafunzo kwa wafanyakazi wa afya, madaktari, lakini pia katika sekta nzima ya afya.´

Ili kuweza kutoa huduma za matibabu na ushauri kwa wagonjwa wa ukoma na kifua kikuu nchini Togo, shirika la DAHW linataka kujengwe zahanati nchini humo na kufanywe kampeni za kuwahamasisha wananchi. Jamii nyingi barani Afrika huwanyanyapaa wagonjwa wa ukoma na kifua kikuu na kwa maoni yake Bi Karin Kortmann wa shirika la BMZ anasema tatizo hili linasababishwa na ukosefu wa elimu juu ya magonjwa hayo.

´Unyanyapaa wa wagonjwa wa ukoma na kifua kikuu kama ujuavyo aidha unaonyesha hakuna elimu au watu hawafahamu kwamba magonjwa haya ni ya kuambukiza na yanaweza kumpata mtu yeyote. Cha muhimu zaidi ni kuwafanya wagonjwa waweze kukubalika na kupewa kipaumbele katika jamii. Ipo haja ya kufanya kampeni za kuwahamasisha watu kuhusu vipi magonjwa haya yanavyoambukiwa, ili waondokane na hofu.´

Shirika la DAHW linadhamini miradi 135 ya kupambana na kifua kikuu katika nchi nane miongoni mwa nchi 22 zilizokabiliwa zaidi na tatizo hilo duniani kote. Miradi hiyo inajumulisha huduma za matibabu katika vitongoji vya miji mikubwa na miradi maalum kwa wagonjwa wa kifua kikuu wanaougua pia ukimwi. Changamoto kubwa katika siku za usoni itakuwa vipi kupambana na aina ya ugonjwa wa kifua kikuu ambayo imekuwa sugu kwa dawa. Matibabu kwa sasa yanakadiriwa kugharimu euro 10,000 kwa kila mgonjwa.

Ripoti ya shirika la DAHW inasema mwaka jana shirika hilo lilipokea kiasi cha euro milioni 18.9. Kwa kudhamini miradi 320 katika nchi 36, zilitumika takriban euro milioni 14.8. Thuluthi mbili ya kiwango hicho kilitumika kugharamia matibabu, na thuluthi moja ikatumika kwa ajili ya kuwasaidia na kuwajumulisha katika maisha ya kawaida watu waliopona kutokana na ukoma na kifua kikuu.

 • Tarehe 10.08.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHjn
 • Tarehe 10.08.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHjn