1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shinikizo la Ufaransa dhidi ya Iran

Oummilkheir21 Septemba 2007

Sarkozy anahisi nmazungumzo hayatoshi kuitanabahisha Iran

https://p.dw.com/p/CH7v
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy
Rais wa Ufaransa Nicolas SarkozyPicha: picture-alliance/dpa

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy anasema “hataki vita”, lakini anaituhumu Iran kutengeneza bomu la kinuklea.Hoja zake zimesutwa na mkurugenzi mkuu wa shirika la nishati ya atomiki ulimwenguni-AIEA,Mohammed El Baradei.

Iran inajaribu kujitengenezea bomu la kinuklea” amesema rais Nicolas Sarkozy kupitia vituo viwili vya televisheni vya Ufaransa France 2 na TF1 .

“Nimeshasema,jambo hilo halikubaliki,na ninawaambia wafaransa-halikubaliki”-amesisitiza kiongozi huyo wa Ufaransa.

Kadhia ya nuklea ya Iran “ni kadhia tete kupita kiasi,lakini Ufaransa haitaki vita” ameongeza kusema Nicolas Sarkozy.

Kiongozi huyo wa Ufaransa amejitenganisha kidogo na msimamo wa waziri wake wa mambo ya nchi za nje Bernard Kouchner,aliyezusha wahka nchini Ufaransa kwenyewe na kwengineko ulimwenguni alipotamka jumapili iliyopita tunanukuu”ulimwengu unabidi ujiandae kwa balaa-yaani vita pamoja na Iran” mwisho wa kumnukuu.

“Nisingetumia neno “vita”,lakini mwenyewe,ameshajieleza” amesema rais Sarkozy.

Lakini alikua kiongozi huyo huyo wa Ufaransa aliyezungumzia Agosti 27 iliyopita juu ya kile alichokiita “bomu la Iran au kupigwa mabomu Iran.”

Hoja za rais huyo wa Ufaransa zimesutwa na mkuu wa shirika la kimtaifa la nishati ya atomiki Mohammed El Baradei.”Iran si kitisho kwa sasa kwa jumuia ya kimataifa” amesema El Baradei pembezoni mwa mkutano wa baraza kuu la shirika hilo mjini Vienna-Austria.

Iran haikufichua bado vipengee vyote vya mradi wake wa kinuklea,lakini bado mpaka sasa hatukupata ishara ya miale yoyote ya sumu iliyotapakaa wala kugundua vituo vya chini kwa chini.”Amesema mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa la nishati ya atomiki-Mohammed El Baradei aliyeshauri mazungumzo yaendelezwe pamoja na Iran na kutanguliza mbele amani.

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy anajiuliza:

“Vipi jumuia ya kimataifa inaweza kuitanabahisha Iran kama ilivyofanikiwa kuzitanabahisha,Korea ya kaskazini na Libya?

Kwa njia ya mazungumzo,majadiliano au kwa vikwazo?Ikiwa vikwazo vya kimataifa havitoshi basi mie nashauri viwekwe vikali zaidi..

Serikali ya Paris inataka umoja wa ulaya uiwekee Iran vikwazo,mbali na vile vya Umoja wa mataifa ili kuilazimisha iachane na mpango wake wa kurutubisha maadini ya uranium . Serikali ya Ufaransa imeyasihi makampuni ya nchi hiyo yasijibu maombi mepya ya Iran.

Msimamo huo mkali umelengwa kuuzindua ulimwengu na wafaransa jinsi harakati za kinuklea zinavyosonga mbele nchini Iran.

Serikali ya mjini Teheran kila kwa mara imekua ikikanusha,haina azma ya kutengeneza silaha za kinuklea na kwamba mipango yake imelengwa kwaajili ya matumizi ya amani.

Wahariri kadhaa na wakuu wa kisiasa wanahisi msimamo wa Ufaransa unajongelea sana na ule wa Marekani katika kadhia hii ya nuklea ya Iran na ndio sababu mojawapo ya ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje Bernard Kouchner mjini Washington.

Mzozo wa kinuklea wa Iran unatazamiwa kuhanikiza pia mkutano wa baraza kuu la Umoja wa mataifa wiki ijayo mjini New-York.