1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shell kuwafidia Wanigeria dola milioni 84

Mohammed Khelef7 Januari 2015

Kampuni ya Shell italipa fidia ya dola milioni 84 kufuatia kuvuja kwa mabomba ya mafuta nchini Nigeria, hatua inayoweza kufungua njia ya kufidiwa hasara zinazosababishwa na kampuni za mafuta duniani.

https://p.dw.com/p/1EG0M
Uchafuzi wa mazingira kutokana na kuvuja kwa mafuta kwenye jimbo la Niger Delta.
Uchafuzi wa mazingira kutokana na kuvuja kwa mafuta kwenye jimbo la Niger Delta.Picha: picture-alliance/dpa/EPA/Marten Van Dijl

Wanavijiji 15,600 kwenye jimbo la Niger Delta watapata dola 3,300 kila mmoja, huku dola milioni 30 zikiingizwa kwenye mfuko wa jamii kwa ajili ya maendeleo ya vijiji vyao.

Hata hivyo, kampuni ya uwakili ya Leigh Day jijini London, Uingereza, ambayo ndiyo iliyofikia makubaliano hayo na Shell kwa niaba ya wakulima hao wa Nigeria, ilisema ni jambo linalokera kwamba imechukuwa miezi sita kwa kampuni tanzu ya SPDC kukubali kwamba ilifanya makosa na kufikia makubaliano ya fidia.

Pamoja na kukiri kwamba makosa kwenye ufungaji wa mabomba ulisababisha kuvuja kwa mafuta, Shell imeendelea kusisitiza kwamba sehemu kubwa ya uharibifu wa mazingira nchini Nigeria husababishwa na hujuma dhidi ya mabomba hayo, uchimbaji haramu wa mafuta na majaribio ya wizi.

Mwisho wa miaka 3 ya vita vya kisheria

Makubaliano hayo ya leo (Jumatano, 07 Januari) yanahitimisha miaka mitatu ya vita vya kisheria nchini Uingereza juu ya uvujaji mafuta wa mwaka 2008 ambao uliharibu maelfu ya ekari za miti ya mikoko na samaki, ambavyo vilikuwa njia kuu ya uchumi kwa wanakijiji wa jamii ya Bodo kusini mwa Nigeria.

Mutiu Sunmonu, mkurugenzi wa Shell Nigeria, ambayo inamilikiwa kwa asilimia 55 na serikali ya nchi hiyo, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba ilikuwa dhamira ya kampuni yake kuwalipa fidia wakulima hao tangu awali, ingawa hakueleza ni kwa nini ikachukuwa kipindi kirefu cha kupambana kisheria kabla ya kutoa fidia hiyo.

Mvuvi kwenye Niger Delta akipita na kidau chake kwenye eneo lililochafuliwa na mafuta yanayovuja.
Mvuvi kwenye Niger Delta akipita na kidau chake kwenye eneo lililochafuliwa na mafuta yanayovuja.Picha: Mazen Saggar/UNEP

Hata hivyo, wanasheria wanaowawakilisha wakulima hao wanasema hata baada ya kukubali kulipa, Shell awali ilikuwa tayari kutoa fidia ya dola 6,000 tu kwa jamii nzima ya wanakijiji.

Miaka 30 yahitajika kuisafisha Ogoniland

Mwenyekiti wa Baraza la Machifu na Wazee wa Bodo, Chifu Sylvester Kogbara, amesema anatazamia kuanzia sasa Shell itaziheshimu jamii wenyeji na kwamba italisafisha eneo zima la Ogoniland.

Kogbara ameliambia shirika la habari la AP kwamba watazitumia fedha za mfuko wa jamii kujenga miundombinu ya huduma za msingi kama vile hospitali, skuli na usambazaji wa maji safi.

Ripoti ya Shirika la Mazingira wa Umoja wa Mataifa inakisia kwamba itachukua hadi miaka 30 kuweza kulirejesha eneo hilo la Ogoniland kwenye haki yake ya kawaida, na ambalo kwa miongo kadhaa wakulima wamekuwa wakipambana na kampuni ya Shell.

Mwaka 1995, serikali ya Nigeria ilimnyonga mtetea haki za watu wa Ogoniland, Ken Saro-Wiwa, ambaye aliwaongoza watu wake kupinga uchafuzi wa mazingira wa kampuni ya Shell ambao umekuwa ukiendelea tangu mwaka 1956.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AP/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga