1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio la kisu lamjeruhi mgombea wa umeya Cologne

17 Oktoba 2015

Mgombea wa kujitegemea wa kiti cha umeya katika mji wa Cologne nchini Ujerumani amejeruhiwa vibaya baada ya kuchomwa kisu wakati wa kampeni katika mji huo wa Ujerumani magharibi Jumamosi (17.10.2015).

https://p.dw.com/p/1Gpns
Mgombea wa umeya wa mji waKöln Henriette Reker.
Mgombea wa umeya wa mji waKöln Henriette Reker.Picha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Henriette Reker mgombea wa kujitegemea ambaye anaungwa mkono na chama cha kihafidhina cha Kansela Angela Merkel na vyama vyengine viwili amepigwa kisu shingoni wakati akiwa kwenye soko Jumamosi asubuhi katika kitongoji cha Braunsfeld taarifa ya serikali ya jiji imesema maisha yake hayako hatarini.

Watu wengine wanne walijeruhiwa mmoja akiwa amejeruhiwa vibaya wakati walipokuwa wakijaribu kumdhibiri mshambuliaji ambaye inaonekana kama ana matatizo ya akili.Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 44 ametiwa nguvuni na dhamira ya shambulio hilo haijulikani ingawa alisikika akitamka kwamba ametenda hayo kutokana na sera ya wakimbizi ya mgombea huyo wa umeya.

Gazeti la "Rheinische Post " limekuwa na maelezo tafauti juu ya shambulio hilo ambapo likimkariri Mwenyekiti wa chama cha CDU kwa mji wa Cologne Bernd Petelkau ambaye alikuwa shuhuda wa shambulio hilo amesema Reker alijeruhiwa vibaya baada ya kuchomwa kisu tumboni na kwamba mshambuliaji alionekana kuwa ni mtu mwenye asili ya Ujerumani.

Gazeti la "Kölner Stadt Anzeiger " limeripoti kwamba mgombea huyo wa umeya amechomwa kisu shingoni.

Kwa mujibu wa mashuhuda mshambuliaji moja kwa moja alikwenda kumvamia Reker na kwamba alikuwa ndio ikwanza amewasili na kugawa mawaridi pamoja na kuzungumza na wanachama wa kundi lake la kampeni.

Shambulio lazusha fadhaa

Shambulio hilo limetokea wakati Reker alipokuwa akilitembelea banda la kampeni lililowekwa na chama cha Angela Merkel cha CDU kabla ya uchaguzi huo wa Jumapili.Reker mwenye umri wa miaka 58 alikuwa mkuu wa idara ya serikali ya jiji ya masuala ya jamii na kujumuishwa kwenye jamii tokea mwaka 2010.

Hali ilivyokuwa katika eneo la shambulio. (17.10.2015)
Hali ilivyokuwa katika eneo la shambulio. (17.10.2015)Picha: picture-alliance/ANC ESSEN/dpa

Waziri wa sheria wa serikali kuu ya Ujerumani wa chama cha SPD Heiko Maas amelilani shambulio hilo kuwa ni kitendo cha uovu kisichoigia akilini wakati waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westphalia Hannelore Kraft pia wa chama cha SPD ameandika kwenye mtandao wake wa Twitter "hili ni shambulio kwetu sote."

Meya anayemaliza muda wake Juergen Roters amesema ameshtushwa sana na shambulio hilo na mpinzani mkuu wa Reker katika uchaguzi huo Jochen Ott wa chama cha sera za mrengo wa wastani kushoto cha SPD amesitisha kampeni zake.

Uchaguzi kufanyika kama kawaida

Hata hivyo maafisa wa jiji wamesema uchaguzi huo utafanyika kama ilivyopangwa hapo Jumapili ambapo Reke ni mmojwapo wa wagombea wenye kuwekewa matumaini miongoni mwa wagombea saba wa uchaguzi huo awali iliopangwa kufanyika Septemba 13 lakini umeaihrishwa kwa wiki tano kutokana na sababu za hiltafu za taratibu za uchaguzi.

Bango la kampeni katika eneo la tukio (17.10.2015)
Bango la kampeni katika eneo la tukio (17.10.2015)Picha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Mashambulizi dhidi ya wanasiasa ni jambo la nadra nchini Ujerumani licha ya kwamba kuliwahi kutokea mashambulizi yaliyogonga vichwa vya habari ikiwa ni pamoja na kupigwa risasi kwa aliyekuwa wakati huo waziri wa mambo ya ndani Wolfgang Schauble na mtu mwenye matatizo ya akili wakati akiwa katika kampeni hapo mwaka 1990.

Miezi michache kabla ya hapo mwanamke mwenye matatizo ya akili alimchoma kisu Oskar Lafontaine wakati huo akiwa mwananachama mashuhuri wa chama kikuu cha upinzani nchini Ujerumani wakati akiwa kwenye kampeni mjini Cologne.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/Reuters/dpa

Mhariri : Isaac Gamba