1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio dhidi ya waasi wa LRA wa Uganda linaweza kusababisha hatari kubwa.

Mohamed Dahman9 Juni 2008

Tishio la shambulio la vikosi vya kanda dhidi ya waasi wa LRA wa Uganda lina nafasi ndogo ya ulitokomeza kundi hilo na hata kusababisha hali ya ukosefu wa utulivu kuwa mbaya zaidi katika eneo zima la Afrika ya kati.

https://p.dw.com/p/EG2s
Kiongozi wa waasi wa LRA Joseph Kony.Picha: AP Photo

Inaelezwa kwamba shambulio hilo linaweza kuandamana na hatari kubwa.

Matarajio ya kurudi vitani yameongezeka tokea kushindwa kwa mazungumzo ya kukomesha miongo miwili ya mzozo hapo mwezi wa April wakati kiongozi wa waasi hao Joseph Kony alipowaacha wasuluhishi wakimsubiri kwa siku kadhaa kichakani bila ya kujitokeza.

Kile kilichoonekana kama kipengele kikuu cha utata katika mazungumzo ilikuwa iwapo au la Kony ambaye anatafutwa na Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu anaweza kukwepa kushtakiwa ikiwa atatoka kichakani lakini hata hivyo pande zote mbili kila moja ilikuwa na mashaka ya nia njema kwa mwenzake kuanzia mwanzo kabisa mwa mazungumzo hayo.

Uganda wiki iliopita ilikubaliana na Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kupambana na waasi wa Kony iwapo waasi hai hawatorudi kwenye mazungumzo.Uwezekano wa kuzuka kwa vita umeonekana mkubwa zaidi tokea shambulio la waasi hao wa LRA kuuwa watu 23 kusini mwa Sudan wiki iliopita mahala pale pale ambapo maafisa wa serikali za mitaa walikuwa wakijaribu kuleta upatanishi.

Mchambuzi wa Uganda Levi Ochieng amesema mchakato wa amani hauna mwelekeo lakini hatua ya kijeshi pia ni kazi pevu na sio tu kwa sababu mahala walipo makamanda hao wa LRA bado hakujulikani.

Ochieng anasema ni kwa kuaguwa tu kwamba hawajui nguvu za Kony,kujiandaa kwake au wa jeshi ambalo litakwenda kumsaka.

Uganda siku hizi sio nchi inayoathirika zaidi moja kwa moja na taathira za vita kaskazini mwa nchi hiyo ambapo vimeuwa maelfu ya watu na kuwapotezea makaazi wengine milioni mbili.

Waasi hao wamehamia kupindukia mpaka wa Uganda na kuingia kwenye maeneo yasioweza kuingilika kabisa duniani ambapo wamekuja kuwa sababu ya kudhoofisha eneo hilo kutokana na mizozo kadhaa ya kuwania utajiri wa mafuta na madini.

Kwa miaka mingi waasi hao walikuwa wamepiga kambi kwenye milima ya Imatong kusini mwa Sudan kabla ya kuhamia kwenye misitu ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo hapo mwaka 2005. Wanaogopewa sana na wenyeji wa nchi zote hizo ambao wao wenyewe ndio kwanza wameibuka kutoka kwenye vita vyao wenyewe kwa wenyeqwe viliodumu kwa muda mrefu.

Mbali na kushambulia kusini mwa Sudan wapiganaji wa Kony mwaka huu pia walishambulia Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuzidi kuukaribia mzozo wa Dafur wenye kupambanisha jeshi la Sudan ya kaskazini. waasi wa Dafur,Chad na wapiganaji wanaotaka kuipinduwa serikali ya Chad.

Wakuu wa usalama kutoka Uganda , Congo na Sudan walikubaliana wiki hii kwamba vikosi vya serikali ya Congo vitaongoza shambulio lolote lile kwa Kony klwa msaada wa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa walioko Congo.

Wale wanaounga mkono hatua ya kijeshi hoja yao ni kwamba hatua nyengine za mbadala ni chache baada ya mazungumzo ya amani yanayoungwa mkono na mataifa ya magharibi kushindwa kuwasadikisha waasi wanaoshtakiwa na mahkama ya uhalifu ya Kimataifa kwa mauaji,ubakaji na utekaji nyara maelfu ya watoto.

Mmojawapo wa wanadiplomasia wa mataifa ya magharibi aliehusika na mazungumzo hayo katika mji mkuu wa Sudan Kusini amesema mchakato wa kisiasa huko Juba umemalizika na kwamba hayo yamedhirishwa na waasi wa LRA wenyewe wakati waliposhambulia Nabanga kusini mwa Sudan hivi karibuni na kuuwa watu 23 wakiwemo wanajeshi 14 wa kusini mwa Sudan.

Kuna wanaohofu kwamba iwapo kundi hilo halitodhibitiwa Kony anaweza kuuza huduma zake kwa yule mwenye kutowa malipo ya juu kwa kukifanya kikosi chake chenye silaha na uzoefu kuwa cha kukodiwa.

Wapiganaji hao wa LRA kwa hakika wanaweza kuleta athari kwa uwiano wa vikosi kwenye mizozo mengine.

Wale wanaopinga kushambuliwa kwa waasi hao wanatabiri yumkini shambulio hilo likashindwa na kupelekea maafa makubwa ya kijeshi ambapo itakuwa rahisi kuwaathiri raia wa Congo kutokana na mashambulizi ya kulipiza kisasi kwenye maeneo yanayodhibitiwa na waasi.