1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali yakubali kuwarudisha kazini Majaji

16 Machi 2009

Kiongozi wa upinzani Nawaz Sharif afutilia mbali maandamano

https://p.dw.com/p/HCov
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Pakistan Muslim League (N), Nawaz SharifPicha: AP

Nchini Pakistan, saa chache kabla ya kuanza maandamano yaliyokuwa yamepangwa na vyama vya upinzani mjini Islamabad, serikali imekubali kuwarudisha kazini majaji na kumaliza harakati za kuwazima wanaharakati wa upinzani. Waziri mkuu, Yousuf Raza Gilani, amesema kwamba majaji wote, akiwemo jaji mkuu, Iftakhar Chaudhry, waliotimuliwa kazini na utawala uliopita wa rais Pervez Musharraf watarudi kazini kuanzia Marchi 21.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema hatua hiyo ya serikali ya kuwarudisha kazini majaji wote miaka miwili baada ya kutimuliwa kazini na utawala uliopita itaipa Pakistan utawala wa kisheria unaohitajika kwa hali zote, na kutoa ushindi kwa kiongozi wa upinzani, Nawaz Sharif.

Mapema leo, waziri mkuu wa Pakistan, Yousouf Raza Gilani, akihutubia taifa, alitangaza kwamba majaji wote, akiwemo jaji mkuu, Iftikhar Chaudhry, watarudi kazini kuanzia tarehe 21 mwezi huu wa Machi. Uamuzi huo umekuja baada ya kufanyika mikutano kadhaa kati ya waziri mkuu huyo, mkuu wa majeshi, Ashfaq Kayani, na rais Asif Ali Zardari ili kuepusha umwagikaji wa damu na hali tete katika taifa hilo, mshirika mkubwa wa Marekani katika vita dhidi ya ugaidi.

Waziri mkuu wa zamani na kiongozi wa upinzani, Nawaz Sharrif, aliyewakusanya wapinzani wa rais Zardari na kuwaongoza maelfu ya watu katika maandamano nje ya mji wa Lahore ameipongeza hatua ya serikali na kuyafutilia mbali maandamano makubwa yaliyokuwa yamepangiwa kufanyika leo.

Hatua ya serikali ya kuregeza kamba inaangaliwa na wengi kama imetokana na shinikizo kutoka nchi za magharibi za kumtaka Zardari kumaliza mvutano wake na Sharrif pamoja na Gilani kuwaachia huru mamia ya watu waliokuwa kizuizini kama ushindi kwa wanaharakati wa haki za binadamu.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na ulinzi nchini Pakistan, Talat Masood, anasema hatua hiyo ni ushindi mkubwa kwa vyama vya kiraia, wanasheria na hata kwa Nawaz Shariff, ingawa ni hatua iliyokuja kuchelewa, lakini ni vyema kwamba imekuja kabla ya maandamano kufika mjini Islamabad.

Kwa mujibu wa Talat, hii itakuwa mara ya kwanza katika historia ya Pakistan kuwahi kuweko mahakama huru, hatua ambayo itaimarisha utawala wa kisheria.

Mchambuzi huyo wa kisiasa anasema Marekani imechukua hatua muhimu na kutambua kwamba chama cha bwana Sharif ni nguvu muhimu katika siasa za Pakistan na hakujakuweko haja ya mivutano.

Kiongozi wa upinzani, Nawaz Shariff, ameitaja hatua ya kurudishwa majaji wote kazini kuwa ni mafanikio makubwa katika historia ya nchi hiyo. Hata hivyo, kwa upande mwingine, msemaji wa jaji mkuu Chaudhry amesikika kuupokea uamuzi huo kwa tahadhari kidogo.

Amesema kumekuweko na ahadi niyngi zilizovunjwa katika kipindi cha nyuma na kusababisha hali ya kutoaminiana. Athar Minullah anasema kutokana na hali hiyo inabidi Wapakistan wasubiri na kuona ikiwa kweli ahadi hiyo itatimizwa. Jaji mkuu Chaudrhy alifutwa kazi na rais wa zamani Pervez Musharraf mnamo mwezi Novemba mwaka 2007 pamoja na majaji wengine 60 ambapo 53 kati yao walirudishwa kazini baadae.

Muahsrraf alihofia kwamba majaji hao wangetangaza kwamba hakufaa kugombea uchaguzi wa rais akiwa ni mwanajeshi. Kabla ya hapo alimfurusha kazini bwana Chaudhry mnamo mwezi Marchi mwaka 2007, lakini akarudishwa kazini kutokana na rufaa ya mahakama kuu.

Mvutano kati ya serikali na wanasheria wa upinzani na wanaharakati ambao walikuwa wakifanya kamepini za kurudishwa kazini Chaudhry ulitishia kusababisha hali tete zaidi nchini Pakistan.

Mwandishi: Saumu Ramadhan Yusuf/AFP

Mhariri: Miraji Othman