Serikali ya Umoja ya Palastina huenda ikavunjika | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 14.06.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Serikali ya Umoja ya Palastina huenda ikavunjika

Hamas wameliteka jengo laq vikosi vya usalama vya Fatah na kuidhibiti sehemu kubwa ya Gaza

default

Rais wa utawala wa ndani Mahmoud Abbas anakutana na wawakilishi wa taasisi za uongozi wa Palastina kuzungumzia mustakbal wa serikali ya umoja iliyoundwa na chama chake cha Fatah na Hamas-makundi mawili yanayopigana huko Gaza.

Rais Mahmoud Abbas anazungumza moja kwa moja pamoja na wawakilishi wa kamati kuu ya chama cha ukombozi wa Palastina na wale wa Fatah kubuni msimamo wa pamoja kuelekea serikali ya umoja na ushirikiano pamoja na Hamas.

Uamuzi muhimu unatazamiwa kupitishwa wakati wowote kutoka sasa.Hayo ni kwa mujibu wa mshauri wa rais Mahmoud Abbad,Nabil Amr.

Dhamana mwengine wa kipalastina amezungumzia uwezekano wa kuvunjwa serikali ya umoja inayodhibitiwa na Hamas.Rais Mahmoud Abbas anafikiria kweli kweli kuivunja serikali“ amesema afisa mmoja wa utawala wa ndani ambae hakutaka jina lake litajwe.

Jana chama cha Fatah kilitishia kujitoa toka serikali ya umoja,na kumfanya rais Mahmoud Abbas apitishe amri ya kutwaa hatamu za uongozi .

Hapo awali rais Mahmoud Abbas alizisihi pande zote mbili akisema:

“La mwanzo kabisa linalobidi kufanywa,mapigano lazma yasitishwe na kuacha kumwaga damu.Mapigano lazma yaakome.Nnasisitiza,nnawalaumu wote, kutoka kila upande,wanaofyetua risasi kuwauwa ndugu zao,mamoja wanatokea chama gani.”,

Hali inatisha hivi sasa huko Gaza baada ya wanamgambo wa Hamas kuliteka jengo la vikosi vya usalama vya chama cha Fatah hii leo.

Ikiwa madai ya Hamas yatathibitishwa basi hilo litakua pigo kubwa kwa vikosi vya Fatah,baada ya siku tano za mapigano mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu Hamas walipoibuka na ushindi uchaguzi wa bunge ulipoitishwa mapema mwaka jana.

Watu zaidi ya 80 wameuliwa tangu jumamosi iliyopita,wakiwemo wanamgambo,raia wa kawaida na watoto pia.

Mashahidi huko Gaza wanasema Hamas wanadhibiti sehemu kubwa ya mji huo na kuwazingira katika sehemu mbali mbali pia wanajeshi wa Fatah.

Akikabiliwa na kitisho cha kuiona Gaza ikiangukia mikononi mwa Hamas,waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert amependekeza patumwe kikosi cha kimataifa katika eneo linalopakana na Misri.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amedhukuru pia uwezekano wa kutumwa vikosi vya kimataifa katika eneo la mpakani wakati wa mazungumzo pamoja na wanachama wa baraza la usalama la umoja wa mataifa.Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa amesema alizungumza kwa simu jana usiku na rais wa utawala wa ndani Mahmoud Abbas aliyependekeza Umoja wa mataifa uingilie kati.

Jumuia ya nchi za kiislam imepinga moja kwa moja fikra ya kutumwa kikosi cha kimataifa huko Gaza.“Hatuhitaji vikosi vya kigeni.Kinachohitajika ni namna ya kuelewana vyema wapalastina wenyewe kwa wenyewe“ amesema hayo katibu mkuu wa jumuia ya nchi za kiislam EKMELEDDIN IHSANOGLU-pembezoni mwa mkutano wa jumuia hiyo mjini Kuala Lumpur Malaysia.

 • Tarehe 14.06.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CB3b
 • Tarehe 14.06.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CB3b

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com