1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Ujerumani yabana matumizi

8 Juni 2010

Je, hatua hizo zitatimiza shabaha yake ?

https://p.dw.com/p/Nkgp
Kanzela Angela MerkelPicha: AP

Hatua za kubana matumizi ilizopitisha jana serikali ya Ujerumani, ni za kwanza tu katika mkondo wa kuimarisha mfuko wa matumizi ya serikali.Bado kuna vizingiti vingi vya kukiukwa tangu ndani hata nje ya Bunge.

Ili kuzuwia kuongezeka kwa madeni ya serikali, Ujerumani, inapanga kuanzia mwakani 2011,kila mwaka kubana matumizi kwa kima cha Euro bilioni 10.Hii ni kwa muujibu wa uamuzi uliopitishwa katika kikao maalumu kilichofanyika Jumapili.Swali sasa ni je, shabaha hii ya kubana matumizi itweza kufikiwa ?

"Hatima ya serikali ya muungano ya Ujerumani" ndio mada kuu katika kikao hicho.Na hii , ilizusha wasi wasi na msisimko ambao, sasa umefungua mlango wa serikali kuvuta pumzi. Baadae, ikadhihirika kuwa, imepasi mtihani-kuwa imeifikia shabaha yake ya kubana matumizi kwa kima cha Euro bilioni 10 kwa mwaka.Unaweza kusema, hata imepindukia na kwamba , sasa hakuna mengi yatakayo kwenda kombo.

Kusema kweli lakini, sasa , ndio hasa kazi inaanza.Takriban yote yaliopitishwa katika kikao cha Jumapili na jana Jumatatu, ni ahadi tu ambazo zinabidi kugeuzwa sheria.Kwa mfano, kutozwa kodi zaidi kwa viwanda vya nishati ya nuklia ambavyo kila mwaka vichangie Euro bilioni mbili katika hazina ya serikali.

Hii ni kama fidia kwa kuruhusiwa kuendelea kufanya kazi kwa miaka 2 zaidi kinyume na ilivyoafikiwa enzi za serikali ya Gerhard Schröder.Lakini kurefusha muda huo, kunapaswa kwanza kugeuzwa kuwa sheria ; na kisheria, kuna mabishano iwapo Bunge la Ujerumani (Bundestag) pekee lina mamlaka ya kufanya hivyo.Swali linaibuka hapo iwapo, Bunge la pili la Ujerumani- Bundesrat ,halina usemi juu ya swali hilo na huko kinyume na Bundestag, serikali , haina wingi wa kura wakati huu.

Imepangwa pia ingawa kuanzia 2012 kila mwaka kutoza kodi mabenki na kodi hiyo itaanza tu iwapo kutakuwapo maafikiano kimataifa au alao barani ulaya.Haya yote , yadhihirisha hatua za kubana matumizi za serikali jinsi zilivyosimamia nguzo inayo regarega.

Ukiacha hayo, hatua za kubana matumizi zilizosalia zinatoa sura njema.Nafuu zilizotolewa kwa makampuni yanayotumia nishati nyingi zitafutwa.Ingawa kwa makampuni hayo, huo utakuwa mzigo, lakini ,ni bora kwa usafi wa mazingira.

Hatahivyo, malalamiko dhidi ya hatua hizo za kubana matumizi hayawezi kuepukwa.Na vilio vya kwanza vya kupinga vimeshasikika.Serikali itabidi pia kujizatiti kuzima malalamiko hayo ikiwa kweli yataka kuifikia shabaha yake ilioweka ya kupunguza nakisi.

Mwandishi: Stützle,Peter (DW Berlin)

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed