1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Sudan yateka jimbo la Blue Nile

4 Novemba 2011

Jeshi la Sudan limetangaza kudhibiti makao makuu ya waasi mjini Kurmuk, katika jimbo la Blue Nile, miezi miwili baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe

https://p.dw.com/p/134yv
Rais wa Sudan Omar Al BashirPicha: DW/AP

Kulingana na mtandao wa waziri wa ulinzi nchini Sudan, majeshi yake yaliingia mjini Kurmuk, wakapigana na kufanikiwa kuuteka mji huo. katika mapambano hayo, waasi kadhaa waliuwawa na wengine wengi wajeruhiwa. Waziri huyo, akizungumza kupitia mtandao wake, amesema kwa sasa mji huo uko chini ya utawala wa rais wa Sudan Omar al Bashir.

Ghasia katika mipaka ya Sudan zimesambaratisha uhusiano kati ya Khartoum na Sudan Kusini ambao bado wanapaswa kusuluhisha maswala yao ya kugawana kodi ya mafuta na mambo mengine, hasa baada ya Sudan Kusini kutia saini mkataba wa amani mwaka 2005.

Sudan Sudan People's Liberation Movement-North
Mpiganaji wa kundi la waasi la SPLMPicha: DW

Msemaji wa mrengo wa kaskazini wa waasi wa SPLM katika jimbo la Blue Nile, Sulaiman Othman, amesema waasi wameondoka mjini Kurmuk, huku kiongozi wao, Malik Agar, akiaminika kujificha huko. Msemaji huyo amsema bado wataendelea na mapambano yao dhidi ya serikali.  Othman amesema kwa sasa wameondoka mjini Kurmuk kwa sababu zao wenyewe; amesema hata kama kwa sasa serikali ya Sudan inadhibiti eneo hilo bado wapanga mbinu za kuendelea kupambana na serikali ya rais Omar al Bashir.

Jimbo la Blue Nile na Kusini mwa Kordofan liko kaskazini mwa mpaka mpya unaobakia kuwa chini ya utawala wa Sudan, lakini ni makaazi ya watu wengi waliojiunga na kusini katika vita vikali vilivyodumu kwa mda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe. Pande zote mbili mpaka sasa zimeshindwa kupata suluhu ya mgogoro wa mpaka wa Abyei uliotekwa na Khartoum mwezi Mei. Hata hivyo, waasi wamesema wametengwa kiuchumi na kisiasa na serikali ya Sudan.

Kwa upande wake, serikali ya Kartoum imewashtumu waasi kwamba wanajaribu kusambaza vurugu na kusema kuwa kamwe hawatakubali waasi waliojihami katika mipaka yao. Mapigano kati ya serikali ya Sudan na mrengo wa kaskazini wa waasi wa SPLM ulitokea katika jimbo la Blue Nile mwezi wa September, na kusambaa katika maeneo jirani ya kaskazini na Kusini mwa Kordofan ambapo huko ghasia zilianza mwezi juni.

Barack Obama im Weißen Haus zum Ende des Irakkrieges
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: dapd

Hata hivyo, Khartoum inashutumu Sudan Kusini kwa kuwaunga mkono na kuwapa nguvu waasi. Serikali ya Sudan Kusini inakanusha madai hayo. Mapigano haya ya mipaka pia yaliharibu mahusiano kati ya Sudan na mataifa ya Magharibi.  Rais wa Marekani, Barrack Obama, wiki hii alirefusha vikwazo vya kiuchumi vilivyokuwapo tangu mwaka wa 1997.

Vita ama ghasia za mara kwa mara zinazoonekana kati ya Sudan na Sudan ya ya kusini zimezua hali ya wasiwasi kuwa huenda kukazuka tena vita vya wenyewe kwa wenyewe. Umoja wa mataifa umesema kwamba eneo la Sudan Kusini ambalo bado halijajiendeleza kabisa kimaendeleo na kiuchumi kuwa na amani, ni lazima maswala ya mzozo baina ya Sudan na Sudan Kusini yawekwe wazi na kusuluhishwa.

Mwandishi Amina Abubakar/RTRE/DPAE

Mhariri Othman Miraji.