1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya mseto ya Kiev yavunjika.

Mtullya, Abdu Said3 Septemba 2008

Rais Viktor Yushchenko atishia kuvunja bunge na kuitisha uchaguzi baada ya serikali ya mseto kuvunjika nchini mwake.

https://p.dw.com/p/FAnb
Rais Viktor Yushchenko wa Ukraine.Picha: AP

Serikali ya mseto nchini Ukraine imesambaratika kutokana na mvutano baina ya rais Viktor Yushchenko na waziri wake mkuu Yulia Tymoshenko . Rais Yushchenko alitangaza hatua ya kuvunja serikali hiyo mapema leo na pia ametishia kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi.


Rais Yushchenko amemlaumu waziri wake mkuu kwa kusababisha kuvunjika serikali hiyo kutokana na waziri mkuu huyo kushirikiana na mahasimu wa rais ikiwa pamoja na chama cha aliekuwa waziri mkuu bwana Viktor Yanukovich na chama cha kikomunisti.

Rais Viktor Yushchenko, amesema chama cha waziri mkuu kiliungana na upande wa upinzani katika kupitisha sheria ya kupunguza mamlaka ya rais na badala yake kumwongezea waziri mkuu mamlaka hayo.

Lakini waziri wake , mkuu bibi Tymoshenko amejibu kwa kusema kwamba serikali imevunjwa na rais Yushchenko mwenyewe.

Rais Yushchenko na waziri mkuu wake bibi Tyimoshenko wamekua wanatofautiana juu ya karibu sera zote tokea mama huyo aanze kushika wadhifa huo.

Waziri mkuu huyo, pamoja na Rais Yushchenko na aliekuwa waziri mkuu wa hapo awali bwana Yanukovich wanatarajiwa kupambana katika uchaguzi wa rais unaotazamiwa kufanyika nchini Ukraine katika kipindi cha miezi 16 ijayo.

Kwa mujibu wa katiba ya Ukraine vyama vilivyounda serikali ya mseto vina muda wa siku kumi ili kuweza kuondoa tofauti zao na kufufua serikali na ikiwa vitashindwa, basi bunge litakuwa na muda wa siku 30 ili kuweza kuunda serikali mpya . Baada ya hapo rais atakuwa na haki ya kuitisha uchaguzi.


Wadadisi wa kisiasa wamesema, ikiwa uchaguzi ungelifanyika sasa,chama cha rais Yushchenko kingelipoteza viti. Kura za maoni pia zimethibitisha utabiri huo.